Enendeni mkabadilishe .....

3:18:00 PM Unknown 0 Comments


ENENDENI MKABADILISHE UTAMADUNI WAO
(Mbingu duniani)
 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.” Marko 16:15
Wakristo wa sasa wanaogopa ulimwengu na mifumuo yake, ilhali BWANA ameagiza akisema enendeni ulimwenguni kote. Kanisa linalopatikana ulimwenguni ndilo kanisa lenye bidii. Kanisa lazima lipenyeze katikati ya mifumo ya kifedha, utawala, ulinzi, elimu, habari, sayansi, bunge na tasnia nyingine zote.
Kanisa limeokolewa ili likaokoe, ‘she was delivered to deliver’, wakristo hawapaswi kujifungia ndani bali wanapaswa kuonekana mitaani, misibani, redioni, magazetini, mashuleni, vyuoni na katika maeneo ya kazi wakimshuhudia Yesu kwamba, ni Kristo.
Jijini Dar-es-Salaam maeneo ya Tegeta kwa ndevu kuna mkusanyiko wa watu na pembezoni mwa ile barabara liko kanisa moja. Jioni watu wa kanisa lile hutoka nje na kuanza kuhubiri, na kwa kuwa kanisa lao liko karibu na soko na maduka injili yao husikiwa na wengi. Mkao wa lile kanisa [ingawa liko katika hifadhi ya barabara] unatufundisha sisi sote kama wanakanisa namna tunavyotakiwa kukaa kiroho kwa ushuhuda katikati ya jamii zetu. Kanisa halina tofauti na wamachinga katika kuenenda kwake kiroho lisikubali kwenda pasipokuwa na watu.
John Wesley ni moja ya wahubiri wa injili na wahudumu waliofanya kazi kubwa katika kumtangaza Yesu Kristo. Moja ya kauli zake alisema, “Naona Dunia yote kama parokia yangu.” Alikua na kiu ya kuinjilisha iliyomfanya asione mipaka iliyopo ulimwenguni. Unapotazama dunia kama parokia yako maana yake unajipa wajibu mkubwa wa kuwahudumia na kuwalisha kondoo wa BWANA. Cha kushangaza ni kwamba, wakati Wesley anapanga kuinjilisha dunia yote wengi hawana mpango wa kuinjilisha hata familia zao. Hawataki kujisumbua kupeleka ujumbe katika kijiji chao, shuleni aliposoma au katika jumuiya anayosali.
Yesu aliposema twende ulimwenguni alitaka utamaduni wa mbinguni uje duniani (Heaven on Earth). Agizo lake lililenga mapinduzi ya utamaduni. Alitaka wakristo waende katika sehemu tisa muhimu kwa kila taifa na kuweka sura ya injili katika nyanja hizo zote.
Kila taifa lina vitu (componentxs) vifuatavyo ambavyo ni kazi yetu kupeleka nuru katika maeneo haya:
  1. Familia -Ndiyo msingi wa kila jamii na taifa na ni mahali ambapo tunu huzaliwa. Utamaduni wa ki-kristo unapaswa uanzie hapa.
  2. Habari na mawasiliano - kazi yao ni kutangaza na kukuza tunu zilizokubaliwa na jamii ambayo msingi wake ni familia. Wakristo ni lazima wamiliki vyombo vya habari ama wawe watangazaji ili watangaze tunu za Kimungu. Kilichopo sasa ni vikaptura na miziki ya hovyo.
  3. Elimu - Hurithisha tunu na maarifa yaliyokubaliwa na jamii hiyo kutoka kizazi hadi kizazi. Mchungaji Oyadepo na Mesa Otabil wamefanya vizuri kwa kufungua vyuo vikuu ili maadili ya kikristo yajulikane kwa wanafunzi.
  4. Ulinzi na Usalama -Hulinda taifa na mifumo yake, mara nyingine majeshi yamewasaidia waovu kumiliki na kutawala. Ni kutokana na watu wa Mungu kutokuwepo katika nyanja hiyo.
  5. Dini - Kila taifa linafanya ibada. Wakristo wanamwakilisha Mungu wa kweli katika mataifa yao hivyo ni lazima Mungu wetu aheshimiwe kupitia sisi kama nyakati za Eliya. Gidioni alivunja sanamu za baba yake na Nabii Eliya aliwachinja manabii wa baali na baali hakuweza kuwatetea. Mungu wetu ni Mkuu kupita miungu yote.
  6. Bunge - Si tu kwamba bunge hutunga sheria bali wabunge pia hutunga yale wanayopendeza mbele za Mungu wao. Mfano mzuri ni suala la mahakama ya kadhi nchini Tanzania, kama idadi ya wabunge wakristo ingekuwa ndogo leo tungeongea lugha nyingine. Kuna umuhimu wa wakristo kuwa wabunge.
  7. Mahakama - Huhusika na utoaji wa haki. Katika ulimwengu huu wenye vitisho, rushwa na uchawi ni watoto wa Mungu tu ndio huweza kusimamia haki. Wana sheria wadhalximu ni wengi, vijana tusome sheria tukamtetee Yesu kisheria na kuwapa watu haki zao bila ya kuwabagua.
  8. Kazi na Biashara - Ndiyo siri ya utajiri ilipo. Watu hawaheshimiwi kwa upako tu, bali kazi pia huleta heshima. Hekima ya masikini hudharauliwa, wakristo wafanye kazi (halali); wawe matajiri, wakitumia mali zao kusukuma gurudumu la injili. Luka 8:3
  9. Sayansi na Teknolojia - Ndiyo uwanja au jukwaa la kisasa. Zamani tulikutana uwanjani leo hii mamilioni ya watu wanakutana katika mitandao ya kijamii. Huwezi kuinjilisha kwa ufanisi wa juu kabisa ikiwa unachukia facebook na twitter. Kanisa linatakiwa liende ulimwengu uliko, leo hii vijana wengi wako mixtandaoni, kanisa halinabudi kuwafuata huko na kuwasaidia. Kanisa linapaswa liwe la kisasa ili liwainjilishe watu wa sasa kwa njia za sasa.  
WITO:
Wakristo wakikaa katika Nyanja hizo tisa utamaduni wa dunia hii utapotea na ule wa mbinguni utachukua nafasi. Ukiwa ni mkristo na uko katika vyombo hivi ujue cha kwanza kwako si mshahara bali ni ufalme wa Mungu na haki yake. Wakristo mjitokeze katika kuanzisha na kumiliki vyuo vya elimu na vyombo vya habari.
Life Minus Regret team inakutakia mwaka wenye Baraka zote kutoka kwa BWANA 2017.

0 comments :

Tunaishi mara moja tu!

12:10:00 PM Unknown 0 Comments


TUNAISHI MARA MOJA TU.
(Tumia vizuri awamu yako ya maisha)
“tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.” 2 Kor 5:14
Tungelikuwa tunaishi mara mbili angalau mtu angeweza kutumia awamu ya kwanza kuishi kwa ajili yake mwenyewe na awamu ya pili kuishi kwa ajili ya Yesu Kristo. Kizuri zaidi ni kwamba, tunaishi mara moja, hakuna mtu mwenye awamu mbili za maisha. We live only once!
Katika kuishi kwetu mara moja ni lazima mtu aamue kuishi kwa ajili yake mwenyewe au kuishi kwa ajili ya Kristo. Wewe unaishi kwa ajili ya nani? Wako wanaoishi kwa ajili ya kazi zao, wako wanaoishi kwa ajili ya michezo, wako wanaoishi kwa ajili ya burudani na wako wenye hekima wachache wanaoishi kwa ajili ya Kristo.
Oswald J Smith mwandishi wa kitabu nilicho kisoma na kukirudia zaidi ya mara mbili, “The Consuming Fire” anasema, “I have only one life to live and I want to invest it for Thee” kwa tafsiri yangu, “Nina maisha haya tu, ninataka niwekeze kwa ajili yako BWANA”
Katika mstari unaotuongoza pale juu 2 Kor 5:14 Paulo Mtume anasema wazi Yesu anatutaka tusiishi kwa ajili ya nafsi zetu wenyewe bali kwa ajili yake. Jiulize, unaishi kwa ajili ya Kristo au kwa ajili yako mwenyewe?
Asubuhi mpaka jioni unafanya nini? Wanaoishi kwa ajili ya Kristo huomba kwa saa moja na kusoma neno kwa angalau saa moja. Pesa zako zinatumikaje? Wanaoishi kwa ajili ya Kristo hutumia pesa zao kwa uinjilishaji. Luka 8:3
Nakualika ujitoe kwa Yesu na kuishi kwa ajili yake kuanzia leo: Sema sala hii, “Ee BWANA YESU mimi ni mwenye dhambi na wewe ni mwokozi wangu. Naomba unisaidie kuanzia leo niyatoe maisha yangu kwako, wala nisiishi tena kwa ajili yangu na kwa ajili ya Dunia badala yake nikufuate wewe milele. Amina.”
Nakutakia msimu mwema wa sikukuu, Shalomu….
>

0 comments :

Uaminifu! Tabia gani bora kama hii?

11:37:00 AM Unknown 0 Comments


UAMINIFU! TABIA GANI BORA KAMA HII?
(Si vema kufanana na watu wa dunia hii)

Ilikuwa mchana wakati wa chakula na nilikuwa nikibadilishana mawazo na wafanyakazi wenzangu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali. Mkononi mwangu kama ilivyoada nilikuwa na kitabu kizuri, “Money won’t Make You Rich” kilichoandikwa na mchungaji Sunday Adelaja.
Na mara rafiki mmoja akaniambia nimweleze kanuni za kumsaidia kufanikiwa kiuchumi, na mimi kwa haraka kama daktari fedha vile nikaanza kumweleza. Kanuni zote nilizomweleza zilikuwa zikikubaliana na neno Mungu. Mwishowe akazikataa kanuni zangu na akazitaja za kwake za kufanikiwa haraka ambazo ni, kuuza dawa za kulevya, meno ya tembo na ufisadi. Akasisitiza bila magendo huwezi kuwa tajiri.
Ndivyo walivyo watu wa ulimwengu, wanadai bila kuiba hakuna mafanikio, bila uasherati kabla ya ndoa hakuna ndoa wanasisitiza bila uchafu hakuna usafi. Ibrahimu, Ayubu na Daudi wote walikuwa matajiri katika Biblia na maandiko hayatuoneshi wizi au udanganyifu katika maisha yao, badala yake neno la Mungu linaonesha jinsi walivyokuwa waaminifu.
Mali ya mtu au ya serikali ni kipimo chako cha kuona kama unaweza kuaminiwa na kupewa mali yako mwenyewe. Siku za karibuni nimekuwa katika nafasi mbalimbali za kijamii na kikazi zinazoniwezesha kushika pesa za watu na za Serikali. Na kwa kweli nimekuwa mwaminifu, na Roho wa Mungu amekuwa akinitia moyo kwamba, ukiwa mwaminifu kwa mali ya mtu Mungu atakupa ya kwako mwenyewe, ukiwa mwaminifu katika pesa kidogo Mungu atakupa nyingi. Hujawahi  kuona wauzaji waaminifu huishia kumiliki mali na amana zao wenyewe. Mara nyingi imetokea sawa sawa na neno la Bwana. “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli” Luka 16:10-11
Kwa lugha nyingine kila unapoiba huwa unamwambia Mungu siko tayari kumiliki mali yangu mwenyewe. Vivyo hivyo kila unapozini na kusema uongo huwa unamwambia Mungu kwamba, “sifai kuwa tajiri.” Ni ukweli uliowazi maana kilichozungumzwa ni uaminifu ambao ni zaidi ya kutokuiba. Yusufu alipimwa uaminifu wake kwa kutaka kubakwa na mke wa Potifa. Kitendo cha Yusufu kukimbia na kukataa uovu huo kilituma ujumbe kwa Mungu kama huu, “Yusufu yuko tayari kuwa tajiri mpatie.”
Matajiri wengi wanafanikiwa kama kuku. Kuku akilishwa vizuri na kunawiri ni ili achinjwe. Matajiri wengi wako tayari kwa kuchinjwa. Utasikia amejinyonga, utasikia amechomwa kisu, utasikia amekufa kwa sababu ya kansa ya koo iletwayo kwa kupitia kuvuta sigara. They get rich only to die young!
Ni heri maskini mwaminifu kama Lazaro kuliko tajiri mwizi na fisadi. Dunia inadanganya inasema kipagani eti, ni sawasawa kuiba ili kuendelea, “The pagan society says,’ its okay, to lie, steal and cheat to get ahead’.” Uaminifu unazawadi yake, raha yake na fahari yake. Watu dhaifu na legelege hawawezi kuwa waaminifu, uaminifu ni haiba ya juu kabisa si rahisi kuipata kwa watu ambao hawajaunganika na Mungu.
Nakutakia msimu mzuri wa Krismas na mwaka mpya 2017, barikiwa tena Mungu na akuhifadhi daima.

0 comments :

Wote wametenda dhambi

6:17:00 PM Unknown 0 Comments


WOTE WAMETENDA DHAMBI
(“kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;” Rum 3:23)
Biblia inasema, wote, haisemi kabila fulani au nchi fulani tu ndiyo imetenda dhambi. Hakuna kabila wala nchi ya wenye dhambi, sote tumetenda dhambi. Kupitia dhambi ya Adam makabila yote, wanadamu wote na nchi zote ziliingizwa katika hali ya dhambi. Hapa hakuna wa kumbagua mwingine.
Nimewahi kusikia watu wakibaguana kikabila wakisema usioe kule na wengine wakidai usiolewe katika kabila lile. Kigezo chao ni dhambi ambazo hata wao na nchi zao, na jamaa zao wanatenda. Katika agano jipya tunapata makundi mawili tu ya watu, waaminio na wasio amini. Biblia inasema, waaminio wataokoka na wasio amini wamekwisha hukumiwa. Imani ndiyo kigezo cha kuungana na mtu fulani au kutokuungana naye.
Nadhani mstari huu ni mstari ambao haujaeleweka miongoni mwa wengi. Sote tuliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ambao kwangu mimi nasema sura hiyo ni utukufu. Biblia inasema, wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu; kwa hiyo sura ya Mungu ambayo ni utukufu wake katika maisha yetu ilipungua kwa sababu ya dhambi. Rum 3:23
Kuna mtazamo wa kuitazama nchi ya Israeli kama bora kuliko nyingine, na wengine hudhani kwamba, ni Baraka kwenda Israel jambo ambalo si kweli kabisa. Wakristo hatuna hija ya kusafiri bali ya imani katika Yesu Kristo. Israel kama taifa hawakumkubali Yesu na ndio sababu iliyomfanya Mungu aachane na wito wa ngazi ya taifa na kuelekea kwa ngazi ya mtu binafsi kama yanenavyo maandiko, “bali wote waliompokea…” Yohane 1:12
Je, unataka kuungane na mtu? Je, unataka kuwa na uhusiano na mtu kibiashara? Unataka kumdhamini mtu? Kigezo si kabila ya au rangi yake, bali unapaswa kuangalia kama ni mmoja kati ya wale wamwaminio Yesu Kristo au lah! Biblia inasema, “Tusifungiwe nira isivyosawasawa na mtu asiye amini.” Inakataza kuunganishwa au kuungana isivyo faa na mtu asiye amini.
Badala ya kunyoosheana vidole ni vema wote tungefika alipofika John Newton yule mwandishi wa wimbo wa, ‘amazing grace’ aliyesema, “Ninachojua mimi ni mwenye dhambi mkuu, Na Yesu Kristo ni mwokozi mkuu.”
Kama unaamini Yesu alikufa kwa ajili yako basi ni muhimu pia uamini ulikuwa uu, mwenye dhambi, kama usingelikuwa na dhambi asingekufa kwa ajili yako. Nina amini hakuna aliyezaidi ya mwingine kikabila, kimataifa wala kiukoo, sote tumetenda dhambi na kupoungukiwa na utukufu na hivyo tunamuhitaji Yesu Kristo, Great Saviour!  Mpaka wiki ijayo shallomu.

0 comments :

Mara nyingi sana

5:45:00 PM Unknown 0 Comments


MARA NYINGI SANA
(Saba mara sabini)
Wanaofuatilia huduma ya Uinjilisti watakuwa wanamfahamu au kumsikia ndugu Jimmy Swaggart, yeye hupenda kujiita brother Swaggart, ni mwinjilisti mwenye alama ya aina yake na mwenye kutembea mwendo mrefu kwa miaka kadhaa katika huduma aliyopewa. Ameonja kuanguka na kusimama na hapa anatoa funzo: “Msalaba wa Yesu kila siku unatenda kazi kamwe haushindwi, ni mimi na wewe tunaoweza kushindwa. Sisemi kama ikitokea ukianguka (maana utaanguka kweli) kama hautaacha kumwamini Yesu hata katika anguko lako, Yeye Bwana Yesu hatakuacha na mwishowe atakusimamisha maana hujaacha kumwamini hata katika kuanguka kwako.”
Kwa tafsiri yangu Jimmy anasema, kuanguka kupo, ndio maana haoni sababu ya kusema ikitokea ukianguka maana anajua itatokea. Katika huduma yake ameanguka na kusimama, anajua machungu ya kuanguka, anasisitiza tusikate tamaa maana msalaba wa Yesu unauweza wa kuokoa nyakati zote. Asubuhi moja nikiwa katika Studio za Ileje Fm radio msikilizaji aliniuliza kama, Mungu anaweza kusamehe dhambi kubwa. Nilimjibu, “Ndiyo anaweza, mara nyingi tu.” Si tu kwamba Mungu anasamehe bali anasamehe mara nyingi. Many times!
Baadaye nilimpa mfano tuliopewa na paroko kanisani kwetu, nanukuu: “mtu mmoja alimuuliza padre mmoja akisema, ‘padri nimemuua bosi wangu, Je! naweza kusamehewa? Padri akamjibu akasema, ‘unaweza kusamehewa bila shaka’ yule bwana akaendelea akasema, ‘wakati nikimuua bosi wangu dereva wake aliniona, ili kufuta ushahidi nikamuua na dereva je, naweza kusamehewa? Akamjibu ndiyo bila shaka. Akamwambia, ‘Padri niwie radhi kwani, nilipokuwa nikimuua dereva mke wa bosi aliniona ikabidi nimchinje na yeye pia. Vipi na hilo nalo Mungu anaweza kusamehe? Padri akajibu ndiyo bila shaka.’”
Usikate tamaa  Mungu anaweza kukusamehe haijalishi umefanya nini. Somo kuu la mfano hapo juu ni hili; Si kwamba Mungu anaweza kusamehe tu, bali anaweza kusamehe mara nyingi zaidi.
Mungu ni upendo. Maandiko yanasema upendo husitiri dhambi nyingi. Usipokata tamaa Mungu hatakuacha, na hata ukikata tamaa yeye ataendelea kukutafuta maana wokovu wako ni muhimu. Si sisi tuliomtuma mjumbe aende mbinguni kumshusha Yesu ili aje atuokoe bali ni Mungu aliyemtuma Yesu ashuke kutuletea wokovu.
Kila mtu anaweza kusamehe lakini si kila mtu anaweza kusamehe mara nyingi. Tabia kuu ya kimungu (great godly character) haiko katika kusamehe tu, bali iko katika kusamahe mara nyingi zaidi. Hata wapagani kuna nyakati husamehe, lakini hawawezi kufanya hivyo zaidi ya mara saba. Mitume walidhani, unaweza kusamehe mara saba tu, na kumbe ni zaidi ya hapo.
Msamaha unaponya mahusiano, unaponya ndoa, unaponya kanisa na nchi kwa ujumla. Asiye mfuasi wa msamaha ni mfuasi wa vita. Kuna wengine husema jino kwa jino, hili linawezekana ikiwa tu aliyekukosea ni mdogo. Ikiwa unapenda kulipiza kisasi badala ya kusamehe napenda kukuuliza, Je, utafanya nini ikiwa aliyekukosea anazo nguvu kuliko wewe? Je, utafanya nini ikiwa aliyekukosea ni mkuu sana? Naamini utamwachia Bwana maana, kisasi ni juu yake. Kama hatuwezi kusamehe hatuwezi kumwachia Mungu, kwani tutaona kama vile Mungu hawezi kumwadhibu vizuri mhusika.  Jifunze kusamehe mara nyingi zaidi, tamka msamaha sirini na hadharani pia, wewe uliyesamehewa makosa yako unawezaje kushindwa kusamehe wengine? Mathayo 6:14-15
Leo ninakuachia kazi ya nyumbani (home work) ifuatayo, piga simu, tuma meseji ya kusamehe na kama aliyekukosea yuko karibu mwambia nimekusamehe.
BARIKIWA

0 comments :