Kutambua uwezo wako, .....

12:07:00 PM Unknown 0 Comments

 
KUTAMBUA UWEZO WAKO; CHUKUA HATUA
(Unlock your potentials)
Hakuna mtu aliyewahi kufikiri kuwa, binadamu anaweza kukimbia mita mia (100) kwa sekunde tisa nukta tano nane (9.58) mpaka pale mwanariadha kutoka Jamaica, Usain bolt alipoweka rekodi hiyo ya dunia katika mji wa Berlin nchini Ujerumani mwaka 2009 ambayo haijavunjwa mpaka sasa. Wala hakuna mtu aliyewahi kufikiri kuwa binadamu anaweza kuruka juu (bila ya msaada wa kitu chochote) umbali wa mita 2.5 yaani zaidi ya futi 8 mpaka pale mwanamichezo Javier Sotomayor (Cuba) alipoweka rekodi ya dunia kwa kuruka umbali huo mwaka 1993.
Watu wote ambao tumeona uwezo wao ukidhihirika hata kutushangaza wakati mwingine, wana namna ya kufikiri ambayo huwatofautisha na watu wengine na hivyo hupata matokeo bora katika kile wanachokifanya kuliko watu wengi.  Je, wewe namna yako ya kufikiri ipoje, je unafiri namna utakavyoshindwa ukijaribu? Namna ambavyo haiwezekani? Kwamba hakuna aliyeweza kufanikiwa katika jambo hilo? Kwamba hapo ulipo imetosha? Au unafikiri namna [njia] ya kushinda/kufanikiwa katika kile unachotaka kufanya? Namna ambavyo utaweza?.
Ile kwamba hakuna aliyeweza jambo hilo kabla yako, haina maana kwamba jambo hilo haliwezekani! Kumbuka hakuna aliyewahi kumuua Goliati kabla ya Daudi, hakuna aliyewahi kusimamisha jua kabla ya Joshua, hakuna aliyewahi kutabiria mifupa na ikawa hai kabla ya Ezekiel. Hakuna aliyewahi kurusha ndege kabla ya the Wringht brothers (kwanza mara ya kwanza iliruka umbali wa futi 120 na kukaa angani kwa sekunde 12)!
Hii haina maana kwamba hakukuwa na watu wengine kabla yao, inawezekana wapo waliopata mawazo kama yao kabla lakini hawakuchukua hatua yoyote katika kuyafanyia kazi. Inawezekana hofu, kughairi mara kwa mara, kutokuzingatia vipaumbele na kila sababu walizokuwa nazo ndio viliwakwamisha na hivyo wamefukiwa na historia bila ya kutambua uwezo waliokuwa nao. Mwanariadha Usain Bolt amewahi kusema, “Anything is possible. I don’t think limits” (Kila kitu kinawezekana. Huwa sifikirii vikwazo: Tafsiri isiyo rasmi). Watu hawa wanatufundisha kuwa, hakuna mtu ataweza kutambua uwezo aliona nao au umbali unaoweza kwenda mpaka pale amechukua hatua.
Kumbuka, hautaweza kutambua uwezo wako katika kuimba mpaka umeimba, hautaweza kutambua uwezo wako katika kuongoza mpaka umechukua hatua na kuongoza, hautaweza kutambua uwezo wako katika kufanya kazi mpaka umeifanya hiyo kazi. Hautaweza kutambua /kujua umbali gani unaweza kwenda katika jambo lolote mpaka umeanza na hatua moja, iwe ni katika huduma, kazi, biashara n.k!
Wazo kuu tunalotaka ulipate siku ya leo ni kwamba; Ili kutambua uwezo wako na umbali unaoweza kwenda katika jambo lolote ni muhimu kuchukua hatua katika kufikia kilele cha uwezo [Abilities, gifts, talents] ambao Mungu ameweka ndani yako ili kuwafaidia wengine na kumpa yeye Utukufu.
“Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye Mbinguni”
There’s a place for you at the top

0 comments :