Mtizamo wako juu ya changamoto

3:15:00 PM Unknown 0 Comments


MTIZAMO WAKO JUU YA CHANGAMOTO
Jambo kubwa linalokwamisha watu wengi kufikia kilele cha mfanikio katika mambo mengi ni mtizamo wanaokuwa nao hasa wanapokutana na changamoto kadhaa katika maisha yao ili kufikia mafanikio hayo. Hakuna mtu anayeweza kwenda mbali zaidi ya mawazo yake na mtizamo wake [Your attitude determines your altitude].
Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu aliyepanda huko? Hakika ametoka ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu Yule atakayemwua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoa binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli” 1 Sam 17:25
Kila mtu alimuona Goliath kama kikwazo cha mafanikio katika taifa la Israeli, kwa upande wa Daudi, Goliath alikuwa njia kuelekea na kufikia  maendeleo na mafanikio yake binafsi, mafanikio ya familia yake na taifa kwa ujumla, hakumuona kama kikwazo cha mafanikio bali njia ya mafanikio. 1Sam17:25-26, 48!
Wakati kila mtu alikuwa akiogopa kuingia Kaanani wa kuhofia majitu, Joshua na Caleb waliwaambia wana wa Israeli kuwa hawa ni chakula chetu, na Mungu alimpa kuona mafanikio ya nchi ya Kaanani (Hesabu14:9). Je una mtizamo gani juu ya changamoto iliyoko mbele yako au inayohusu familia au taifa lako? Je unaona ni kikwazo cha mafanikio yako au unaona ni mlango na njia ya kuelekea mafanikio yako.
Unaona nini?
Changamoto katika ulimwengu huu si jambo la kuepukika. Mara nyingi tunapotatua changamoto moja huibuka nyingine; kuna changamoto mbalimbali katika maisha ya mtu.  Wakati mwingine tunapokutana na changamoto mtu huweza kujihisi hana msaada; na tena hakuna namna anavyoweza kutoka salama katika changamoto hiyo. Mtu anapopitia wakati mgumu, huweza kufikiri ndio mwisho wa maisha yake, au mwisho wa ndoto na mipango yake. Ukweli ni kwamba hakuna changamoto itakayo dumu milele, kila jambo ni kwa wakati tu.
Mpaka tumechagua kuona kama Mungu anavyoona, changamoto hazitakuwa njia ya kuelekea mafanikio yetu bali vikwazo. Mpaka tumechagua kuona kama Mungu anavyoona hatutaweza kusema kama Daudi, “Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauiti sitaogopa mabaya…!” BWANA alimuuliza Yeremia anaona nini, Yeremia aliona ufito lakini Mungu alilitazama Neno lake alilosema juu ya Yeremia ya kwamba atakuwa kiongozi wa mataifa na hakuna jambo litakaloweza kumzuia kufikia mafanikio hayo. [Yeremia 1:4-12]
“Kama sisi hatuamini,  yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwamaana hawezi kujikana mwenyewe”2Timotheo2:13
Hii inatupa kujua kuwa haijalisha ni jambo gani linatokea, endapo mtu atachagua kuamini Neno la Mungu juu ya Maisha yake, hakika litatimizwa. Mungu analo Neno juu ya Afya yako, familia, biashara, ndoa, masomo n.k. Ni jukumu letu kujua Mungu anasema nini katika Neno lake juu ya maisha yetu. Hakuna upande salama isipokuwa upande wa Neno la Mungu. Katika Israeli wafalme walienda vitani baada ya kujua Neno la Bwana linasema nini juu yao kwa wakati wao, Mungu aliposema waende walienda hata walipokuwa wachache kwa kuwa walikuwa na Uhakika ya kuwa Mungu atafanya yale yote aliyoyaahidi.
Daudi akauliza kwa Bwana, akasema, Je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, Fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote. Basi Daudi akaenda…” 1Sam 30:1-9
Uweza wa Mungu unafunuliwa na kuwekwa dhahiri kwetu ili kutusaidi na kutuokoa pale tunapoamini Neno la Kinywa chake. Mt. Luka anaandika, “Heri aliyesadiki, kwa maaana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana”