Je unalijua hili?

11:38:00 AM Unknown 0 Comments

 
JE UNALIJUA HILI?
Ili kufanikiwa katika jambo lolote; liwe kubwa au dogo, inahitajika nidhamu; pia ili kutunza mafaniko ya jambo hilo ulilolipata kwa sababu ya nidhamu uliyokuwa nayo wakati unaanza, unahitaji nidhamu pia. Hakuna mafanikio ya kweli yasiyohitaji nidhamu dhabiti.  Nioneshe mtu aliyefanikiwa; nikuoneshe mtu mwenye nidhamu katika njia yake. Ni nidhamu ndiyo inayoleta mafanikio; Ni nidhamu ndiyo itakayotunza mafanikio hayo.

Mchezaji wa mpira wa kikapu kwa jina Michael Jordan, alikuwa akiamka alfajiri na mapema na kwenda uwanjani peke yake, ili kufanya mazoezi. Wakati vijana wa umri wake wamelala, yeye alifanya mazoezi.  Alijua kuwa hawezi kuwa bora katika kikapu “basketball” endapo atafanya mazoezi kwa kiwango na kiasi cha muda ule ule sawa na watu wengine. Nidhamu yake ilikuwa ya hali ya juu. Kwa sababu ya nidhamu hii, jina lake linatajwa katika kila kona, kama shujaa wa mpira wa kikapu ulimwenguni. Watu wengi hutamani kuwa na mafanikio kama yake; lakini hawako tayari kulipa gharama ya kuwa na nidhamu aliyokuwa nayo. Nioneshe mtu mwenye nidhamu, nikuoneshe hatima yake.

Watu wakuu hawakufikia kilele cha cheo kwa sababu walikimbia (hawakuwa na uwezo kuliko wengine); bali wakati wenzao walipolala wao walipanda juu” (kitabu cha uongozi wa Kikristo, Oswald Sanders, msisitizo umeongezwa)

Kama ungejua mambo uliyoyapoteza katika maisha kwa sababu ya usingizi [uliopitiliza], ungeshangazwa sana” (Pastor Chris Oyakhilome, msisitizo umeongezwa)

Nidhamu ni uwezo na nia ya kujitawala na kujiongoza; kuamua kujiwekea mipaka, kujinyima, kujikatalia na kujizuilia mambo yanayoonekana kuwa mazuri sasa ili kupata yaliyo bora zaidi kesho. Ni muhimu kujiwekea viwango (standards) vya maisha na kuvisimamia, lazima kujijengea uwezo wa kuwa na msimamo ulio dhabiti; na kusimamia maamuzi yako ili kufikia mfanikio ya malengo uliyojiwekea.

Je unajua gharama ya kutokuwa na nidhamu [discipline /self-control]? Gharama ya kutokuwa na nidhamu ni kuharibu maono na ndoto zako. Hata kama tutakuwa na malengo, pamoja na mipango mizuri, hasa katika mwanzo huu wa mwaka; kama hatutachagua kujenga nidhamu dhabiti; ni sawa na mtu anayekimbia haraka ili kuwahi mahali asipopajua.

Njia ya mkato inatajwa kuwa chanzo cha ukosefu wa adabu na nidhamu. Badala ya mazoezi watu wanatumia dawa za kuongeza nguvu michezoni kama njia ya mkato. Badala ya kusoma watu wanaiba vyeti kama njia ya mkato. Badala ya subira watu wanaingia katika tabia chafu kama njia ya mkato. Ni kweli, easy way is the source of all immoral behavior! 
Kumbuka; kusoma Neno la Mungu kunahitaji nidhamu, Kuweka akiba kunahitaji nidhamu, kuamka mapema kunahitaji nidhamu, mahusiano bora yanahitaji nidhamu, matumizi bora ya muda yanahitaji nidhamu, kusoma kunahitaji nidhamu; ili kufikia malengo na mipango yako uliojiwekea unahitaji nidhamu pia…kwa kifupi, hakuna jambo lenye kufaa  ambalo nyuma yake hakuna nidhamu iliyojengeka ili kufanikisha jambo hilo.


0 comments :