Jizoeze kufikiri .....

4:20:00 PM Unknown 2 Comments

JIZOEZE KUFIKIRI JUU YA MATOKEO YA MAAMUZI YAKO KABLA YA KUAMUA (Zaburi 119:9)
Jambo kuu linaloleta majuto katika maisha ya watu wengi ni kukosea katika kufanya maamuzi; hasa kwenye mambo muhimu ya maisha yao. Mara kadhaa tumesikia watu wakijilaumu, “Ningejua nisingefanya nilichofanya au nisingeamua jinsi nilivyoamua”; watu hawa wanajutia matokeo ya maamuzi yao. Kama wangetambua matokeo ya maamuzi yao kabla ya kufanya maamuzi au wangepewa nafasi ya kuamua tena bila shaka wangeamua tofauti na walivyoamua hapo awali.
Hakika majuto ni mjukuu kama ulivyo msemo huu ambao umezoeleka katika masikio ya wengi. Ukweli ni kwamba katika maisha hakuna anayependa kukosea katika kufanya maamuzi hasa katika mambo muhimu yanayogusa maisha yake au maisha ya watu wake wa karibu. Mungu amekusudia kila mtu kuishi maisha yenye ufanisi na furaha; si mpango wa Mungu ukosee katika kuamua na kuishia katika majuto.
Njia mojawapo ya kukusaidia kufanya maamuzi vizuri, ni kwa kujizoeza kufikiri juu ya matokeo ya mwisho ya uamuzi wako kabla ya kuamua. Kuwa na picha ya mwisho ya matokeo ya uamuzi huo. Kuangalia kwa makini aina ya matokeo na endapo pia utakuwa tayari kuishi na matokeo ya maamuzi unayotaka kuyafanya.  Mfano; Ikiwa unajua kuwa mchumba wako sio mwaminifu au ana hasira kupita kiasi na unataka kufunga naye ndoa hapo baadaye, usiangalie kwanza kama unampenda au la, kwanza angalia na kufikiri endapo utakuwa tayari kuishi na matokeo ya yeye kutokuwa mwaminifu au kuwa na hasira kupita kiasi; kabla ya kufikiria kwamba atabadilika mkishafunga ndoa; kwa sababu kama hataki kubadilika mkiwa wachumba au marafiki, una uhakika gani atabadilika mkiwa familia?.
Matokeo mengi ya uamuzi na uchaguzi wako ni matokeo ya kudumu (permanent), ndio maana iko haja ya kuwa mwangalifu. Unaweza kuishi maisha yote bila amani, na hii ndio picha ya matokeo ya kudumu. Kama huridhishwi na matokeo ya baadae ni vizuri usiamue kwanza. Unaweza ukafumba macho sasa na ukafanya maamuzi, lakini matokeo yatakapoanza kuonekana hautaweza kufumba macho tena, na mwisho wake ni kuishi maisha yenye majuto na kujilaumu. Biblia inaweka msingi wa kutusaidia hasa inapofika kwenye kuamua, hasa mambo muhimu yanayogusa maisha yetu na maisha ya watu wengine.
Ni muhimu kuongeza umakini katika miamala ya maisha yetu, kwani tunaweza kufanya kila kitu lakini hatuwezi kutengua kila tulichokifanya, [we can do everything but we cannot undo everything]. Kabla ya kuamua kufanya hiyo kazi, fikiri kwanza juu ya matokeo ya mwisho ya uamuzi wako juu ya kazi hiyo. Mara nyingi tumesikia habari za familia zilizokuwa zinaendelea vizuri mpaka pale ambapo baba au mama aliamua kufanya kazi fulani. Mtu huyu anafanikiwa ofisini au kazini lakini kwa gharama ya familia yake au gharama ya roho yake. Au mwingine anafanikiwa katika biashara kwa gharama ya uhusiano wake na watu wake wa karibu. Uamuzi sahihi hauleti majuto wala kujilaumu baada ya kuamua bali hukupa amani, utulivu na ujasiri hata pale unapokutana na changamoto mbalimbali baada ya kuamua.
Biblia inashauri inapofika wakati unataka kufanya maamuzi fulani, usikimbilie katika kuamua bali uketi kwanza uhesabu gharama na kufanya shauri ili matokeo ya maamuzi hayo yawe yenye ufanisi na kukuwezesha kuishi maisha yenye furaha na ujasiri bila majuto wala kujilaumu hapo baadae. Luka 14:28-32.
Kama Adamu na Eva, wangefikiri au wangejua matokeo ya maamuzi yao ya kwenda kinyume na maagizo ya Mungu ya kutokula tunda, naamini wasingekula lile tunda. Maagizo ya kutokula tunda hayakuwekwa ili kuwaonea bali yaliwekwa ili kuwalinda wao dhidi ya mauti na uharibifu katika maisha yao. [It was for their advantage].
Hekima ni uwezo wa kujua matokeo ya maamuzi yako kabla hujaamua. Unapojua matokeo kwanza inakusaidia kujua nini unatakiwa kuamua, nini hutakiwi kuamua, lini unatakiwa kuamua na lini hutakiwi kuamua n.k! Mara nyingi tumesikia watu wakisema, tunajifunza kutokana na makosa; lakini mwenyehekima mmoja ameongeza na kusema ni vyema makosa hayo yakawa ya mtu mwingine, kwa sababu kuna baadhi ya maamuzi yakikosewa hamna nafasi ya kujifunza; Hauwezi kujifunza kama sumu ya panya inaua kwa kuionja, ile kwamba panya wanakufa wakiila hilo ni darasa tosha [1Kor10:5-11].
“Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia”- Mithali 22:3
Amani ya Kristo iamue ndani ya Mioyo yenu 
Kama ndani ya moyo wako hauna amani na utulivu juu ya uamuzi unaotaka kufanya, usifanye maamuzi kwanza. Kukosa amani na utulivu juu ya jambo hilo unalotaka kuamua ni ishara ya Roho Mtakatifu ndani yako kwamba kuna jambo haliko sawa bado; inawezekana muda bado au jambo lenyewe haliko sawa. Inawezekana kuna mtu unataka kuingia naye katika uhusiano fulani mfano Kibiashara na hauna utulivu na amani juu ya mtu huyo au biashara hiyo, usiamue kwanza. Tumia muda wa kutosha katika kuomba Mungu ili akuongoze juu ya uamuzi huo; na kama bado haupati amani juu ya uamuzi huo jipe muda wa kutosha wa kutafakari na Kuomba ili Mungu akuongoze katika lililo bora zaidi. [Wakolosai3:15]
Usikubadili kusukumwa katika maamuzi na watu wengine au mazingira yanayokuzunguka kwa sababu baada ya kufanya hivyo ni wewe peke yako ndiye utakaye kabiliana na matokeo ya uamuzi huo; na haitakuwa na msaada wowote hapo baadae ukisema fulani ndiye aliyesababisha niamue hivyo. Jambo la msingi ambalo tungependa ukumbuke mahali hapa ni kwamba, wewe ni nahodha wa meli ya maisha yako; inategemea unaloazimia (unaamua binafsi) kwenda wapi. Jukumu hili si la mtu mwingine, watu wanaweza kukushauri lakini jukumu la uamuzi au uchaguzi ni lako binafsi.
Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana; Na kwa shauri la akili fanya vita- Mithali 20: 18
Tafuta mashauri ya neno la Mungu kwanza na uyazingatie kabla ya kufanya uamuzi, ushauri wa neno la Mungu juu ya kuwa na mahusiano bora, namna ya kumpata mwenza bora wa maisha, namna ya kuwa na ndoa nzuri, namna ya kulea watoto, ushauri juu ya mambo ya kiuchumi, biashara, namna ya kumtumikia Mungu kwa ubora, mambo ya uongozi, mambo ya kijamii…….n.k!
Hakuna aliyemshauri bora kwako kupita neno la Mungu. Ushauri wa Neno la Mungu ni bora kwa afya yako ya roho na mwili. Mungu hutoa ushauri ulio BORA kwa ajili yetu kwa sababu mwanadamu anaweza kuchagua jambo la kufanya lakini hawezi kuchagua matokeo ya jambo hilo atakalolifanya.
Tafuta watu wenye hekima na hofu ya Mungu ndani yao ili kukushauri juu ya jambo ambalo hujui ufanye nini na wakati huo huo unatakiwa kulifanyia maamuzi; usiamue kwa siri kama hauna utulivu wala amani nalo, usiamue peke yako ikiwa ndani ya moyo wako unajua kabisa kuwa unahitaji msaada.  Vijana wengi hufikiri kwamba kila aliyeko kwenye ndoa, ni mshauri nzuri juu ya mambo ya mahusiano na ndoa, hili halina ukweli sana. Lakini hii haina maana hauwezi kujifunza jambo la kukufaa kutoka kwao la hasha!
Jambo la muhimu ni kwamba, Unapoenda kuomba ushauri kwa mtu juu ya jambo lolote, ni vizuri kujiridhisha kwamba ushauri huo haupingani na kanuni za  neno La Mungu, kinyume na hapo ninakusihi usifanyie kazi ushauri huo bila ya kujali nani ameutoa. Neno la Mungu linashauri kwamba ni shauri la AKILI tu ndio ufanyie kazi. [Mithali 13:20

2 comments :

  1. Nashukuru kwa msaada maana ninawakati mgumu sana, nilikuwa na mchumba ambaye nilijikuta kwenye mahusiano naye baada ya kujiona kuwa muda unanitupa, lakini sikutambua kuwa mapenzi ya MUNGU ni kuwa tuwe na amani,kiukweli tangu niingie kwenye mahusiano nasikia kuhukumiwa na sina tumaini kanisani naenda lakini nasikia uzito Moyoni sana, nikimwomba MUNGU SIPATI AMANI KILA KUKICHA NAZIDI KUKOSA AMAN,lakini nimemwomba MUNGU anipe la kufanya maana naona kila nalolifanya nazidi kumkosea mwenzangu japo yeye ni mtaratibu kiasi kwamba nahofia kuja kumharibia maisha, nilijaribu kumwambia kuhusiana na kusitisha mahusiano ili tuombe uongozi wa MUNGU zaidi na akanielewa na nako naendelea kumsihi MUNGU atokeze msaada maana hata huduma nashindwa kufanya, nahitaji maombi yenu ili kama kuna jambo limejificha MUNGU aliweke wazi

    ReplyDelete
    Replies
    1. Daniel Mungu wetu ni mwema na ndiye hutoa majibu ya maswali magumu. Tupo pamoja katika kuombea suala lenu. Bwana akubariki sana

      Delete