Yanayo Ondoa Furaha Yetu
YANAYO ONDOA FURAHA YETU
Yako
mambo mengi yanayotuondolea furaha na kutujaza mioyo yetu huzuni kuu. Kuyajua mambo hayo ni ufunguo kuelekea furaha
ya kweli. Mambo hayo ni pamoja na dhambi. Dhambi hufanya tujisikie vibaya, toba
ya kweli huturejeshea furaha hiyo. Kama tunataka nyakati za kubarizi katika
uwepo wa Mungu ni lazima tutubu; Mungu ameahidi kwa kinywa cha mtume Petro
kwamba tukitubu tutapata burudiko la moyo.
“Tubuni basi,
mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako
kwake Bwana;” Matendo ya Mitando 3:19 Ahadi gani nzuri kama hii? Ningekuwa
na kalamu ningeandika pembeni ya mstari huu, “I can’t miss this promise”.
Burudani itarajea baada ya toba, uchungu na mgandamizo wa mawazo vitatoweka
tukitubu. Yanayoondoa furaha yetu ni mengi, lakini toba ni mlango wa pekee wa
kurejesha furaha.
Fyodor
Dostoevsky ni Mrusi aliyeacha alama ya aina yake, maneno yake yamejaa mafunzo.
Katika moja ya kauli zake anasema, “The greatest happiness is to know the
source of unhappiness” kwa tafsiri isiyo rasmi, “Furaha kuu ni kujua
chanzo cha mambo yanayotuhuzunisha”. Ukishajua nini chanzo cha huzuni yako basi
huna budi kujitahidi kukifunga chanzo hicho.
Wakati
mwingine tunagubikwa na huzuni kwa sababu ya kuficha siri ambazo zinatuumiza
sisi wenyewe, hakikisha unatumia hekima kutoka katika kitanzi hicho. Wakati
mwingine ni uhusiano usio afya; nao pia si wa kuulea sana.
Ni
kweli kabisa, hatuwezi kukwepa maumivu ya kukosa uadilifu au huzuni ya
udhalimu. Ni ama uingie gharama ya kuwa mwadilifu na mwaminifu au uingie
gharama ya kuwa dhalimu na asiyeaminika. Kukimbia dhambi ni gharama, lakini
kutenda dhambi na kukaa nayo ni gharama kubwa zaidi.
Watu
wengi wenye dhambi hawapendi kusali. Ninapata funzo kubwa katika Luka 18:13
ninaposoma kwamba mwenye dhambi alikwenda kusali na Mungu akajibu sala yake. Ni
jambo zuri mno kwamba, Mungu huwasikiliza hata wadhambi. Ikiwa Mungu
huwasikiliza hata waovu basi tunataraji kuona dunia nzima ikisali.
Tatizo
si dhambi, tatizo ni kutokwenda kusali; tatizo ni kutokumwendea Mungu. Wenye
makosa wengi hawapendi kusali na ni ujanja wa shetani kwani anajua wakisali
Mungu atawasikia na kuwasamehe. Twendeni tukasali, twendeni tukaombe toba. Wito
wa toba si wito kwa watu binafsi tu, bali ni wito kwa makanisa, taasisi za
kiraia, mashirika, mataifa na dunia nzima, sote tunahitaji kutubu.
Inawezekana
umekosea, unahuzuni na unaogopa kusali tafadhali leo naomba tusali pamoja.
Nalifurahi Yesu aliposema mtoza ushuru mwenye dhambi alikwenda kusali [Luka
18:10na 13]. Oh! akatoka amesamehewa na amejibiwa. Mpendwa usikate tamaa amua
kusali leo. Nikualike useme maneno haya kwa imani kama mwanzo wa sala yako leo:
“ BWANA YESU WEWE UMEWAKUBALI WAKOSAJI NA MIMI UNANIKUBALI. NAOMBA UNIREHEMU
KWA DHAMBI ZANGU ZOTE AMBAZO NIMETENDA. NINA KIRI WEWE NI BWANA NA NINAAMINI
MUNGU ALIKUFUFUA KUTOKA KWA WAFU” AMINA.
0 comments :