Wito binafsi

2:01:00 PM Unknown 0 Comments


WITO BINAFSI.
(Umeitwa kwa jina lako)
Wakristo, wanafunzi, wachungaji, waimbaji, wainjilishaji, wafanyakazi, wataalamu, wanaharakati n.k, ni majina ya vikundi ambayo hayatoi wajibu mkubwa kwa mtu binafsi. Ukweli ni kwamba wito ni ile sauti inayokuhamisha kutoka katika kikundi fulani, nchi yako, mipango yako binafsi na hata katika mwelekeo binafsi.
Wito si jambo jepesi, unaweza ukuleta usumbufu. Wito unahitaji aliyeitwa awe shupavu katika kukata kona (kuitikia wito), awe na uwezo wa kugeuka haraka. Pale mwanafunzi anapoteseka miaka zaidi ya mitano katika masomo yake ili awe daktari na baadaye sauti ya Mungu inamwita katika mwelekeo mwingine tofauti na udaktari, kunahitajika ushupavu na usikivu. Pamoja na kuwepo kwa gharama ya usumbufu, wale wanaotii sauti ya Mungu baadaye hufurahi na kufaidika.
Kuna wito ambao Mungu anamwita kila mtu, wito huu huhusisha aina na mtindo wa maisha tunaopaswa kuenenda nao hapa duniani. Uko wito wa kuishi maisha matakatifu, uko wito wa wokovu uko wito wa kumfuata Yesu yaani ufuasi. Wito wa ujumla haubagui kila mtu lazima aitikie sauti hiyo.
Katika makala hii ninalenga wito wa kipekee, wito ambao hauhusishi mke wala mume, hauhusu kikundi fulani cha watu bali unahusu mtu binafsi. Ameandika mchungaji mmoja, “Yuko wapi mke wa Petro?” Hatutazamii kumuona mwingine katika wito wako bali wewe peke yako.  Ibrahim aliacha nchi, baba na nduguze kwa ajili ya wito. “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.” Yohana 21:15
Yesu alimwita Petro kwa jina, na alimpa kazi kwa jina. Alimwita mara tatu kwa jina lake. Badala ya kusema mitume alisema, Simoni Petro lisha kondoo zangu, Baadaye akamtaja kwa jina kwamba, achunge kondoo zake.
Watu wenye wito wa pekee mara nyingi wanashangaa kwa nini hawasaidiwi au kupunguziwa mzigo, mara nyingi wanajiuliza, “kwani watu wengine hawaoni umuhimu wa jambo hili?” Yesu alipokuwa akiomba alishangaa mitume wake wakilala usingizi, alijaribu kuwaamsha mara kadhaa lakini bado walilala. Ninaamini ni kwa sababu wito wa wokovu si wa kwao, ulikuwa ni wa Yesu Kristo peke yake. Kwenye familia kunaweza kukawa na watoto wengi lakini si wote wanakuwa na mzigo wa kuwasaidia ndugu na jamaa, mara nyingi mzigo wa kusaidia wazazi na ndugu unaweza kumwangukia mmoja. Mwenye mzigo huo (wito wa kusaidia) huwa anatamani apate msaada na mara nyingi haiwi hivyo kwa kuwa ameitwa kwa jina lake.
Ili kijana afanikiwe ni muhimu ajue wazi kwamba kati ya vijana bilioni 1.8 waliopo duniani ni yeye tu ameitwa tena kwa jina lake. Ili mtu mwenye wito wa pekee afanikiwe ni lazima ajue kwamba katika dunia hii yenye watu bilioni nane ameitwa peke yake, tena kwa jina lake. John Wesley akitambua hili alisema, “Naona dunia nzima kama parokia yangu”.
Endelee kubakia kilele…..mpaka wiki ijayo shalom.

0 comments :