Utamaduni wa Yesu
UTAMADUNI WA YESU
(JESUS CULTURE OF WORSHIP)
Utamaduni
wa Yesu Kristo ni kuabudu. Katika siku zake hapa Duniani Yesu alijijengea
kasumba ya kuabudu mara kwa mara. Wanaoabudu sanamu wanafanana na sanamu, na
wanao mwabudu Mungu hufanana na Mungu. Kwa jinsi tunavyomwabudu Mungu zaidi
ndivyo tunavyofanana naye zaidi. Si
ajabu ndio maana Yesu alifanana na Baba yake wa mbinguni. Nawaonea huruma
wanaoabudu sanamu; fedha, muda, watu au vinyago kwa kuwa mwisho wa siku
watafanana na sanamu zao, “Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia.”
Zaburi 115:8
Ni
saa kumi na mbili jioni namaliza kutafakari. Mawingu ni ya bluu kidogo na hali
ya hewa ni tulivu. Jua linaanza kuzama na mwangaza wake unafifia. Japokuwa kule
kwetu Mpanda ni joto, lakini wakati jioni hali huwa ni rafiki. Na mara namwita
kwa sauti mpwa wangu, “Benjamini, Benjamin, twende.” Tabiri, tunataka kwenda
wapi na Benjamini? Tunakwenda mlimani mahali ambapo watu ni wachache, huko
tutamwabudu Mungu na kumshukuru. Tunadumisha utamaduni wa Yesu ambao ni kuabudu.
It was His dominant culture to worship
God.
Zamani
za kuhani Eli, Elkana wa Rama alikuwa akienda kuabudu kila mwaka. Alikwenda
kila mwaka kwa kuwa zama zile watu walikwea kwenda mbali sana kuabudu. Walikuwa
wakiabudu milimani tu ama Yerusalemu tu na hivyo ililazimu safari ndefu. Lakini
sasa tunamwabudu Mungu katika roho na kweli, tunamwabudu mahali popote na muda
wowote. “Na mtu huyo alikuwa akikwea
kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi
dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani
wa Bwana, walikuwako huko.” 1Samweli 1:3
Leo
hii hatuendi mlimani wala Yerusalemu. Tunamwabudu Mungu barabarani, chumbani,
kanisani, ofisini hata vitandani mwetu. Tunapofanya kwa utukufu wake maana yake
tunamwabudu Mungu. Unaweza kumwabudu Mungu wakati wowote iwe ni katika kusoma
au wakati unakula chakula. [1Kor 10:31]
Je,
unataka kufanana na Mungu? Hakikisha unamwabudu na unamshukuru. Je, unatabia ya
kuabudu? Unaweza kuamua kujijengea tabia ya kuabudu; na ni rahisi, tabia ni
mazoea, mazoea hujengwa kwa kutenda jambo kwa kurudia rudia. Unamshukuru Mungu
asubuhi, mchana jioni hata usiku.
Kwa
kuwa Mungu ni mkuu ni vema ukapiga magoti na kumwangukia, ukijua wazi kwa njia
hiyo unafanana naye. Ametutaka tumwabudu akijua kwa njia hiyo atatuinua. Tafadhali mwabudu leo. Amani ikae na waabuduo halisi na watu wote
waseme Amina!
0 comments :