UTAJIRI WETU KATIKA KRISTO YESU-II

8:25:00 PM Unknown 0 Comments


UTAJIRI WETU KATIKA KRISTO YESU-II
Njia kuu ya kutambua mapenzi ya Mungu juu ya maisha yetu, ni kwa kulisoma Neno lake. Neno la Mungu linatupa fursa ya kuyajua mawazo ya Mungu na mipango yake juu yetu katika siku zetu za kukaa hapa duniani. Neno la Mungu ni kama kioo, tunachopaswa kijitizama ili kuona kama maisha yetu yanaendana na mpango wake uliowekwa wazi katika Neno hilo.
Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yao, kama vile roho yako ifanikiwavyo”3Yohana1:2
Jambo moja wapo tunalopaswa kutambua ni utajiri wetu tulionao katika Kristo juu ya afya. Ni mpango wa Mungu ulio kamili kwa watu wake kutembea katika afya njema siku zote za maisha yao. Si mapenzi ya Mungu usumbuliwe na magonjwa. Ukombozi wa mwanadamu hakuishia tu katika kukomboa roho yake, bali pia ulihusu ukombozi kwa nafsi, mwili na mazingira yake pia.
“Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti….; na kwa kupigwa kwake mliponya
1Petro 2:24
Biblia inasema kwa kupigwa kwake mliponywa, haisemi mtaponywa; hii inatupa kujua kuwa uponyaji wetu umekwisha kutolewa tayari, yaani gharama imekwisha kulipwa, hivyo magonjwa ya aina yoyote ile hayana uhalali wa kuwepo katika maisha yetu. Yesu Kristo alichukua madhaifu yetu [Math 8:17] hakuchukua udhaifu wetu ili aturudishie baada ya muda, alichukua ili kutupa fursa ya kufurahia uzima wa Mungu katika maisha yetu kwani alikufa mara moja na yupo hai kwa ajili yetu.
Ikiwa Yesu allichukua magonjwa na madhaifu yetu, sisi tulioitwa kwa Neema yake tumebakiwa na jambo moja tu nalo ni Afya, mahali ambapo ugonjwa au udhaifu umeondolewa ni jambo moja tu ambalo hubaki kutawala, nalo ni Afya dhabiti. Kumbuka, Yesu hakufa msalabani ili tu aokoe roho zetu, kifo chake kimelipia afya ya miili yetu pia ili ipate kutumika kama Hekalu la Roho wake Mtakatifu kueneza Ufalme wa Mungu hapa duniani. Kuishi bila ya kusumbuliwa na magonjwa au madhaifu katika maisha yetu hapa duniani inawezekana, shetani hakuna anachodai.
Ni kweli shetani ni mungu wa ulimwengu huu [2Kor10:4], lakini Neno la Mungu liko wazo kuwa, wewe si wa ulimwengu huu; hivyo basi shetani hana mamlaka juu yako wala juu ya afya yako. Una uhalali wa kutembea kifua mbele kwa kuwa upo katika ulimwengu ambao Yesu Kristo ndiye Mungu anayetawala, na katika Yeye hakuna magonjwa [Kolosai 1:13].
Kumbuka jambo hili, Ikiwa Yesu Kristo ndiye aliyekuweka huru, hakuna anayeweza kukuweka katika utumwa tena. Ikiwa ni Kristo ndiye aliyekubariki, hakika hakuna anayeweza kukulaani, ikiwa ni Yesu Kristo aliyechukua magonjwa na madhaifu yetu, je ni nani anayeweza kutuzuia kuwa na afya dhabiti? Tukiijua kweli, kweli itatuweka huru na hakuna atakayeweza kuchukua uhuru wetu.
Sawasawa na imani yako unapokea
.
Tunapokosa kujua utajiri tulionao ndani ya Yesu Kristo katika eneo fulani la maisha yetu, tunakuwa watumwa katika eneo hilo. Ndio maana Mungu hulituma Neno lake ili kuokoa. Biblia inasema watu “wanaangamizwa” kwa kukosa maarifa; maana yake ni kwamba “huyo” anayewaangamiza anatumia ujinga [ukosefu wa maarifa] wa hao watu wa Mungu kama mtaji wa kuwaangamizia. Watu wamechukuliwa mateka si kwa sababu ni wanyonge hawana nguvu bali wamechukuliwa mateka kwa sababu ya kukosa maarifa.   
“Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana”
Isaya 5:13
Nabii Isaya anasema, “Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani?... (Isaya 53:1-8)! Mkono wa Mungu hufunuliwa kwake yeye anayesadiki habari iliyotolewa juu ya kile ambacho Mungu amesema. Uweza wa Mungu hufunuliwa na kuwekwa dhahiri kwetu ili kutusaidia na kutuokoa, pale tunapoamini ujumbe wa Neno lake. Mpaka tumejua na kukubali mioyoni mwetu kuwa kazi moja wapo ya msalaba ni kutupatia afya dhabiti, hatutaweza kufurahia afya ya Ki-Mungu katika maisha yetu.
Naye heri aliyesadiki, kwa maaana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana” Luka 1:45
Jambo kubwa ambalo tunataka ulipate siku hii ya leo ni kwamba, Mungu anajali mafanikio ya roho yako, nafsi yako, mwili wako na mambo yako YOTE [3Yoh1:2]. Kwa kifo na ufufuko wake, una uhalali wa kuwa mzima na kuanza kufurahia uponyaji na afya kamili juu ya jambo lolote lililokuwa likikusumbua. Katika Jina la Yesu Kristo, kama ulikuwa mgonjwa uwe mzima, kwa imani pokea Afya tele tangu leo; kwa kuwa Damu ya Yesu imeshakwisha kumwagika, na gharama imeshalipwa kwa ajili yako; Na sasa ni wakati wa kuishi maisha ya Ushindi katika Kristo Yesu kama ulivyokuwa umekusudiwa tangu awali.