Ongeza ufanisi ......
ONGEZA UFANISI WAKO KUPITIA VIPAUMBELE
Uwezo
wa mwanadamu unakikomo chake katika kila afanyalo. Ndio maana kuweka vipaumbele
ni jambo la msingi. Nguvu za mwanadamu ni kidogo, hawezi kufanya vizuri kila
kitu kwa wakati mmoja. Hawezi kuwekeza katika kila mradi. Hawezi kumfikia kila
mtu. Kwa kuwa pesa tulizonazo ni kidogo, muda nao hautoshi na watu tulionao
wanamajukumu mengi ndio maana tunahitaji kuweka vipaumbele.
Ni
muhimu kuwa na kipaumbele katika wito na Kusudi tuliloitiwa na Mungu. Usain
Bolt mkimbiaji kutoka Jamaika ni mmoja wa watu waliofanikiwa sana kwa sababu ya
kujua kusudi na hivyo kuweka vipaumbele. Badala la kuwekeza katika mpira wa
miguu na riadha baba yake alimtaka adumu katika riadha tu, yaani, achague moja.
Alimsisitiza: “Usain my son you belong to the running tracks”
“Muda ni bidhaa pekee inayochacha haraka kupita mboga yoyote ile unayoifahamu. Muda ukipoa (ukipita) hakuna kuchemsha kama mboga, ni rasimali isiyorejesheka.”
Ni
muhimu kuwa na vipaumbele katika mawasiliano, katika kazi, katika fedha na
katika muda. Vipaumbele huamua kwa nani na kwa ukubwa gani rasilimali zako
zitatumika. Kila alichonacho mwanadamu hakitoshi mpaka pale anapoamua kuwa na vipaumbele.
Watu wote wana saa 24 lakini si wote wanatumia saa 24. Wengi wanatazama saa 24
zikienda, au wanawatazama wenzao jinsi wanavyotumia saa 24 za siku. Kila
unapotazama filamu, unaposikiliza vituo vya redio lazima ujue, unamtazama
mwenzako akifanya wakati wewe unapoteza muda. Muda ni bidhaa pekee inayochacha
haraka kupita mboga yoyote ile unayoifahamu. Muda ukipoa (ukipita) hakuna
kuchemsha kama mboga, ni rasimali isiyorejesheka. You cannot restore (recycle)
time once wasted.
Kwa
leo tunazungumzia sana pesa, ni muhimu tukajua vipaumbele vyetu vinavyohusiana
na pesa kwa mujibu wa biblia. Mwana mpotevu alipochukua pesa hakuwa na
vipaumbele, ila anasa tu. Biblia inasema, “akatapanya mali kwa maisha ya anasa.”
Angeweza kutumia pesa zake kufungua makanisa, pia anagaweza kuziwekeza katika
miradi ili ziongezeke, bali yeye akajitafutia makahaba akatapanya. Wengine wanatafuta pesa, wengine wanazo na
hawajui kutumia.
Vifuatavyo
ni vipaumbele vya pesa kibiblia:
Moja, Pesa ni kwa ajili ya chakula. Kila
unaponunua chakula au unapowapa watu chakula unafanya matumizi mazuri,
“Imenenwa wapeni watu chakula.” Mungu akitupa pesa anajua ametupatia kifurushi
chenye chakula cha roho na mwili, maji, elimu, teknolojia, maarifa, uzima na
msaada. Pesa na matolea lazima yapelekee uwepo wa neno la Mungu la kutosha
katika makanisa na katika mikutano. Imenenwa, “Leteni zaka kamili ghalani ili
chakula cha kutosha (neno la Mungu) kiwemo katika nyumba yangu, asema BWANA.”
Nabii Isaya naye alinena kwa habari ya pesa na wapi itumiwe. Alitaka iende
kwenye chakula kinachoshibisha. Mambo ya anasa huleta kiu zaidi (addiction)
badala ya utoshelevu. Ndio maana si vizuri kununua pombe, sigara au kuwekeza
katika zinaa. “Kwani kutoa
fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu
kisichoshibisha?... ”Isaya 55:2a
“Tutoapo fungu la kumi la pesa au mazao, ni fungu la kumi la nguvu zetu zilizotumika kuzalisha kiwango hicho cha pesa. Mungu ndiye atupaye nguvu”
Pili, Pesa ni
kwa ajili ya kumwabudu Mungu. Huwezi
kuabudu pasipo sadaka. Imeandikwa, “Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko
ya mazao yako yote.” Mithali 3:9. Nilipokuwa mdogo nilipewa pesa ili nikatoe
sadaka, wengi wetu tunapenda mtindo huu usio na baraka sana. Daudi
alikataa vitu vya bure, alisema hawezi kwenda kutoa vya kupewa na akaamua
kulipia gharama. Tutoapo fungu la kumi la pesa au mazao, ni fungu la kumi la
nguvu zetu zilizotumika kuzalisha kiwango hicho cha pesa. Mungu ndiye atupaye
nguvu. We need money for worship.
Tatu, Pesa ni kwa ajili ya kununua
maarifa. “Naam, kwa mapato yako yote jipatie
ufahamu,” Mithali 4:7b. Ni kazi bure kuwa na pesa na ujinga.
Kuwekeza katika elimu na maarifa ya kiroho ni jambo la msingi. Kama hununui
vitabu, husomi vitabu; tena wala huwekezi katika elimu, kwa kweli bado hujaanza
kuishi. Kama pesa haikuletei akili basi inakuletea ujinga, na hapa lazima uwe
upande mmoja. Ama ujinga au maarifa. Kwa mjinga ni rahisi kutumia pesa kujiua,
biblia inasema, “Kufanikiwa kwao
wapumbavu (wasio na maarifa) kutawaangamiza.” Mithali 1:32b
Nne, Pesa ni kwa ajili ya kusaidia
wengine. Huwezi kutoa usichokuwa nacho, kama hatuna pesa hata kama
ni wakarimu tutaonekana wachoyo. BWANA Yesu alisema, “Ni heri zaidi kutoa
kuliko kupokea.” Na hapa kuna pande mbili mtoaji na mpokeaji, Yesu amesema
unaheri upande wa mtoaji kuliko ule wa mpokeaji. Mara zote mpokeaji ndiyo
huamini amebarikiwa, anaweza hata kufanya maombi ya kushukuru. Lakini Yesu
anasema mtoaji hubarikiwa zaidi, ukiweza kutoa unathibisha kwamba umebarikiwa. Rafiki
unapenda kuwa upande gani? Nadhani sote tunapaswa kuwa upande wenye heri ambao
ni wa kutoa au wa mtoaji. Basi na tutafute pesa kwa njia halali ili tuweze
kutoa. “Usimwambie
jirani yako, Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; Nawe unacho kitu kile
karibu nawe.”Mithali 3:28
“Mungu alijua akitupa akili hatutapungukiwa na chochote hata kama haturuki kwa mbawa. Tumia akili, acha ndege waruke mpaka shambani bali wewe ruka mpaka miaka 10 au 20 ijayo kupitia uwekezaji.”
Tano, Pesa ni kwa ajili ya
uwekezaji. Kuwekeza katika hisa, katika kilimo, ardhi na biashara ni
jambo la msingi na la muhimu. Katika biblia tunasikia kwa habari ya kabaila
ambaye kwa lugha ya leo anaitwa, mwekezaji. Mwekezaji ni mtu anayetumia pesa
leo ili imtumikie kesho. Anataka baada ya kitambo apate pesa bila kufanya kazi.
Uwekezaji katika miradi ya muda mrefu ni uwezo wa kuona mahitaji ya kesho
tukiwa leo. Uwekezaji huleta mategemeo na matumaini yenye uhakika kwamba, pesa
itaingia (we expect cash to inflow). Ni tofauti na ndege ambao nao wana mfumo
wao waliopewa na Mungu. Ndege hawana mashamba lakini wana mabawa ambayo
huwarusha na kuwaingiza shambani, mwanadamu ana-akili ambayo ni zaidi ya
mabawa. Mungu alijua akitupa akili hatutapungukiwa na chochote hata kama
haturuki kwa mbawa. Tumia akili, acha ndege waruke mpaka shambani bali wewe
ruka mpaka miaka 10 au 20 ijayo kupitia uwekezaji. “Invest don’t plan spend and squander”
Kimsingi
kila pesa yako inapotumika katika mambo haya matano haufanyi anasa. Nje ya haya
inaweza kuwa anasa, japo si rahisi kukuandikia kila kitu. Huwezi kuwa mchoyo
kama huna cha kutoa, ukiwa nacho na usipotoa ndipo huitwa mchoyo. Pesa si tu
kwamba itafafanua vipaumbele vyako, bali pia itaifunua tabia yako ili ionekane
dhahiri. Pesa ni, “amplifier” hukuza tabia ili ionekane wazi kwa watu. Mkarimu
akiwa na pesa ataonekana sana, mchoyo akipata pesa ataonekana pia. Kule mtaani
wanasema, “pata pesa tuijue tabia yako, kosa pesa tuijue tabia ya mkeo”
Tabia
yawezwa kuchagizwa na pesa lakini bado msingi wa tabia njema ni Roho Mtakatifu.
Tangu kale hata sasa Roho Mtakatifu amekuwa msingi wa matokeo mazuri ya kitabia
ya wale wamwaminio Kristo. Tabia ni tunda, hukomaa na kuiva kwa kadiri watu
wanavyodumu katika Kristo Yesu. Usikate tamaa, hakuna tunda linalo komaa kwa
siku moja, yote hupitia mchakato wa kitambo kirefu. Naamini baada ya miaka
kadhaa mwenendo wako utakuwa wa kumpendeza Mungu. Hata Ibrahimu hakubadilika kwa siku moja,
ilipita miaka kabla ya kuenenda kwa ukamilifu. “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu,
utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”
Wagalatia 5:22