Yesu ni Bwana ...

12:51:00 PM Unknown 0 Comments

 
YESU NI BWANA WA YOTE NA VYOTE
(Huwezi kuwa bwana wa wachache) 
Jumapili iliyopita (Tar. 16 Aprili 2017) tumesherehekea Pasaka, ni sikukuu kubwa kweli kweli! Pasaka ni sikukuu ya U-Bwana wa Yesu Kristo. Bila Pasaka hatuwezi kumwita Yesu Kristo awe Bwana.
Kanuni za kufanyika BWANA zinamtaka mtu awe BWANA juu ya vyote na juu ya wote. Hakuna uchache, ukiwashinda wachache ni sawa na hakuna. Ndio maana Yesu ni BWANA hadi kwa wasiomjua na kumwamini. Ili uwe BWANA lazima uwashinde wote, na uwaweke chini ya miguu yako wote, wa kabila zote na nchi zote. Ili uwe BWANA ni lazima ushinde magonjwa, Yesu hakuwahi kuugua, ili uwe BWANA ni lazima ushinde dhambi, Yesu hakutenda dhambi. “bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;” Wafilipi 2:8-9
Mapema kabisa katika siku zake YESU Kristo aliwashinda maadui zake wote. Alimshinda adui, dhambi, mapepo, umasikini, laana, balaa na mikosi. Maadui wa mwanadamu ndio walikuwa maadui wa Kristo Yesu. Alibakia adui mmoja tu jina lake mauti.
Sheria za U-bwana zinabana sana. Hata ukiwashinda adui wote akibakia mmoja bado wewe hautapewa ubwana. Sheria inataka asisalie hata mmoja ambaye hujamkanyaga miguuni pako. Ni kama alivyofanya Daudi kwa kuwapiga adui zake wote, asisalie hata mmoja.
Adui aliyekuwa amesalia ni kifo na tunaposherekea Pasaka tunafuraha kwani Yesu Kristo ameshinda kifo cha kiroho na cha kimwili. Pasaka inamtangaza Yesu kuwa BWANA wa vyote na wa wote kwa kuwa hakuna kilichosalia tena ambacho hajakishinda. Katika pasaka Yesu anashinda kilichosalia ambacho ni kifo. Baada ya hapo hakuna adui mwingine tena machoni pa BWANA YESU KRISTO.
Pasaka ni pigo la ushindi, ndio maana jiwe lilikutwa mbali, maana shujaa Yesu Kristo alitoka kwa ushindi.
Ukubali au ukatae Yesu Kristo atabaki kuwa BWANA. Hakuna tena kuitisha uchaguzi ili watu waamue awe BWANA au asiwe. Hata nchi yote na dunia yote waamue kukataa, Yesu hatabadilika bali ataendelea kuitwa BWANA na kutawala mbinguni na Duniani.
Yeye ni BWANA si tu juu ya watu bali hata juu ya vitu na hali ya hewa. Ndio maana kwa jina la BWANA Yesu; upepo, UKIMWI, Upofu, na kila hali mbaya hukaa kimya. “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba” Wafilipi 2:9-11
BWANA YESU ASIFIWE…..hiyo ndio furaha ya Pasaka. Hiyo ndiyo sherehe ya Pasaka yaani, U-BWANA WA KRISTO YESU.
Jiandae kwa msimu wa tano wa weekend of purpose, tukutane Dar-es-salaam.
Barikiwa.

0 comments :