YEYE badala ya Wewe

11:48:00 AM Unknown 0 Comments

 
“YEYE” BADALA YA WEWE 
(Alikwenda kama mwakilishi, kwa ajili yako) 
Watu wengi wanaposoma biblia wanadhani Adam na Eva walizeeka. Ukweli ni huu, walikufa mapema hawakuweza kudumu kabisa; kwa jinsi ya mwili waliishi miaka mingi na kuzeeka, lakini kwa jinsi ya kiroho walikufa mapema mno, kumbuka mtu ni roho, anayo nafsi na anakaa ndani ya mwili; mtu sio mwili bali roho. Siku waliyotenda dhambi, ndiyo siku waliyokufa. Ndivyo walivyoambiwa na Mungu na ndivyo ilivyokuwa. Hata sasa dhambi ni rafiki yake kifo, huwezi kwenda matembezini na dhambi na ukamuacha kifo nyumbani. Hawa ni mapacha, siku ya dhambi ni siku ya kifo. “walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” Mwanzo 2:17
Siku mtu anapotenda dhambi ndiyo siku anayokufa, uzima wa mwili unadanganya tu. Dhambi ni mbaya, mistari mingi katika biblia inayotaja dhambi, inaitaja kwa kuiunganisha na kifo (soma Methali 6:32, Warumi 6:23). Dhambi huoana na kifo. Kama ni msomaji wa biblia utakubaliana na mimi kwamba, ndoa kati ya dhambi na mauti ni imara sawasawa na shetani na kuzimu. Huwezi kutenda dhambi bila ya kukikaribia kifo. Hatua muhimu kuelekea kifo ni kuanza kutenda dhambi. Yesu alikufa kwa sababu alichukua dhambi zetu, mauti ilimpata kama mshahara wa dhambi zetu.
Mungu anachukia dhambi, chuki yake dhidi ya dhambi ni dhahiri. Chuki ya Mungu dhidi ya dhambi ni chuki ya milele. Dhambi zetu zilikusanywa mahali pamoja yaani, katika mwili wa Yesu Kristo. Kama mtu akusanyavyo takataka au uchafu sehemu moja na kisha akauchoma moto, ndivyo uasi wa wanadamu wote ulivyokusanywa katika mwili mmoja wa Yesu Kristo na kisha akafa msalabani kama fidia yetu. Maasi yote na uovu wote uliwekwa juu ya mwili wake.
Yesu ni mwakilishi wetu katika mauti, yeye badala yetu {vicarious death}. Badala ya sisi kwenda katika mauti yeye alikwenda kwa niaba yetu. Watu maalumu wanaposhindwa kuhudhuria katika hafla fulani au katika chakula cha jioni huteua wawakilishi wao. Ni rahisi kwa watu hawa wakuu kumpata mwakilishi  kwani ni suala la kwenda kula na kunywa. Lakini akitafutwa mwakilishi atakaye kwenda kufa kifo cha aibu kwa niaba yao, hakika hawezi kupatikana. Yesu hakutuwakilisha katika hafla na karamu za raha na furaha, bali alituwakilisha katika mauti naamu mauti ya msalaba na aibu. Alituwakilisha katika baridi, katika kukosa usingizi katika kuteswa na kuvuja jasho la damu, na katika kulia sana.
Kwa kitambo kirefu tulihitaji mwakilishi na hakupatikana, kwa nyakati tofauti tofauti nabii Isaya na Daudi walitamani Mungu aje na afanyike mwakilishi wetu. Walisikika wakisema, “laiti mbingu zingekuja duniani” au “laiti BWANA angepasua mbingu” walitamani kuona kile kinachoitwa kwa kizungu, ‘Heaven on Earth.’ Yaani mbingu duniani
Ombi lao lilijibiwa pale Yesu alipokuja duniani. Yesu ndiye ukamilifu wa mbingu dunian. Mungu pamoja nasi yaani, Mungu katika maisha na ratiba za kwaida kabisa za mwanadamu. Yesu ndio mbingu zote, badala ya kutazama mbinguni sasa tunamtazama Yesu aliyekuja na aliye mbingu duniani (Emanueli).
Ili uwe mpatanishi ni lazima uzifahamu pande zote zinazokinzana kwa uzuri wote. Ili uwe mkalimani ni lazima ujue lugha zote mbili kwa ufasaha, Yesu aliijua lugha ya Mungu na ya wanadamu pia. Yesu alimjua Mungu (alitoka kwa Mungu) lakini kwa kuwa alikuwa mwanadamu alimfahamu vizuri mwanadamu. Alijua namna Mungu anavyochukia dhambi (alikuwa Mungu) lakini alijua jinsi dhambi inavyomtesa mwanadamu kwa kuwa aliishi kama mwanadamu. Aliona magonjwa, hali zao ngumu za kimaisha, aliona utawala wa giza na utumwa wa dhambi. Kwa kuwa alizijua namna zote ndio maana hakulalamika kwamba mateso yamezidi pale msalabani, kwani aliijua chuki ya Mungu dhidi ya dhambi. Huwezi kujiandaa kufanya malipo kama hujui gharama au bei ya bidhaa.
Yesu alibatizwa ili aitimize haki yote. Ubatizo wa Yesu ni muhimu sawasawa na kifo chake. Alikufa kwa ajili yetu, alibatizwa kwa ajili yetu pia. Yesu hakuwa na haja ya kubatizwa, hata Yohana alitaka kukataa kumbatiza. Ubatizo wa Yohana ulikuwa ni ubatizo wa toba, Yesu hakuwa na sababu ya kutubu, hakutenda dhambi. Asiye na dhambi hana haja ya kubatizwa ubatizo wa toba. Lakini kwa ajili yako alibatizwa. “Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.” Mathayo 3:13-15
Ubatizo ndio ulikuwa mlango pekee ambao Yesu alipitishwa ili kuutwaa uovu wetu na kuitimiza haki yote. Pale mtoni alikwenda kuchukua dhambi zetu, pale msalabani alikwenda kulipia deni lililotokana na dhambi alizochukua pale mtoni-katika ubatizo. Ni baada ya ubatizo ndipo yalinenwa maneno haya: “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”Yohana 1:29
Ni muhimu kujua kwamba tu wadhambi na Yesu alituwakilisha katika kupokea mabaya. John Newton mtunzi wa wimbo wa ‘Amazing grace’ katika moja ya maandishi yake ameandika hivi: “mimi si mtu mwenye kuweza kukumbuka mambo yote lakini mambo mawili siwezi kuyasahau kwa hakika kwamba, ‘mimi ni mdhambi mkuu, na Yesu Kristo ni mwokozi Mkuu”. Ukweli huu ni muhimu kwa kila anayetaka kuwa karibu na Yesu
Mtu mmoja amewahi kusema “katika matendo yote atendayo mwanadamu, toba au kutubu ni tendo la Ki-mungu zaidi kupita yote.” Inawezekana kabisa hujazaliwa mara ya pili au bado una dhambi zinatendeka kwa siri, hakuna anayejua zaidi ya wewe; fanya uamuzi wa kuziacha leo, jikatalie ya dunia na ungana na Yesu sasa. Alikufa kwa ajili yetu, hatuna budi kuishi kwa ajili yake 2Kor5:15. Kama uko tayari basi tamka maneno haya kwa imani:
“BWANA YESU, NAOMBA UNIREHEMU MIMI MWENYE DHAMBI. NINAAMINI KATIKA UBATIZO WAKO, NINAKIRI WEWE NI BWANA NA NINAAMINI KWA MOYO KWAMBA, MUNGU ALIKUFUFUA KUTOKA KATIKA WAFU. NIPE NA ROHO WAKO BWANA ILI ANIONGOZE DAIMA.” AMINA
Hongera kwa uamuzi uliofanya, usisite kuwasiliana nasi kwa email au simu zetu, nasi tutazidi kukuombea na kukushauri.
MUNGU AKUBARIKI SANA.

0 comments :