Mimi si sehemu ya .......

12:45:00 PM Unknown 0 Comments


MIMI SI SEHEMU YA TAKWIMU MBAYA
(I’m not a bad statistic)
Januari tano 2017, nikiwa kwenye daladala  nilisikia kituo kimoja cha redio kikitoa takwimu kwamba, kwa mwaka 2017 ambao ulikuwa na siku tano tu tangu umeanza kwamba, tayari watoto laki tano na themanini na kenda (581,000) wameshatolewa kabla ya kuzaliwa.  Wastani wa kutoa mimba kwa siku ni watoto laki moja na kumi na sita kwa siku (116,000). Je, wewe ni sehemu ya takwimu hizi za mauaji ya kukusudia?
Hivi juzi juzi nchini Tanzania tumeona dawa za kulevya zikitafuna vijana, hususani wasanii wa kizazi kipya na waigizaji. Utumiaji wa mihadarati, pombe na aina nyingine za dawa za kulevya zinawaangamiza vijana kwa kasi ya ajabu. Je, wewe ni miongoni mwa waathirika hao?
Wakati takwimu za uovu zinaongezeka, wakati mambo yakiendelea kutisha katika ulimwengu huu, ni vizuri pia uchunguze nini kinaendelea katika ulimwengu wako. Ulimwengu wako ni moyo wako. Inawezekana baada ya siku moja na wewe ukaingia katika takwimu mbaya za ulevi, utoaji mimba, utazamaji wa picha chafu, ubakaji, wizi, utumiaji wa dawa za kulevya na kadhalika. Ni rahisi kuwa sehemu ya takwimu mbaya kuliko kuwa sehemu ya takwimu nzuri.  Chukua hatua, soon you may become a statistic! Mhubiri 9:12
Mwaka jana nilipata masomo mazuri kutoka kwa rafiki zangu Kassimu na Faraja, ambao mara kadhaa tumekuwa tukienda kunywa maziwa pamoja nyakati za jioni. Kassimu alitueleza jinsi mama yake mlezi alivyomuhusia kwamba, akitaka kuoa aangalie namna ambavyo mchumba wake anatatua matatizo. Mamaye alimwambia, wako watu wanatatua matatizo kwa kujiua, ukimuudhi anajiua na anaamini kwa njia hiyo ya kukatisha maisha yake ametatua tatizo. Kwa mtu mwenye kufanya kuuchukia uhai wake kama njia ya kutatua matatizo punde si punde ataingia katika takwimu za marehemu. Atatajwa kati ya waliojinyonga ambao ni wale wauchukiao uhai. (Mhubiri 2:17)
Ziko takwimu za talaka, ziko za wasio olewa na wanataka kuolewa, ziko pia za umasikini. Umejipanga vipi ili kuepusha haya? Ziko takwimu za magonjwa ziko pia za afya njema. Kila jambo lina sababu yake na hivyo linaweza kuzuilika. Ziko takwimu za wasio na kazi na wana uwezo wa kufanya kazi, ziko za wenye vipaji na serikali haijawaona na vipaji vyao. Kama serikali haijakuona ni muhimu ujione na ujitambue. Yusufu alijitangaza na kukitangaza kipaji chake, alimtuma mtu akakielezee kipaji chake. Mwanzo 40:14
Naamini 2017 ni mwaka wako wa kutoka katika takwimu mbaya mpaka nzuri. Hali mbaya haitajibadili yenyewe, bali inabadilishwa na watu kama wewe. Ifanye 2017 kuwa mwaka wako wa kuamka kama ulikuwa umelala, ufanye mwaka 2017 kuwa mwaka wa kutuma barua nyingi za maombi ya kazi. Uwe mwamini wa dini ya bouncebackability (uwezo wa kuanguka na kusimama kwa kishindo). Ni ule uwezo wa kutoka katika uathirika mpaka kuweza kuathiri jamii zetu (positively).  Ni ile hali ya kuifanya hali mbaya ikuzalie mambo mazuri kabisa.
Wakati natafuta kazi nilikutana na mtu aliyenunua stamp hamsini za barua za kuombea kazi, wakati huo nakutana naye alikuwa ametuma zaidi ya barua 50 bila ya kupata kazi. Mimi nilikuwa nimeanza kuchoka na kukata tamaa wakati hata barua kumi (10) zilikuwa hazijatimia. Huenda wewe pia unaanza kuchoka wakati hata barua ishirini hujafika. Amka na endelea Mungu wa mbinguni na afanye 2017 isiishe uwe kazini.
Mwombe Bwana ili mwaka huu, 2017 uwe mwaka wa majibu yako na mabadiliko yako. Uhamishwe kutoka takwimu zenye kuhuzunisha mpaka zenye kufurahisha sana. Katika mchakato wa mabadiliko kila siku ni muhimu, katika mchakato wa kuacha kutumia vilevi kila saa ni muhimu. Hatuwezi kuitawala siku kama hatukutawala saa, hatuwezi kutawala mwaka kama hatukutawala mwezi. Hatushindi mara moja kwa mwaka mzima, bali tunashinda kila siku ya mwaka katika BWANA (Daily victory in Jesus). Ukitaka kubadili mtindo wako wa maisha mara baada ya kumpokea Yesu basi itakupasa ubadili mtindo wako wa maisha ya siku.
Tukutane kileleni.

0 comments :