Mungu anaheshimu chanzo chako

12:53:00 PM Unknown 0 Comments


MUNGU ANAHESHIMU CHANZO CHAKO
(Heshimu ulikotoka)
Ni usemi wa kawaida kwamba usidharau ulikotoka, au usisahau kwenu. Mungu anaheshimu walio kulea, wazazi wako, walezi, nchi unayotoka, anaheshimu pia kanisa ulilotoka hata shule uliyosoma awali.
Uhai wako umefungwa na chanzo chako, maendeleo yako ya kudumu yanategemea sana uhusiano wako na chanzo chako. Taasisi zinaweza kuwa chanzo chako, wazazi ni chanzo chako pia. Epuka kuwa mjane au mgani ukiwa angali kijana.  Ameandika mwalimu Mwakasege, “Unataka kujua mchumba wako ataishi miaka mingapi? Chunguza uhusiano wake na wazazi wake.”
Vyanzo vyetu ni vingi, vipo vya kiroho, kimwili, kifedha, kitaaluma na hata kimaisha. Wako waliotuzaa kwa kutupa mitaji, wako waliotupa ushauri, na wako pia waliotuadabisha ili tufanye mambo ya msingi. Usidharau shule uliyosoma, usidharau chuo ulichosoma, usidharau hata kanisa lako mama. Mungu anaheshimu chanzo cha awali (primary producer) na ameufunga uhai wako na chanzo chako cha awali. Ukitoka toka kwa heshima na amani.
Unapaswa kuheshimu wazazi wako wa kiroho, unapaswa kuheshimu kanisa ulilotoka kabla hujaanzisha huduma yako. Ustawi wako katika huduma mpya unategemea namna ulivyoondoka katika chanzo chako. Si vyema kutukana au kutamka maneno mabaya dhidi ya chanzo chako. Usidharau wale waliokuhubiria injili ya kwanza ni watu muhimu kwako.
Kanisa katoliki ni kanisa mama na linamchango mkubwa katika uenezaji wa injili na huduma za jamii. Naliheshimu kanisa Katoliki kwa mchango wake mkubwa wa kuzaa madhehebu mengi mno ya Kikristo, umewahi kuwaza nini kingetokea kama kanisa hili kongwe lingesambaza uislamu au upagani.  Siku nilipowaza kwamba, ingekuwaje kama kanisa lingeeneza uislamu kupitia huduma zake za jamii (shule, elimu, maji, ungozi na ushawishi) nilijikuta nikilipatia heshima badala ya kuona mapungufu yake kama wengi walivyozoea kutazama.
Haya ni maneno ya heshima kutoka kwa Strive Masiyiwa bilionea mwafrika aliyeitikia wito wa kikao cha Papa Francis na mabilionea wa ulimwengu. Bilionea huyu si Mkatoliki ila ni mkristo tu aliyeokoka alisema, “Mimi si mkatoliki, lakini ninatoa heshima kubwa kwa kazi ya awali ambalo kanisa hili limeifanya”.
Kila mahali ambapo biblia imetaja chanzo imetaja pia uhai, maana yake uhai wako unaweza kuathiriwa na uhusiano wako na chanzo. Kumbukumbu la torati 22:7 na Kutoka 20:12
Ukiwaheshimu wazazi utapata miaka mingi na heri duniani, kwa sababu wazazi ni chanzo chako. Ukimkuta mama wa ndege na makinda yake katika kiota maandiko yanasema, usimuue huyo mama ili siku zako ziwe nyingi. Ni kwa sababu huyo mama ni mzalishaji (producer) anauwezo wa kukuzalishia sana. Wafanya biashara wanaheshimu kampuni mama, wanawakumbuka waliowapatia mitaji na kuwapa hisani.  Wafanya kazi wanaheshimu kazi zinazowapatia kipato chao kila mwaka. Rafiki yangu MC Mzonya hupenda kusema, “Chezea mshahara usichezee kazi.” Kazi ni chanzo chako, inahitaji kuheshimika.
Nakutakia heri katika 2017 BWANA  akupe uhusiano mzuri na chanzo chako.

0 comments :