Ni atakayevumilia
NI ATAKAYEVUMILIA MPAKA MWISHO
(Endelea kufanya, anzia ulipoishia)
Taasisi
ya taarifa za takwimu za kazi nchini Marekani (US Bureau of Labor Statistics Information) inaripoti hivi, “katika nyanja
zote za biashara, asilimia arobaini na nne (44%) ya makampuni mapya hutoweka
ndani ya miaka miwili na asilimia sitini na sita (66%) hutoweka ndani ya miaka
minne ya uhai wa makampuni hayo.”
Mwisho
wa siku si yule aliyeanza safari, wala si yule mwenye nguvu, bali ni yule aliyevumilia
na kufika kileleni. Biblia haisemi ajuaye sana ataokoka, wala haisemi anayekaa
karibu na kanisa ndiye atakaye okoka, badala yake imenena, “atakaye vumilia
mpaka mwisho.” Kuanzia katika mafunzo ya kawaida kabisa ya maisha mpaka kwenye
neno la Mungu ni mvumilivu ndiye aliyetabiriwa kushinda.
Kwenye
ujasiliamali watu huambiwa, “winners
never quit, quitters never win.” Uzoefu wa maisha unampa nafasi kubwa
mvumilivu kuliko mtu mwenye akili kubwa lakini ana tabia ya kukata tamaa. Kaka mmoja
alikuwa na nia ya kuwa daktari (medical
doctor) na aliendelea na nia hiyo licha ya vikwazo vingi. Kikwazo kikubwa
kilikuwa ni kupata sifuri (division zero)
kidato cha sita. Lakini ilikuwa ni habari njema kwangu kusikia kwamba, mwakani
atamaliza miaka yake mitano na kupata alichotamani maishani mwake kwa siku
nyingi, udaktari. Daraja la mwisho limeshindwa kumkwamisha kwa sababu ya
uvumilivu wake.
Rafiki
yangu aliandika, “ukichoka usiache, jifunze kupumzika.” UKiwa kwenye uhusiano
jifunze kutafuta njia ya kuendelea na si ya kutokea. Ukishindwa kupambana na
changamoto katika uhusiano omba kupumzika ili upate muda wa tafakari na maombi.
Moja ya changamoto ni tamaa isiyozuilika, ukikaa pembeni utakumbuka kwamba,
kuna faida katika kumtii Mungu na raha ya ajabu hutokea ikiwa miili yetu
itatumika kama mahekalu ya Mungu. Dakika moja ya tafakari ina maana zaida
kuliko masaa mengi ya majibizano.
Mchana
mmoja Dominick Mzonya, aliniomba nimsindikize ili akazungumze na kuwatia moyo
wanafunzi. Katika moja ya mambo aliyowasisimua kwayo ni kumbukumbu ya tafiti ya
makundi matatu ya watu. Makundi hayo matatu yalihusisha watu wenye uwezo wa juu
(akili sana), wenye uwezo wa kati (kawaida), na wale wenye uwezo wa chini. Mwisho
wa siku katika kutazama maisha ya watu hawa mafanikio yao hayakutokana na akili
au uwezo wao bali yalitokana na uvumilivu wao. Wa kundi la mwisho alipovumilia
alifanikiwa, wa kundi la kwanza alipovumilia alifanikiwa hatimaye hata wa kundi
la katikati alipovumilia bila ya kukata tamaa alifanikiwa. Nguvu haipo katika
akili kubwa (High IQ) bali katika
kufanyia kazi upendacho, kujitoa, na kudumu bila ya kukata tamaa. Christiano
Ronaldo anaonekana kusifiwa sana katika soka moja ya siri ya mafanikio yake ni
hii, “Ni wa kwanza kuingia uwanjani kwa mazoezi kabla mchezaji mwingine awaye
yote hajaingia na ni wa mwisho kutoka wakati wote wameshamaliza mazoezi.”
Washindi
ni wavumilivu, sifa nyingine wanazopewa na watu ni urembo tu. Washindi hufanya
mazoezi kila siku kwa uaminifu mkubwa. Mwanafunzi hawezi kufaulu mtihani kwa kusoma
siku moja nzima yenye saa 24. Bali mwanafunzi atakayesoma kwa saa moja kila
siku ndani ya siku 24 atakuwa bora kupita yule aliyesoma usiku na mchana.
Ingawa wote watatumia saa ishirini na nne lakini yule wa kila siku saa moja
anaonesha kudumu na kujizatiti katika maandalizi kwa siku ishirini na nne,
wakati yule aliyekesha usiku na mchana anaonekana kudumu kwa siku moja tu.
Kila
mtu ni mvumilivu lakini si mpaka mwisho, wengi ni mpaka katikati. Kila kitu ni
kigumu ila ni lazima tudumu katika kukifanya. Usikate tamaa endelea kuomba
kazi, endelea na kipaji chako, wekeza muda mwingi katika kazi zako. Hakuna
kuchoka, hakuna kuzimia mpaka tumefika kileleni. Ili timu yetu, “Life minus
regret program” iweze kutoa makala hizi kila wiki inatulazimu kusoma kila siku,
kusali na kuandika kila wiki. Usisahau tuna majukumu yote kama wewe. Usiache,
usirudi nyuma, na Mungu atakusaidia na kukusimamisha. Mapambona yanaendelea,
well done is waiting for you.
0 comments :