Si kwa kazi wala si kwa matendo mema
SI KWA KAZI WALA SI KWA MATENDO MEMA
Tumeokolewa bure
Biblia
inanena wazi wazi kwamba, tumeokolewa kwa Neema kwa njia ya imani katika Yesu
Kristo. Hakuna kazi inayoweza kutosha kumwokoa mwanadamu isipokuwa kazi ya
msalaba tu, ni ile ambayo Kristo aliitenda. Kazi ya msalaba ni kazi timilifu
hatuwezi kuchangia kitu. Iliyo kamili haihitaji kusaidiwa, Yesu alishasema
imekwisha. Hakuna namna unavyoweza kuikamilisha iliyo kamili badala yake
unapaswa kuamini tu. “Kwa maana
mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu,
ni kipawa cha Mungu; wala si kwa
matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.” Waefeso
2:8-9
“Utii wetu katika sheria za nchi unatufanya tuwe raia wema katika nchi na si raia wa Mbinguni. Tunaweza kupata uraia wa mbinguni tu kwa njia ya Imani katika Kristo Yesu.”
Matendo
mema hayaokoi bali humthibitisha mwamini. Ni lazima tujue ukweli huu, raia
mwema si raia wa mbinguni. Katika mataifa mbalimbali kuna raia wema, wanalipa
kodi kwa wakati, hawavunji sheria, wananidhamu na wanaishi vizuri na jamii zao.
Pamoja na wema wote na uzalendo wao, bado watakwenda motoni kama hawatamkubali
Yesu kuwa BWANA na mwokozi. Utii wetu katika sheria za nchi unatufanya tuwe
raia wema katika nchi na si raia wa Mbinguni. Tunaweza kupata uraia wa mbinguni
tu kwa njia ya Imani katika Kristo Yesu.
Wako
ambao kila siku huenda kuwatazama wagonjwa, wako ambao huenda gerezani
kuwatazama wafungwa na wengine wengi huwalisha masikini. Matendo haya yote
humthibitisha mwamini lakini kamwe hayataweza kuokoa. Biblia inasema, “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa
kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;” Yohana
1:12
Biblia
inasema “bali wote waliompokea Yesu Kristo” haisemi wanaokwenda kanisani,
haisemi wanaokwenda gerezani, haisemi wanaowalisha masikini, haisemi wenye
nidhamu. Je, umempokea? Kumpokea ndio dili. Matendo
yetu mema yataleta maana kama tayari tumekwisha kumpokea Kristo ndani yetu.
Swala ni moja tu, Umempokea? Anakaa kwako? Ni rafiki yako? Je, wewe ni mtoto wa
Mungu?
Hakuna
msafi, hakuna mwenye haki yake, hakuna mwenye matendo yenye kuweza kuokoa. Si
fulani tu ndiye mwenye dhambi hata wewe uu mdhambi na unamuhitaji YESU. Sote tu
wagonjwa na tunamhitaji tabibu. Mungu alinena kwa kinywa cha nabii Isaya: “Kwa maana sisi
sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama
nguo iliyotiwa unajisi; ” Isaya 64: 6a
“Inawezekana mtu ana matendo mazuri, inawezekana mtu ni mtaratibu inawezekana ni mfanyakazi katika shirika la kutoa misaada wa wahitaji, lakini pasipo kumpokea Yesu ataishia Jehenamu ya moto”
Watu wengi wanadhani wanaanza kuwa
wenye dhambi pale wanapozini, wanapoiba au wanapowaza mabaya. Lakini mawazo yao
si ya kweli sana. Mwanadamu kwa mara ya kwanza hawi mwenye dhambi kwa sababu ya
uongo, mawazo mabaya au uchawi, bali ni kwa sababu Adamu wa kwanza alitenda
dhambi [Warumi 3:23]. Hapa hata
kabla hujatenda baya lolote unakuwa mwenye dhambi kwa sababu ya dhambi ya
Adamu. Ndivyo ilivyo, ndio maana
ikanenwa kuwa, sote tumetenda dhambi. “Kwa
sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya
wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika
hali ya wenye haki.”Warumi 5:19
Hali hiyo ya kuzaliwa wadhambi
haiondoki mpaka pale mtu atakapompokea Yesu, hali hiyo ya dhambi haitamwacha
mtu mpaka pale atakapobatizwa katika Kristo Yesu. Inawezekana mtu ana matendo
mazuri, inawezekana mtu ni mtaratibu inawezekana ni mfanyakazi katika shirika
la kutoa misaada wa wahitaji, lakini pasipo kumpokea Yesu ataishia Jehenamu ya
moto. Wokovu ni zawadi, hauwezi kununua kwa matendo yako wala kwa
fedha. “Lakini Petro akamwambia, Fedha yako (jitihada/bidii) na
ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu
yapatikana kwa mali.” Matendo 8:20
Rafiki yangu tangu kale hata sasa Yesu
humwokoa mtu anayeliamini neno lake, anayekubali kwamba, hajampokea lakini
anamuhitaji. Ikiwa unamuhitaji Yesu Kristo aje kwako kama BWANA na mwokozi sema
sala hii kwa imani. “BWANA YESU KARIBU MOYONI MWANGU, MIMI NI MWENYE DHAMBI.
TAFADHALI BWANA NIREHEMU NA UNIOKOE HIMA. AMEN”
Kwa sala hiyo fupi amekupokea na
amekuja kwako, tafadhali mshukuru kwani ungeliweza kufa pasipo kufikiwa na
ujumbe huu, kwa hakika hii ndio siku aliyoifanya BWANA nasi tunaifurahia na
kuishangilia. Tuliokolewa na tuseme, fadhili zake ni za milele. Haleluyah!
Glory Haleluyah.