Usikasirike Unapohuzunishwa

12:26:00 PM Unknown 0 Comments

 
USIKASIRIKE UNAPOHUZUNISHWA
(ASUBUHI NI FURAHA)
Mara nyingi katika mazingira yetu ya kazi au katika mahusiano yetu na wenzetu ni rahisi kuhuzunishwa. Wakati mwingine tunahuzunishwa kwa sababu mfumo wetu wa vipaumbele na thamani [Priority and Value systems] umetofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Lile ambalo ni kipaumbele kwako linaweza lisiwe la thamani/kipaumbele kwa mtu mwingine, hata hivyo bado kila mtu atapaswa kuheshimu vipaumbele vya mwingine.

Pamoja na hayo, watu ni muhimu kwetu, hatuwezi kuwa kamili kama hatutakubali kuishi maisha ya jumuiya kwa namna moja au nyingine. Watu ni muhimu kwetu; Unaweza kukaa bila mke au mume lakini si kukaa bila ya jamii au bila ya ushirika na watu kwa namna moja au nyingine. Ukijua umuhimu wao hata wakikuudhi utatafuta kuwa na amani nao. [1 Wakorintho 12:25]

Wakati mwingine jambo zuri linalotarajiwa linapozidi kuchelewa, mtu huweza kuhuzunika na kuugua moyo. Ni vema tukumbuke kuwa, Mungu ni Mungu wa nyakati zote na kamwe hafungwi na muda. Wewe una hofu inayoletwa na muda lakini Mungu anakuhofia wewe kwa kuwa uwathamani machoni pake. Mungu ni wa milele, kwahiyo muda si kikwazo kwake.

Mtoto aliyechelewa kwenda shule anaweza akavuka barabara pasipo kuchukua tahadhari ya kutosha. Kwa mtoto muda ni muhimu; kwa mzazi wake mtoto ni muhimu. Mungu anajua umuhimu wako, japokuwa wewe unaangalia sana muda wako. Kumbuka; Mungu hajishughulishi na jambo lolote ambalo halijakamilika katika mtazamo wa neno lake [He is not God of Premature issues]. Kwetu sisi tunaweza kuona kwamba jambo hilo limeiva; lakini kwa Mungu laweza kuwa bado kabisa. Kutii neno lake na muda wake, ni vema kuliko kujali wakati wetu.

Wana wa Israeli walikaa utumwani Misri zaidi ya miaka 400. Inawezekana wako walioanza kuhuzunishwa na mateso waliyoyapata tangu siku ile walipoanza kutendewa vibaya. Lakini Mungu hakutoa hukumu kwa Farao na Wamisri kwa haraka. Mateso yalipozidi ndipo Mungu alimpomtafuta Musa ili kuwaokoa watu wake, kwa udhihirisho wa Nguvu kuu na ushuhuda mkuu.

Huwa natiwa moyo na maneno ya Henry Ward Beecher [1813-1887] anasema, “Our best successes often come after our greatest disappointments” yaani, “Mara nyingi, Mafanikio yetu makubwa hutokea baada ya kuhuzunishwa sana”. Israeli walipolia na kuhuzunishwa juu ya watesi wao ndipo BWANA aliposikia na kuwajilia kwa mkono wa Musa.

Mzaburi naye amewahi kusema, “Huenda kilio [huzuni] huja kukaa usiku [mmoja], Lakini asubuhi huwa furaha.”Zaburi 30:5 [Msisistizo umeongezwa]; akiwa na maana kwamba, picha pekee tunayoipata pale tuonapo giza limetanda sana ni kwamba asubuhi imekaribia. Hakuna muujiza kama hakuna changamoto; mambo kuonekana hayako sawa, bila ya magonjwa, kifo, kuachwa, kufukuzwa kazi na kuanguka; si tu kwamba hakuna muujiza bali ni wazi kusingelikuwepo hata na muujiza mmoja

Njia yetu inaweza kuwa si nyepesi; hata hivyo hatutakata tamaa katika kutenda mema. Endelea kupendeza, endelea kuvumilia, endelea kung’aa, endelea kuwa mtanashati kwa nje na hata kwa mapambo ya moyoni kwa maana asubuhi yako ii karibu.

Napenda ukweli huu toka kwa Mhubiri T.D Jakes, “Enjoy the journey not destination” akimaanisha, “Furahia safari yako na si hatima ya safari yako”. Furahia changamoto zako; zifanye changamoto zako kuwa ngazi ya kufikia mafanikio yako; changamoto ziwe chachu ya kujifunza zaidi, kumsogelea Mungu zaidi katika sala, na kukujengea mwenendo bora zaidi [character]; na endelea kufurahi katika Bwana.

Mpaka wiki Ijayo, Shalomu, amani!!!!

0 comments :