Umuhimu wa kutambua ........
UMUHIMU WA KUTAMBUA VIPAUMBELE KWA WAKATI
(Nioneshe vipaumbele vyako; nikuoneshe hatima yako)
Watu
wengi hawafanikiwi si kwa sababu hawana uwezo wa kufanikiwa; bali, ni kwa
sababu hawafanyi mambo yatakayowaletea mafanikio. Ile kwamba mtu hajafanikiwa haina maana mtu huyo hana uwezo wa
kufanikiwa; bali ni kwa sababu mtu huyo hafanyi au hajafanya mambo
yatakayomletea mafanikio.
Mafanikio
katika ufalme wa Mungu sio mchezo wa bahati nasibu (lottery) au mchezo jackpot
bingo bali ni matokeo ya utendaji kazi wa kanuni
(principles) zilizopo katika neno la Mungu, kwa eneo husika na muda husika; kwa
mfano; hata ukifunga na kulia mbegu ya mti iliyowekwa sakafuni haiwezi kuota na
kufikia kuwa mti, unahitaji kuiweka katika kanuni ya mazingira na hali ya hewa
sahihi ili iweze kuota (The principle of an environment). Kuongeza au
kupunguza, katika utekelezaji wa kanuni yoyote huathiri matokeo yaliokusudiwa
katika eneo husika.
Kanuni ya kuishi kwa kuweka
vipaumbele (principle of priority)
Kanuni
mojawapo inayoweza kukuhakikishia mafanikio katika maisha, ni uwezo wa kutambua
na kuweka vipaumbele katika maisha ya kila siku; uwezo wa kutambua mambo ya
msingi yanayotakiwa kupewa kipaumbele kwa wakati;
hasa katika utekelezaji kabla ya jambo lingine lolote. Vipaumbele
hutusaidia kuzingatia mambo yaliyo muhimu na yenye kufaa kwa wakati husika,
hutusaidia kutokupoteza rasilimali katika mambo yasiyo ya msingi au muhimu.
Vipaumbele
maana yake vitu vifaavyo sasa na muhimu, vitu vya kuwekwa kwanza kabla ya
vingine, vitu vya kuwekwa mbele ya vingine katika mgawanyo na matumizi ya
rasilimali muda na rasilimali
nyingine; vipaumbele ni vitu au jambo lililo bora kwako kwa wakati huu kuliko
mengine, uko tayari vingine vipotee ili kupata na kulinda kipaumbele chako.
Vipaumbele huendana na muda.
Jambo la kwanza sasa ukiliweka la
kwanza kesho hutapata matokeo yaliyo bora (Mhubiri 3:1, 11a). Wanaisraeli
walipata shida katika hali zao za uchumi kwa sababu ya kushindwa kuzingatia
muda katika kuweka vipaumbele vyao; walipotakiwa kutoa sadaka na kujenga Nyumba
ya BWANA wao walisema huu sio wakati na hivyo iliathiri hali yao ya kiuchumi na
kimaisha (Hagai 1:2, 4).
Ndio
maana biblia imeweka msingi wa vipaumbele kwa vijana katika muda wao wa ujana
ili watumie muda wao huo kwa kujenga uhusiano bora na Mungu na kumtumikia kabla
ya siku za uzee wao (mhu12:1). Hiki ni kipaumbele muhimu kuliko vyote unavyoweza kuwa navyo.
Mtu
asiyetambua nini ni kipaumbele kwa
wakati husika, ni sawa na meli isiyokuwa na uelekeo katikati ya bahari.
Vipaumbele vinasaidia kujua ufanye/usifanye nini kwa wakati huu; inakupa kujua
njia (dira) sahihi ili kufikia malengo yako. Mtu asiyekuwa na vipaumbele ni
sawa na mtu asiyejua njia. Mtu huyu hawezi kupotea njia, anaweza kufika
anapotakiwa kufika na asijue kama amefika. What a waste!!
Ukiamka
asubihi Tv inataka uingalie muda wote; Redio inataka uisikilize, hakuna muda
watazima mitambo yao ili wakupe nafasi ya kufanya mambo yako mengine; masaa 24
wanarusha matangazo; simu inataka uchat muda wote; marafiki wanataka mkae masaa
sita mpige stori tu. Magazeti yanataka uyasome, bado majukumu ya shule kama ni
mwanafunzi au ofisi kama ni mfanyakazi
au mfanyabiashara. Kila kitu kinataka
kutumia muda wako; usipojua nini kianze na nini kifuate; niulize, nami
nitakuambia mwisho wako. Nioneshe vipaumbele vyako; nikuoneshe hatima yako.
Kipaumbele cha kwanza kuliko vyote unavyoweza kuwa navyo.
Kipaumbele
cha kwanza ili kufanikiwa ni kuwa na uhusiano binafsi na Mungu (daily
communion). Daudi alitafuta neno moja tu nalo ni kukaa nyumbani mwa BWANA. Mafanikio
halisi huanza na Mungu mwenyewe. Maisha ya mwanadamu Huanza, Hukamilika na
Kupata maana katika Mungu pekee; uhusiano huu ni zaidi ya kwenda kanisani
jumapili, ni zaidi ya kwenda kwenye kikundi cha sala; ni kutamani kukaa katika
uwepo wake Muda wote, kuzijua njia zake, kuungana naye na kushikamana naye
katika Neno lake katika maisha yetu ya kila siku.
“Neno moja nimelitaka kwa BWANA,
Nikae nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu. Niutazame uzuri wa BWANA,
na kutafakari hekaluni mwake” Zab 27:4
Mwandishi
wa kitabu cha ‘Momentary marriage’, John Piper amewahi kuandika jambo kuhusu
umuhimu wa vipaumbele kwa kusema, “kuweka
jambo la kwanza kuwa la kwanza, hufanya jambo la pili kuwa bora zaidi”
(keeping first things first, makes second things better). Hivyo kuweka jambo la kwanza kuwa la pili huathiri
matokeo ya mambo yote katika hali zote.
“…Bwana akajibu akamwambia… Martha, unasumbuka
na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja; na
Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa” Luka 10:39-42
Kipaumbele
cha Mariamu ilikuwa ni jambo moja tu ambalo lililokuwa linatakiwa kwa wakati
huo, nalo ni kukaa miguuni pa Yesu ili apate kusikiliza maarifa yatakayompa
ufahamu na hekima katika maisha. Kipaumbele hakikua katika kufanya kazi bali
kukaa na kumsikiliza kwanza mwenye kazi. Ndio maana Mfalme Daudi alitaka kukaa
nyumbani mwa BWANA siku zote apate kuutazama uzuri wa BWANA na kutafakari
(meditate) Neno hekaluni mwake na hivyo alipata hekima iliyomsaidia kujua namna
ya kuishi ili kufikia mafanikio katika maisha yake; si ajabu ni miongoni mwa
wafalme waliofanikiwa sana katika
nyakati zao (zab119:97-98, 104).
Ni
muhimu kukumbuka kuwa, Maisha ya
mwanadamu ni kama kitabu, kwa jinsi anavyokaa na Mungu ndivyo kinavyozidi
kufunguka kurasa hadi kurasa. Unaposhindwa kutambua vipaumbele kwa wakati,
maisha yanakuwa hayana ladha, yanabeba mafadhaiko, kulaumu wengine na masumbufu
ya kila namna; kwa sababu kuweka jambo la kwanza kuwa la pili huathiri matokeo
ya mambo yote katika hali zote.
Tujifunze kwa Nehemia
Usipokuwa
na vipaumbele, hauwezi kusema hapana kwa mambo yanayoonekana kuwa mazuri (good)
ili kuyafikia yaliyo bora (best). Nehemia wakati ameanza kazi ya ujenzi wa
ukuta wa Yerusalemu uliokuwa umebomolewa, alijua kipaumbele kwa wakati ule ni kazi iliyokuwa mbele yake,
hakukubali kuyumbishwa na jambo lingine lolote. Usipojua nini unatakiwa kufanya
kwa wakati husika, utafanya kila kitu na kujitahidi kuwa kila kitu (committed in the wrong things).
“Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe
kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono… Na
mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata
nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie? Nao
wakaniletea maneno hayo mara nne, nikawajibu maneno kama yale…” Nehemia
6:2-5
Iwe
ni mfanyakazi, mwanafunzi, mzazi au mlezi ni muhimu kutambua na kuzingatia
vipaumbele katika kila eneo muhimu la maisha yako kwa wakati; vipaumbele vyako
ndivyo vitakavyoamua uelekeo wako na hatima yako, ni muhimu kujizoeza kutenga
muda mara kwa mara na kujiuliza ni nini kipaumbele, nini kianze na nini kifuate
iwe kwa mambo ya ofisi, biashara, shuleni au nyumbani;
“If you don’t know where you are
going, any way can take you there”
0 comments :