Unayo Nafasi ........
UNAYO NAFASI YA KUANDIKA
HISTORIA YAKO
Hatakama
hatujui alipozikwa Nelson Mandela, Mama Teresa, Mwl. J. K. Nyerere, Dr. Myles
Munroe; majina yao na kumbukumbu zao haziwezi kufutika; hatuhitaji kuona
makaburi yako ili tujue kama wamewahi kuishi; kazi zao na michango yao juu ya
ulimwengu ni alama tosha. Watu kama Mt. Paul, Moses, Joshua, Daudi hawakuhitaji
msalaba wa chuma juu ya makaburi yao, wala hawakuhitaji kujengewa zege makaburi
yao ili tujue kama wamewahi kupita hapa duniani; na tena hawahitaji majina yao
kuwa juu ya majengo marefu; mahali ambapo tetemeko linaweza kuharibu. Kazi zao
na mchango wao katika kuboresha maisha ya watu katika nyakati zao ni kaburi
tosha; watu hawa wanaishi mioyoni mwetu; kwa kuwa kazi zao na kujitoa kwao
kumerahisisha maisha yetu ya sasa, na kufanya ulimwengu kuwa bora zaidi.
Watu
hawa walijua kuwa maisha yao ni dhamana, na kwamba mwanadamu anaishi mara moja;
hivyo walihakikisha wanaishi katika ubora na ufanisi wote. Walijua kwanini wapo
duniani katika nyakati zao; walijua wanawajibika kwa jamii zao na kwa vizazi
vitakavyo kuja baada yao ambao wangehitaji kujenga juu ya msingi ambao ni
mafanikio yao kama watangulizi; walitambua kuwa maisha yatakuwa na maana
watakapoliishi kusudi la kuumbwa kwao kwa kuwa msaada kwa watu wengine. Wewe pia unayo nafasi ya kuandika historia
yako, kalamu iko mkononi mwako.
Hata
mimi sitaki jina langu liwekwe juu ya majengo na kaburi, mahali ambapo mafuriko
na tetemeko vinaweza kuharibu na kufuta kabisa; na kumbukumbu yangu isiwepo
tena; nataka jina langu na kumbukumbu yangu ibaki katika maisha ya wale
niliowasaidia kufikia malengo [purpose] yao katika maisha; tetemeko na mafuriko
halitaweza kuondoa kumbukumbu hiyo.
Watu wengi wanaogopa kufa kwa sababu
hakuna jambo walilofanya duniani, linaloleta maana mbinguni. Rafiki
yangu hupenda kusema, “Ulimwengu sio hifadhi ya wanyama, mahali ambapo
hauruhusiwi hata kuacha ganda la pipi au ndizi”.
“ni katika kusudi la kuumbwa kwetu pekee ndipo tunaweza kuacha alama kwa kufanya jambo duniani litakalote maana mbinguni.”
Hivyo, kila mtu amekusudiwa
kuacha alama [legacy] duniani itakayoleta maana Mbinguni. Na ni katika kusudi la kuumbwa kwetu pekee
ndipo tunaweza kuacha alama kwa kufanya jambo duniani litakalote maana
mbinguni.
Ninapoandika
makala hii, moyoni mwangu najua, toleo hili sio la kila mtu; nashawishika
kusema toleo hili ni maalumu ili kukuhamasisha na kukutia moyo wewe unaetaka
kufanya jambo duniani litakaloleta maana mbinguni; toleo hili ni kwa ajili yako
wewe unayetaka kuacha alama [legacy] na kuwa msaada kwa kizazi chako na vizazi
vijavyo katika eneo la wito wako. Toleo hili ni kwa ajili yako
wewe unayetamani kuishi sawa sawa na kusudi la Mungu katika maisha yako; ni kwa
ajili yako wewe ambaye ndani ya moyo wako unatakama kusahihisha historia,
kwamba katika dunia hii, amewahi kuwepo mtu aliyeishi na kutimiza kusudi la
Mungu juu ya kuumbwa kwake. Hatutaki vizazi vijavyo wafikiri kuwa katika kizazi
hiki waliishi mafisadi tu, wala rushwa tu, wafanyabiashara wasio waadilifu tu,
wanasiasa wanaotumia nafasi zao vibaya tu, wanyonyaji tu wasiojali wengine; au
viongozi wasioweza kusimamia yaliyo sahihi tu.
Usisubiri uwe kila kitu ili ufanye kitu
Mama
Teresa hakuwa na fedha alipoanza kuwasaidia masikini kule India; alijua kamwe
hawezi kuwafikia masikini wote na kuwapatia huduma muhimu katika maisha yao;
hii haikumkatisha tamaa, alianza na mmoja. Huitaji kuwa millionea ili ujifunze
kutoa, huitaji kuwa Bill Gate ili kusaidia muhitaji aliyekaribu nawe; Hauhitaji
uwe Mwakasege ili utangaze habari njema ya Ufalme wa Mungu. Mother Teresa
alianza na mtu mmoja, leo hii ulimwengu mzima unazungumza habari zake; binafsi
sijui kaburi lake lilipo lakini naijua na kutambua kazi yake katika kuboresha
maisha ya wengine.
Wanatheologia
na wataalamu wa maandiko ya kale wanadai ni Veronica, aliyemfuta Yesu uso
wakati akielekea msalabani; inawezekana, kama ni mimi ningekuwa mwandishi kwa
wakati ule, nisingeandika tukio hili, inawezekana ningeandika miujiza ya Yesu
tu zaidi;
“Hauhitaji kuwa mtu fulani ili uache alama; unahitaji kuwa wewe tu ili kuacha alama duniani, itakayoleta maana Mbinguni.”
Lakini Roho Mtakatifu alihakikisha jambo hili linaandikwa ili kutupa
kujua kwamba haijalishi kitu tunachokifanya kinaonekana kuwa kidogo namna gani
na kwamba hakuna mtu anaonekana kujali sana wala hakuna mwandishi aliyeandika
habari hiyo, Kitu hicho Mbinguni hawawezi
kusahau. Maria Magdalena alimfuta Yesu miguu kwa nywele zake, kila mtu
aliyekuwa pale alisema alichoweza kusema juu ya kitendo kile, Lakini
hakukatishwa tamaa kwa maneno yao; Na Yesu alisema kitendo kile kitajulikana
duniani kwote; hata leo tunaposoma, tunatimiza unabii huo [Mathayo 26:7-13]
Hauhitaji kuwa mtu fulani ili uache alama; unahitaji kuwa
wewe tu ili kuacha alama duniani, itakayoleta maana Mbinguni. Fanya unachoweza
kufanya mahali ulipo. Usisubiri uwe kila kitu ili ufanye kitu; anza na
unachoweza kufanya mahali unapoweza kufanya. Usisubiri uwe Mwakasege wa pili,
Bill Gate wa pili. au mama Tereza wa pili.
Kama mtu anahitaji kutiwa moyo, fanya hivyo sasa, kama mtu anahitaji
ushauri au msaada ili kufikia mafanikio yake, na unaweza kufanya hata jambo
dogo, lifanye;
“Kama unaona kuna uhitaji mahali na unaweza kufanya jambo juu ya uhitaji huo, fanya; usisubiri uwe na kila kitu au uwe kila kitu.”
Kama unaona kuna uhitaji mahali na unaweza kufanya jambo juu ya
uhitaji huo, fanya; usisubiri uwe na kila kitu au uwe kila kitu. Mwenyehekima
mmoja amewahi kusema, “Tunapowasaidia wengine kupata wanayoyahitaji,
ndipo na sisi tutapata tunayoyahitaka” [Luka 6:38a]
See you at the top
0 comments :