Siachi
SIACHI
(Dhambi ni kutelekeza kipaji chako)
“If you can’t walk then crawl. But whatever you do you have to keep
moving Forward'” Martin Luther King Jr.
Katika siku za
karibuni tumeshuhudia migomo ya watu wenye taaluma na vipaji mbalimbali. Kumekuwa
na migomo ya walimu, madereva, madaktari na watu wa kada na tasnia nyingine
tofauti tofauti. Migomo hii hulenga kuifanya jamii na serikali itambue mahitaji
ya makundi haya kipekee, hususani tafsiri ya uwiano wa mchango wao kwa jamii na
mishahara wanayolipwa.
Katika migomo
yote, mgomo wa madaktari hutikisa zaidi, madhara yake ni dhahiri machoni pa
wote. Watu hupoteza maisha, wagonjwa huteseka na ndugu zao hupoteza matumaini.
Kama ilivyo kwa madaktari, yako madhara kwa kila mwenye kipaji ambaye ataacha
kukitumia. Waathirika ni wale ambao Mungu alitaka wanufaike kwa kipaji chako.
Ni wazi hakuna mto unaokunywa maji yake wenyewe. Yako madhara kama viongozi
watajiuzulu bila msingi, yako madhara kama wahubiri watasimama na kuacha
kuhubiri. Yesu alisema, atazamaye nyuma hafai kwa ufalme wake.
Dereva mwenye
hekima akikimbia nafasi yake atafanya madereva walevi wapate ajira na kisha
kuua watu kwa ajali isiyo na sababu. Kwa sababu ya wenye hekima kuogopa siasa,
nchi zimeongozwa na mabaradhuli. Mchungaji akiacha kuombea kondoo shetani
anawatafuna. Kuacha wajibu wetu ni dhambi, Samweli akasema, siachi…… 1Sam 12:23
Wizi, uzinzi,
ulevi na uasherati si dhambi kubwa ukilinganisha na mhandisi kuacha kazi
aliyoitiwa na Mungu. Dhambi kubwa ni mwimbaji wa kusifu na kuabudi kuacha
huduma yake, mhubiri kuacha kuhubiri, kiongozi kuacha kuongoza.
Wewe kama ni
ndege jielekeze katika kuruka na si kuogelea. Ni kwa faida yako, ukitaka kujua madhara
ya kutokutumia kipaji chako jifunze katika vipaji ambavyo madhara yake yako nje
kama vile udaktari au udereva, ambapo kosa moja hugharimu pumzi za watu.
Paulo alisema,
“Ole wangu nisipo ihubiri injili”. Usipofanyia kazi kipaji ulichopewa na Mungu unafanya
dunia iwe kama kibogoyo, maana pengo lako halitazibika. Uzuri wa dunia ni
pamoja na mchango wa kipaji chako.
Jaribu kufikiri
familia yenu bila ya wewe, kanisa lenu bila ya wewe, kazini kwako bila ya wewe
kuwepo kama hakuna pengo lolote katika
kutokuwepo kwako ujue wazi hautumii kipaji chako. Imagine the World without
Jesus Christ!
Mimi siachi
kuhubiri, siachi kuimba, siachi siasa safi, siachi ufundi, siachi sanaa, siachi
nasema siacha ubunifu wangu. Usiache karama yako ya maombi (1Sam 12:23); usiache
biashara yako wala usidharau mwanzo wako mdogo, wala usipuuze wazo lako la
ushindi. Kuendelea mbele inapaswa kuwa kama wimbo wako. Mungu Baba na
akuimarishe katika kipaji na wito wako ulioitiwa, ukawe hodari; kama jua
lisivyo acha kuangaza na wewe kwa kupitia kipaji chako ukaangaze milele kwa
jina la Yesu Kristo. Amen
Kileleni ndipo
tunapopatikana.
0 comments :