Mbona umeacha
(Hakikisha unaanza tena)
Ulianza
kusali vipi mbona umeacha? Ulianza biashara vipi mbona umeishia njiani? Ulianza
kusoma kozi ile vipi mbona umekwama? Kwa nini umeacha kufanya mazoezi? Tatizo
liko wapi? Hauoni kwamba, huu ni muda sahihi kwako kurejea kwa kishindo.
Katika
siasa kuna neno maarufu liitwalo, “bouncebackability”
ambalo linaelezea uwezo wa mwanasiasa kuinuka tena. Anaweza kuonekana ameishiwa
sera au ameanguka kabisa, na ghafla anasimama na kushinda kwa kishindo. Ufufuko
wa Yesu nao ulikuwa na sura hiyo. Kwa siku mbili na zaidi alizokuwa kaburini
wengi walidhani ameshindwa kabisa, hata mitume wake walikata tamaa, siku ya
tatu alifufuka na kutoka mzima.
Hii
ni wiki yetu ya kusimama tena na kurejea katika nafasi zetu kwa kishindo. Ni wiki ya kumwomba BWANA, afufue kazi zake
ndani yetu. Inawezekana wewe ni mhubiri mfu, ni kiongozi mfu, ni mkristo mfu au
ni mhandisi mfu. Lakini ni saa yako na yangu kumwambia, “EE BWANA FUFUA KAZI
ZAKO NDANI YANGU”
Ni
muhimu kumaliza ile kazi tuliyoianza, ni muhimu zaidi kuanza tena kutokea pale
tulipoishia. Mwanariadha mmoja wa Tanzania akiwa katika mashindano ya Olimpiki
aliendelea kukimbia na kumaliza mbio hizo ndefu licha ya kuumia. Napenda maneno
ambayo mtangazaji alimpamba mwanariadha huyo aliyekuwa majeruhi alisema: “Sikutumwa
na Nchi yangu kutoka mamilioni ya maili ili kuanza mbio, bali nimetumwa
kumaliza mbio.”
Ni
kweli kabisa hatukuitwa kuanza bali kumaliza, hatukuitwa kuwa washiriki tu wa
maisha bali tumeitwa kuishi kama washindi. Je, Nguvu yetu inatoka wapi? Nguvu
yetu si tu ile itokanayo na chakula tunachokula yaani, protini, vitamin, maji
na vyakula vya nguvu. Nguvu yetu ni zaidi ya chakula tulacho, nguvu yetu yatoka
kwa Bwana Mungu aliyeziumba mbingu na nchi. Kwa Yeye (Yesu Kristo) tunayaweza
mambo yote na tunahakika tutamaliza.
Kwa
kuwa bado tuko hai basi kila kitu kinawezekana. Napenda mchezo wa mieleka, somo
kubwa katika mchezo huu ni kwamba, kuwekwa chini si kushindwa na kupigwa sana
si kupoteza mchezo. Mara nyingi katika mchezo huu hata aliyechoka huweza
kuibuka mshindi. Ni siku yako leo, toka kaburini, anza tena, maliza kazi yako,
Mungu Baba na afufue kazi yake ndani yako katika jina la Yesu Kristo. Amen
0 comments :