Umuhimu wa kutambua kusudi - III
“Moyo wa mtu hufikiri njia yake;
Bali Bwana huziongoza hatua zake” Mithali 16:9
Katika biblia tafasiri ya kiingereza
[NIV] mithali 16:9 inasema, “Moyo wa mtu
hupanga mipango yake ili kufikia malengo yake, lakini Bwana huongoza hatua
zake” (Tafsiri ya mwandishi). Hii inatupa kufahamu kuwa jukumu la
kupanga mipango ili kufikia malengo fulani katika maisha yetu ni jukumu la mtu
binafsi. Mpaka tumekuwa na mipango dhabiti katika kufikia malengo tuliyonayo, Mungu hataongoza hatua
zetu ili kufikia malengo hayo.
Akielezea umuhimu wa kuwa na
mipango, na jinsi ambavyo Mungu huongoza hatua zetu ili kufikia malengo, kutimia
kwa ndoto/maono, katika maisha ya mtu; mwenyehekima mmoja amewahi kusema, “Ni vigumu kuongoza meli iliyosimama”.
Mtu mwenye malengo au ndoto/maono katika maisha yake lakini hana mipango
dhabiti ya kufikia jambo hilo, ni kama meli iliyosimama; hakuna namna nahodha
ataweza kuiongoza meli hiyo; na hivyo hakuna namna meli hiyo itaweza kufika
mwisho wa safari yake.
Jambo moja muhimu napenda ukumbuke;
Kabla ya mipango hutangulia malengo. Malengo ni mambo unayotaka kuyafikia
katika kipindi cha muda fulani; Mipango ni hatua na njia za kupita ili kufikia
malengo hayo. Watu wengi wanashindwa kufanikiwa, si kwa sababu hawana uwezo wa
kufanikiwa; ila ni kwa sababu hawajui wanataka kufanikiwa katika jambo gani
hasa [specific targets]. Mtu asiye na malengo ni sawa na msafiri anaye safari
kwenda mahali kusipojulikana. Mpaka
umekuwa na malengo mahususi, hauwezi kuwa na mipango dhabiti ya kukutoa hapo
ulipo.
Nakumbuka wakati ninaanza mwaka
2015, mojawapo ya malengo niliyokuwa nayo ni kuhakikisha ninasoma angalau
kitabu kimoja kipya kila mwezi; na nikaweka mipango/mikakati ya kufikia lengo
hilo. Mpaka mwaka unaisha nimefanikiwa kutimiza na kuvuka lengo hilo la kusoma
angalau kitabu kipya kila mwezi; hii ni mbali na machapisho mbalimbali
ninayosoma; ambapo kwa ujumla imeongeza maarifa, ufahamu, hekima na kupanua
uelewa wangu juu ya mambo kadhaa.
Kumbuka jambo hili; Ili kuishi
maisha yenye ufanisi, ni muhimu kwa malengo yako kuendana na ndoto zako au
maono au kusudi la Mungu juu maisha yako.
Kama mojawapo ya malengo yako
katika mwaka huu ni kuongeza au kukuza uhusiano wako na Mungu, au kujijengea
tabia na mwenendo fulani wa kimaisha au kurudi shule au kusoma hadi kufikia
ngazi fulani, kuanzisha biashara/jambo fulani au kuboresha mahusiano yako
katika eneo fulani; weka mipango ya kufikia lengo hilo.
Mipango ni kama malighafi za
kutengenezea bidhaa [malengo], tunapoanza mwaka huu mpya amua kupanga mipango
na kuiweka mipango hiyo mbele za Mungu; na mwisho wa yote utapata bidhaa kamili
yaani kufikia malengo/ndoto na maono uliyonayo ndani yako kwa mwaka huu
[Mithali 16:3].
Unapokuwa na malengo pamoja na
mipango dhabiti; inakuwezesha kuweka vipaumbele vyako vizuri juu ya matumizi yako
ya fedha, rasilimali ulizonazo, muda wako na aina ya watu unaotaka kutumia nao
muda wako; kama mtu hakusaidii kufikia malengo yako ni vizuri ukapunguza
matumizi ya muda wako kwake.
Kumbuka; watu
wanaosafiri kwenda mahali kusikojulikana hupenda kusafiri pamoja na watu
wengine; watu wasiotaka kufikia malengo yoyote katika maisha yao, hupenda kila
mtu afanye kama wao.
0 comments :