Mtu Mwaminifu
MTU MWAMINIFU
(Tujifunze kwa nabii Samweli)
Ukuaji wa tabia ni mchakato, sawa na ukuaji wa mwili. Mwili
hupokea chakula kwa kupitia mdomo bali tabia hujengwa kupitia milango ya fahamu
kama vile, macho na masikio. Tuonacho sana na kusikia sana hugeuka kuwa tabia
yetu. Leo tunatamani usikie kuhusu Samweli ili tabia yake iwe tabia yako.
Samweli alikuwa kiongozi mwaminifu katika ofisi yake.
Tunahitaji kuwa watu waaminifu katika mazingira yasiyo aminika. Mtu asiye
mwaminifu hawezi kumudu mazingira korofi, yaani: umasikini, vishawishi na
mivuto ya kidunia. Mtu mwaminifu anaaminika hata kama
mazingira hayaaminiki, asiyemwaminifu haaminiki hata katika mazingira salama. Leo hii
kuna nakisi ya watu waaminifu. Hatuna upungufu wa watendaji bali tunaupungufu
wa watendaji waaminifu; hatuna upungufu wa wanasheria, bali tunaupungufu wa
wanasheria waaminifu; hatuna upungufu wa wanasiasa bali tunaupungufu wa wanasiasa
waaminifu.
“Mtu mwaminifu anaaminika hata kama mazingira hayaaminiki, asiyemwaminifu haaminiki hata katika mazingira salama”
Uaminifu si hamasa au shauku ya siku moja, uaminifu ni tabia
inayojengwa na kujengeka ndani ya mtu.
Uaminifu ni tunda la Roho (Gal 5:22), tunda halikomai na kuiva kwa siku
moja, huchukua muda. Uaminifu ni uwezo wa kujifuata mwenyewe. Lazima tuweze
kujifuata na kujiongoza wenyewe. Mitume pasipo Yesu, nasi pasipo mitume.
Nabii aishi katika uaminifu wa kinabii, baba wa familia na atimize
wajibu wake kwa uaminifu na mwalimu ashike maadili yake. Jaji na afuate
hadhi ya ofisi yake. Kama umeitwa
kumwimbia Mungu basi jifuate mwenyewe, usiwe mwimbaji wa nyimbo za dini lakini
unapendelea kusikiliza taarabu ukiwa gizani.
Kama umeitwa kuwa mchungaji jifuate pia yaani, tabia yako ifanane na ofisi yako.
“kiongozi ni mtu mwenye kuijua njia, anayepita hiyo njia na anayeonesha wengine namna ya kupita njia hiyo.”
Samweli alikuwa mwaminifu alitenda kile alichosema; imani
yake ndiyo ilikuwa tabia yake na huo ndio huitwa uaminifu. Lissy M. ameandika
maneno haya katika kijitabu chake cha mafanikio, “kiongozi ni mtu mwenye kuijua njia, anayepita hiyo njia na anayeonesha
wengine namna ya kupita njia hiyo.”
Samweli alianza vizuri na kumaliza vizuri, ni mfano wa
kuigwa. Alipowahutubia Israeli hotuba yake kuelekea mwisho wa uongozi wake
hakupatikana mtu aliyeona dosari katika maisha yote ya Samweli. Samweli alihoji
kama yuko mtu mwenye kumdai chochote na hakupatikana mtu awaye yote. Samweli
hakuiba, hakuchukua rushwa, hakupotosha hukumu, wala hakujitia katika uchafu
wowote. Samweli ni kiongozi mwenye karatasi safi yaani, clean sheet!1
Samweli12:3
Hata baada ya Samweli kuwaambia mkutano wa Israeli
washuhudie kama kuna kosa au dosari yoyote aliyofanya katika huduma yake kama
kiongozi wao, mkutano ulithibitisha
kwamba, hakuna tatizo lolote katika maisha yote ya Samweli tangu utoto
hata utu uzima wake. Samweli ni mfano wa kuigwa kwa utumishi uliotukuka katika
ofisi yake.
Nani katika viongozi wa leo wa kiroho na hata ki-siasa
atathubutu kugawa karatasi nyakati za mwisho wa muhula wa uongozi wake ili
wananchi wamtathimini? Samweli alitenda hivyo na alimaliza vizuri, bila ya
lawana wala bila ya kulitukanisha jina la BWANA Mungu wake. Uaminifu ni bidhaa
adimu, kufuzu na kupata vyeti vya bodi kama vile; CPA(T), ACCA, PSPTB, bodi ya
wakandarasi hata shule ya sheria haitawezesha upatikanaji wa watu waaminifu
hadi wataalamu hawa wahusiane na Muumba wao. Ndivyo ilivyotokea kwa Zakayo
mtoza ushuru.
Kilele cha tabia njema ni kufanana
na Yesu (1Yohana 4:17b). Hatuwezi kusema tumefika au tumekamilika
kitabia mpaka pale tutakapofanana na Yesu, kama hatujafikia hapo, basi
tunapaswa kukaza mwendo kuendelea na safari yetu ya ukuaji kuelekea mwenendo
bora.
Kwa
kweli hakuna njia ya mkato, Christ likeness should be the summit of our good
character!
0 comments :