Utajiri wetu katika Kristo Yesu
UTAJIRI WETU KATIKA KRISTO YESU
(Waefeso1:17-23)
(Waefeso1:17-23)
Biblia
imeweka wazi kwamba, watu wamjuao Mungu
wao watatenda mambo makuu. Ufunguo wa maisha yenye ufanisi upo katika
kupata maarifa, ufahamu na kujua hekima ya jinsi itupasavyo kuenenda ili kuishi
maisha ya ushindi katika Kristo Yesu. Ili kuona na kuishi ushindi katika maisha
yetu ya kila siku itategemea na kiwango cha maarifa na ufahamu wetu juu ya
“siri” za ufalme wa Mungu. Hakuna njia ya mkato katika hilo. [Mithali 4:7-9]
Mara
kadhaa utasikia wapendwa wakisema “shetani kajiinua”, swali ambalo huwa
nawauliza watu wengi kila mara ninapopata nafasi ya kuzungumza nao juu ya
Habari za Ufalme wa Mungu ni kwamba, wakati shetani anajiinua, Mungu
wao huwa anakuwa wapi? Inasikitisha kuona watu wa Mungu wanakuwa waathirika
(victims) wa mazingira/shetani sawa sawa na watu wasio mjua Mungu; nao
wanalalamika na kunungunika kila kukicha. Kwa sehemu kubwa hali hii inatokana
na kukosa maarifa ya Neno la Mungu.
“Ikiwa Yesu Kristo ndiye aliyekuweka huru, hakuna anayeweza kukuweka katika utumwa tena. Ikiwa ni Kristo ndiye aliyekubariki, hakika hakuna anayeweza kukulaani.”
Ukweli
ni kwamba, Mungu Baba ametuhamisha kutoka katika nguvu za giza, na kutupeleka
katika Ufalme wa mwana wa Pendo Lake. Hii ina maana kwamba, mtu akiwa ndani ya
Kristo hayupo tena chini ya himaya ya ufalme wa giza. Ikiwa Yesu Kristo ndiye
aliyekuweka huru, hakuna anayeweza kukuweka katika utumwa tena. Ikiwa ni Kristo
ndiye aliyekubariki, hakika hakuna anayeweza kukulaani. Tukiijua kweli, kweli
itatuweka huru na hakuna atakayeweza kuchukua uhuru wetu.
“Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa…” Hosea4:6
Watu
wengi wanaujua mstari huu wa Hosea 4:7 na tena wameukariri vizuri kichwani,
lakini si watu wengi wanaelewa uzito wa maneno hayo. Hakuna mahali biblia
inasema, watu wanaangamizwa kwa sababu ya uwepo wa shetani katika maisha yao.
Adui mkubwa wa mwanadamu sio shetani au mapepo. Adui mkubwa wa mwanadamu ni ukosefu
wa maarifa sahihi (Ignorance). Unaweza kukemea pepo kwa Jina la Yesu na
likamuachia mtu saa hiyo hiyo, lakini hauwezi kukemea ujinga (ignorance).
Silaha pekee ya kuondoa “ujinga” ni kwa kupata maarifa na ufahamu sahihi. Mungu
alinena kwa kinywa cha Nabii Isaya kwamba, “kwa
sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na
watu wao wenye cheowana njaa, na wengi wao waona kiu sana” Isaya 5:13
Tujifunze kwa
Joshua
Mafanikio
ya Joshua katika njia yake, hayakuwa katika mikono ya Mungu bali katika m ikono
yake mwenye. Mungu alishafanya kila kinachotakiwa kufanyika ili Joshua anaweze
kufanikiwa. Maneno haya, maana ndipo utakapoifanikisha njia yako yanatupa
kujua kuwa mafanikio ya Joshua hayakutegemea mazingira yake, jamii yake, historia
yake bali yalitegemea utayari wake katika kutenda na kufuata maagizo ya Mungu
katika maisha yake.
“Kitabu hiki cha torati kisiondoke
kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia
kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapostawi
sana” Yoshua 1:8
Wakati
Fulani nikiwa kidato cha nne nilikuwa nasumbuliwa na maumivu ya kichwa ya mara
kwa mara kwa muda mrefu, nakumbuka nikiwa kwa shangazi yangu siku moja niliamua
kupekua mavitabu yaliyokuwa yamewekwa bila mpangilio kwenye boxi, ili nione
kama nitapata kitabu cha kusoma, baada ya kupekua kwa muda nikakutana na kitabu
cha Dr. David Oyedepo, kilichokuwa kimeandikwa “Ufunguo wa Afya ya Ki-ungu”
baada ya kukisoma kitabu hicho kilichokuwa kimechakaa na kimeanza kuchanika,
ndio ulikuwa mwanzo wa kuishi maisha ya afya bila kusumbuliwa na magonjwa mpaka
leo.
“Ikiwa
tutasoma Neno la Mungu na kusiwepo na badiliko lolote katika maisha yetu basi
tunapoteza muda bure, ni sawa na kukimbiza upepo”
Mwenyehekima
mmoja amewahi kusema “The cheapest way to secure a great future is to have
great investment in knowledge” (Njia rahisi ya kuwa na maisha yaliyotukuka ni
kuanza kuwekeza katika maarifa sasa). Amua kuwekeza muda wako na rasilimali
zako katika kupata maarifa sahihi. Tenga
muda wa kujifunza Neno la Mungu, tenga muda wa kusoma vitabu sahihi visivyopingana na Neno la Mungu.
Usisome tu kama burudani au kutimiza ratiba ya kusoma biblia au kitabu, Nuia
kupata maarifa kila usomapo na jizoeze kumuomba Roho Mtakatifu ili akujalie
kupata uelewa kila usomapo. Ikiwa
tutasoma Neno la Mungu na kusiwepo na badiliko lolote katika maisha yetu basi
tunapoteza muda bure, ni sawa na kukimbiza upepo.