Nguvu Zako ni Kidogo ..........

2:52:00 PM Unknown 0 Comments

 

NGUVU ZAKO NI KIDOGO, UNAMUHITAJI MUNGU
Nawapenda watu wanaotia moyo na kusisimua wengine, ingawa baadhi yao ni watu hatari. Naziogopa baadhi ya kauli zao, ndio maana mara zote husoma vitabu vyao kwa umakini mkubwa. Watia moyo wengi (motivators/inspirational speakers) humwondoa Mungu katika mahubiri yao, huwaaminisha watu katika uwezo wa akili na fikra chanya tu (positive thinking). Nimewahi kusoma kauli ya zamani kidogo ya mtu aliyejulikana kama kiongozi wa haki za wanawake, nikaogopa sana. Amenukuliwa hivi: “Ifikapo mwaka 2000 natumaini tutawalea watoto wetu kuamini katika uwezo wa kibinadamu, na si Mungu” Gloria Steinem, Mhariri wa Ms. Magazine.
Mungu ndiye anayeweza kujenga ustawi pekee wa mwanadamu. Alikuja ili tuwe na uzima tele katika mwili, roho na nafsi. Ustawi wa mwanadamu bila ya Mungu ni anguko kuu. Mungu ndiye anayepaswa kulijenga kanisa lake. Ni Mungu ndiye ajengaye uhusiano wetu, uchumi wetu, huduma zetu na hata ukuaji wetu kiroho. Kufanya bila ya yeye ni kufanya kazi bure. Kujenga asiyoyajenga ni kujitaabisha. Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure.” Zaburi 127:1
“Ni Mungu ndiye ajengaye uhusiano wetu, uchumi wetu, huduma zetu na hata ukuaji wetu kiroho”
Mtakatifu Agustino alisema, “Bila ya Mungu hatutaweza kufanya jambo, bila ya sisi Mungu hatafanya jambo.” Mungu hatafanya kwa niaba yako bali atakusaidia kufanya. Hauwezi pasipo msaada wake, lakini pia hatafanya pasipo wewe. Biblia inasema, “kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu”.  Maana yake yeye hutupa msaada ila watendaji ni sisi. Daudi ndiye aliyekuwa akipigana wala si Mungu, lakini alipigana kwa kuwezeshwa na kupakwa mafuta na Mungu. Zaburi 89:20-21
Kila unapokaribia muda wa kusimama jukwaani, kwenye gari au mitaani katika huduma za kijiji kwa kijiji huwa tunajiona hatuwezi kuhubiri. Huwa tunajua pasipo upako ni sifuri. Ni wazi mwokozi ni mmoja jina lake ni Yesu, mponyaji ni Mungu na huwa ni vigumu kuiona sehemu yetu. Maneno yake Bwana Yesu ni dhahiri, “Ninyi hamwezi kufanya jambo lolote pasipo mimi” kwa hiyo ili kusimama na kutangaza ujumbe wa injili huwa namwita BWANA ili anipake mafuta na awe pamoja nami.
Katika kitabu cha Matendo ya Mitume 10:38 siri ya mafanikio ya huduma ya Yesu Kristo imewekwa wazi. Siri hii ni katika mambo mawili: moja ni kwa sababu alipakwa mafuta kwa Roho, mbili ni kwa sababu alikuwa pamoja na Mungu. Na sisi leo kwa kuwa nguvu zetu ni kidogo tunahitaji kupakwa mafuta kwa Roho (upako), na pia tunapaswa kuwa na Yesu (Mungu) ndani yetu. “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.”
“Je, haiogopeshi kwamba mahubiri ya mitume siku ya pentekoste yalilizidisha kanisa kwa watu 3000 kuokolewa ndani ya siku moja? Na leo hii tuna miji au vijiji ambavyo mahubiri 3000 yamehubiriwa na hakuna hata mtu mmoja aliyeokoka”
Bila nguvu ya Roho Mtakatifu haiwezekani; Mitume waliweza kwa sababu walipokea nguvu itokayo juu, Daudi aliweza kwa sababu alitiwa mafuta na mimi na wewe tunahitaji kupokea nguvu. Ukishajua kwamba kazi hiyo uliyonayo imetoka kwa Mungu, basi ni muhimu umtafute kila unapojihusisha na jukumu hilo. “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Matendo 1:8
Leonard Ravenhill mhubiri mwenye alama alikaririwa akisema kwamba, “Je, haiogopeshi kwamba mahubiri ya mitume siku ya pentekoste yalilizidisha kanisa kwa watu 3000 kuokolewa ndani ya siku moja? Na leo hii tuna miji au vijiji ambavyo mahubiri 3000 yamehubiriwa na hakuna hata mtu mmoja aliyeokoka.” Binafsi naamini ni kwa sababu wahubiri wamekosa nguvu, upako na ushirika na Mungu. Wanahubiri dini badala ya ufalme wa Mungu, wanaogopa jela na mashtaka; wanataka vyeo na hivyo wanavilinda kwa mahubiri poa na baridi kama barafu. Kwa namna hii hata yakiwa mahubiri 10,000 hayawezi okoa mtu. Tunahitaji nguvu!
Mambo yaliyotoka kwa Mungu huhitaji mhusika amtegemee Mungu. Kila kitu kitakamilika kwa utii na sala tu. Katika kutimiza ndoto na malengo yako unapaswa kumtegemea Mungu na kuzisahau nguvu zako.
“Ili kumaliza bila ya majuto ni vema usiende kwa nguvu zako”
Ili kumaliza bila ya majuto ni vema usiende kwa nguvu zako, Musa alijaribu kutembea kwa nguvu zake ili kutimiza matamanio yake lakini hakuweza. Alitamani awaokoe watu yeye binafsi lakini nguvu zake zilikuwa ni kidogo. Hakuweza! Mpaka alipogeuka na kumtazama Mungu.
Wewe pia unaweza kugeuka leo na kumtazama Mungu, yeye ndiye chanzo cha nguvu zetu. Mzaburi amenena, “Ee Bwana nguvu zangu nakupenda sana” Unaweza kumwita pia na atakujaza nguvu. Omba sasa, mwite sasa.

0 comments :