Toa huduma bora, Uza bidhaa bora

11:44:00 AM Unknown 0 Comments


 
TOA HUDUMA BORA, UZA BIDHAA BORA
(Ubora si ajali, “Quality is not accident”)
Tangu zamani tumesikia kwamba, ukimpa mtu samaki utakuwa umemlisha kwa siku moja lakini ukimfundisha mtu kuvua samaki utakuwa umemlisha kwa maisha yake yote. Kumpa mtu mtaji bila maarifa ya kufanya biashara ni sawa na bure. Anayekusaidia kuijua teknolojia ya uzalishaji anamsaada zaidi kwako kuliko anayekupatia pesa.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia bara la Ulaya lilijikuta likiwa hoi kiuchumi. Viwanda vyake vingi vilidorora, watu wengi waliuawa na uchumi wake ulikuwa umeanguka kabisa. Marekani iliamua kuisaidia Ulaya katika mpango uliojulikana kama Marshall plan ukiasisiwa na Mwana Amerika George Marshall. Katika pragramu hiyo ya ujenzi wa Ulaya (Uerope Recovery Program) Marekeni ilitoa dollar zake billion 13. Na mara baada ya pragramu hiyo kuisha, uchumi wa nchi nufaika  ulikuwa bora kwa zaidi ya 35% ukilinganisha na uchumi wao kabla ya msaada.

Msaada huo alioutoa Marekani haukuwa katika mfano wa samaki bali ulikuwa katika mfano wa uvuvi. Wahandisi walitoka ulaya na kwenda kujifunza Marekani namna ya kuendesha na kuhuisha tena viwanda vyao, wahandisi wengine walitoka Marekani na kwenda kushirikiana na nchi nufaika. Kupitia kubadilishana wataalamu nchi hiazi zilibadilishana teknolojia pia (transfer technology). Nchi nufaika pia ziliondoa vizuizi vya kibishara na kuamua kushirikiana kitu ambacho kilipelekea kuzaliwa kwa Jumuiya ya Ulaya. UJerumani iliyokuwa ikikabiliwa na shida ya chakula iliimarika sana na  viwanda vyake vya uzalishaji vilihuishwa na kuweza kuzalisha vema.

Ni wazi kama msaada huo ungekuwa ni pesa tu, Ulaya isingelisimama kiuchumi. Pesa mikononi mwa mpumbavu ni kifo. Kabla hujapata pesa lazima uwe na uzoefu na maarifa ya namna ya kuitumia. Mtu mwenye pesa akikutana na mtu mwenye uzoefu na maarifa, pesa zake huenda kwa mtu mwenye maarifa na yeye hubakia na maarifa. Kwa hiyo ili mtu akae na pesa ni muhimu pia awe na maarifa.

Naungana na Donald Trump, Robert Kiyosaki , Anthony Robbins na wengine wengi tunaoamini kwamba mifuko ya hifadhi ya jamii imefeli. Mifuko ya hifadhi ya jamii inawapa watu pesa wakiwa wamechoka na pengine ni wazee yaani, unaweka magurudumu mapya (new tyres)katika injini ya gari  iliyochoka kabisa.

 Inawapa wastaafu pesa bila maarifa wala namna nzuri ya kuzitumia, wengi hawana elimu juu ya usimamizi wa fedha. Hata Marekani ingetoa pesa kwa mtindo wa mifuko ya pensheni kusingelikuwa na mafanikio yoyote katika kuisaidia Ulaya. Mwenye hekima mmoja anasema, “Umewahi kuwaza kitu gani kitatokea ikiwa Mhasibu atafanya ‘wiring’ ya umeme? Umewahi kuwaza kitu gani kitatokea ikiwa Mhandisi atamng’oa mtu meno? Je, nini kitatokea ikiwa mtu ataenda kwa daktari ili kupata ushauri wa nyota?” Majibu unayoyapata ndiyo kinachotokea pesa inapotua mikononi mwa mtu asiyejua namna ya kufanya.

Ili watu wapate uhuru wao kiuchumi na kifedha ni lazima wajipenyeze katika utoaji wa huduma au uuzaji wa bidhaa. Bidhaa zinapaswa kuwa bora, ubora hauji kama ajali ni matokeo ya bidii, maarifa, sadaka na jitihada. (Quality is not an accident) Ile huduma unayoweza kuitoa vizuri na wateja wakaridhika (shule, televisheni, muziki, mgahawa, hoteli, uambaji, uandishi, usisimuaji na usanii) ndio mlango wa utajiri wako. Mpaka watu waingie katika uuzaji wa bidhaa (duka la nguo, duka la vifaa vya magari, mazao ya chakula, duka ya huduma, maduka ya vitabu, viwanda, mazao ya misitu, uandaaji na uuzaji wa samaki, usindikaji n.k) ndipo uhuru wao huja. Ni vema kujifunza teknolojia inayotumika katika kusindika na kuandaa bidhaa mbali mbali.

Sunday Adelaja anasema: “Maombi peke yake hayatoshi, kutoa fungu la kumi peke yake haitoshi”. Utoaji wa huduma nzuri na uuzaji wa bidhaa bora ni jambo muhimu. Ubunifu nao si wa kubezwa, wabunifu wengi ni viongozi. Unaweza kubuni Saluni ya watoto yenye picha za watoto, silabi na picha za Yesu badala ya saluni ambazo ukutani kuna picha chafu za uharibifu.

Wakristo si wana maombi tu, bali ni wauzaji waaminifu, watoa huduma bora, wenye lugha nzuri. Mteja anayekuja katika duka au hoteli ya Mkristo anapaswa kukutana na matunda ya Roho Mtakatifu. Furaha, amani, uvumilivu na mengine mengi ambayo yote si tu kwamba, yatamtukuza Mungu bali pia yatakupatia fedha.

Kila mtu anapaswa awajibike na kujitokeza katika utoaji wa huduma bora na uuzaji wa bidhaa bora. Kutokujiamini kwa watu wengi kunatokana na watu hao kushindwa kumwamini Mungu hivyo kumtanguliza Mungu ni jambo jema lakini si la mwisho. Baada ya kumtanguliza Mungu biashara na utoaji wa huduma ufuate.

Rais Obama akiwataka wananchi wa Marekani kuwajibika alisema, “Hata kama Serikali itatoa elimu bora, hata kama serikali itaweka miundombinu bora ya elimu bado mzazi atawajibika, usitegemee serikali itakuja nyumbani kwako kuzima televisheni ili mtoto wako afanye kazi ya nyumbani (home work) kama mzazi unawajibu wa kuzima televisheni”.

0 comments :

Linda sifa yako nzuri

4:27:00 PM Unknown 0 Comments

 
LINDA SIFA YAKO NZURI
(Mwenendo wangu ni mzuri kuliko uzuri wa huyu dada)
Manukato au marashi husifika kwa kutoa harufu nzuri sana, hata hivyo harufu hiyo haiwezi kwenda mbali ukilinganisha na sifa njema. Sifa njema huenea kijiji kizima, manukato hayana uwezo huo. Sifa njema huenda mbali sana mahali ambapo manukato hayafiki. Nelson Mandela, nani asiye mjua? Yesu Kristo Mfalme, nani aisiyemjua? Askofu Desmond Tutu, nani asiyemjua? Vipi kuhusu sifa za mama Teresa? Sifa za hawa wote zimeenea mno.
Imenenwa katika Mhubiri 7:1a “Heri sifa njema kuliko manukato mazuri” ikiwa na maana, heri mwenendo bora na halisi kuliko mwenendo mbaya na feki. Ikimaanisha heri kuwa na mwenendo mmoja wa kweli kuliko kuwa mnafiki. Heri kuonesha tabia yako ya ndani kuliko kuificha. Manukato au marashi hutoa harufu ambayo kwa asili si ya mtu. Hata kama mtu hujaoga manukato yanauwezo wa kufanya anukie vizuri. Manukato yanaficha uchafu wala hayauondoi. Manaukato yanakusanya uovu na kuupa harufu ya wema.
Jina jema ni jumla ya matendo yako, jina jema ni kitambulisho chako. Marhama au manukato [perfume] hufanya tunukie vizuri hata kama moyoni mwetu tumeoza kwa sababu ya dhambi. Maandiko yanatutaka tuchague jina jema. Ninafananisha jina jema na utakatifu wa ndani na manukato ni harufu inayoficha ile dhambi ikaayo ndani ya mtu.
Siku moja tulikuwa mahali fulani na kulikuwa na dada mrembo kweli kweli. Na wengi walimtolea macho, na rafiki zangu walitamani na mimi nitoe macho. Kwa kweli alikuwa dada mlimbwende lakini haina maana yoyote kama kila tunapokutana na mrembo tunashindwa kujitawala. Kushindwa kujizuia ni dalili ya watu wa siku za mwisho. “…Wasiojizuia…” 2Timotheo 3:3
Rafiki zangu walitaka nichangamkie fursa ya yule dada wakiniambia, “pastor vipi” yaani, “mchungaji vipi” na mimi nikawajibu kizungu, “my character is beautiful than the beauty of this lady” yaani, “mwenendo wangu ni mzuri kuliko uzuri wa huyu dada”. Mara nyingine tumepotea kwa sababu tumekwenda haraka bila ya kujali muda mwingi ambao tumetumia katika kujenga haiba, tabia na wasifu wetu.
Dada mmoja aliniambia kwa masikitiko jinsi sifa yake ilivyoharibiwa haraka na kaka waliyeingia naye kwenye uhusiano. Aliandika kwa huzuni, “ameharibu sifa yangu yote”. Huenda ni sifa ambayo aliijenga kwa muda mrefu ya mwenendo bora. Imeharibiwa katika mwendo wa sekunde tu!
Katika karne hii waaminifu na wenye mwenendo bora wamekuwa bidhaa adimu. Watu hawaamini kama utakatifu unawezekana tena. Hawawezi kukubali kama utawaambia wewe si mlevi wala si mwasherati. Rafiki yangu hupenda kusema, “simba akisema hali nyasi hajidai ndivyo alivyo”.  Leo hii tabia nzuri zimekuwa adimu, dunia haimini kama Simba hali nyasi, inachojua ni kwamba kila mtu ni mwovu tu.
Kuna jambo linashangaza kidogo, wakati mji mzima wa Ninawi ukiokoka, mji mzima wa Sodoma na Gomara uliangamia. Yaani wakati mkoa fulani wote unaokoka mkoa mwingine wote unaangamia. Kanuni ni hii, ni vigumu kumpata mtakatifu katikati ya waovu, na ni vigumu kumpata mtu mwovu katikati ya watakatifu. Miji hupambana kuhakikisha ama ni uovu tu unaoshamiri au utakatifu tu ndio unashamiri. Kwa asilimia hamsini mtu ni mazingira yake. Pastor Sunday Adeleja anasema, “Mazingira yanatutengeneza kwa takribani asilimia 50”  sisi pia ni matokeo ya mazingira yetu.
Kazi ya wahubiri ni kufanya mazingira ya mbinguni yaje duniani, ambayo ni amani, utakatifu na uaminifu. Dunia ni kama msitu mkubwa ambao wanyama wote hula nyasi. Sasa wanyama walao nyasi hawataki kuamini kwamba wapo wasiokula nyasi, simba hali nyasi. Ndivyo walivyo watakatifu katikati ya ulimwengu ambao BWANA mwenyewe amesema ni wa mbwa mwitu. Chukua muda huu kutafakari tabia, mwenendo na haiba yako na kisha amua kubadilika na kuulinda mwenendo wako mzuri. Mpaka wiki ijayo Shallomu…

0 comments :

Moto wa milele upo

2:14:00 PM Unknown 0 Comments



MOTO WA MILELE UPO
(Neno liko kama lilivyo wala si zito)

Ben Carson ni mwanataaluma mstaafu, mwandishi na mwanasiasa ninayempa heshima kubwa. Lakini kuna eneo moja tunatofautiana sana ki-msimamo na ndugu Ben Carson. Ben haamini katika moto wa milele licha ya kwamba, neno la Mungu linasema kuna moto wa milele, linasisitiza waziwazi jehanamu ya moto ipo.

Ben anajenga hoja kwamba, “Mungu hawezi kumhukumu mtu aliyefanya makosa kwa miaka sitini (60) adhabu ya milele labda adhabu ya miaka sitini (60)”. Ben anaona ni afadhali mtu akikosa kwa mwaka mmoja akae Jehanamu kwa mwaka mmoja, ni mawazo yake. Mawazo ya mwanadamu yeyote kama Ben si ya kusikilizwa ikiwa tu yanakinzana na neno la Mungu. Neno litasimama imara hata kama wanasiasa wote watalipinga hata kama ulimwengu wote utalikataa. Alichosema Yesu kitabaki pale pale, neno lake halibadiliki kamwe. Yeye mwenyewe amesema, “Mimi ni Mungu, Sina kigeugeu”

Jehanamu ilikuja kama dharura, katika uumbaji hatusikii Mungu akiumba Jehanamu. Mwandishi wa kitabu cha Mwanzo, Musa haoneshi kama hapo mwanzo jehanamu iliumbwa. Mungu hakuumba watu au Malaika ili awaangamize, wote aliwaumba kwa utukufu wake. Lusifa alipokosa ndipo Jehanamu ilipoundwa kwa ajili yake na si kwa ajili ya wanadamu.  Jehanamu ni kwa ajili ya shetani ambaye ni muasi, wanadamu wakienda huko wanakwenda mahali ambapo si pao.

Yesu alisema, “Nakwenda kuwaandalia makao”. Makao ya wandamu ni mbinguni mahali alipo Yesu. Ukiangalia mateso yaliyoko Jehanamu utagundua si eneo ambalo Mungu anataka watu wake waende. Kumbuka alipoweka bustani nzuri ya Eden, ikiwa na mito, miti mizuri, ndege, samaki na wanyama wazuri ndipo alipowaweka Adamu na Eva. Je, alipoweka moto mkali, sehemu yenye kiu kali, sehemu ya mateso na dhiki kuu alimkusudia nani? Bila shaka alimkusudia shetani na malaika zake. Ufunuo 20:10 “Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.

Watu wengi hawaamini katika uwepo wa moto wa milele na kama wangeliamini basi wangelibadilika. Lakini ukweli ni kwamba, moto wa milele upo. Watu wataungua usiku na mchana, watu watalia na kusaga meno. Wataona kiu bila ya kupewa maji, wataishi motoni milele, yaani bila mwisho. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. Ufunuo 20:15

Siku moja nikiwa ofisini dada mmoja alinieleza kwamba, anampenda Mungu lakini hawezi kuacha dhambi. Kwa kuwa napenda kuhubiri nikaamua kurefusha maongezi huku nikimweleza jinsi jehanamu palivyokuwa pabaya. Ni kweli pasipo neema ya Kristo na msalaba wake hatuwezi shinda dhambi, lakini ni lazima tujue sana kuhusu matokeo ya kudumu ya dhambi (eternal repercussions).

Nilimweleza kwa hekima, Ok! Unaona ugumu kuacha dhambi vipi umejiandaaje kuikabili jehanamu ya moto. Kila tunapotenda dhambi kwa lugha nyingine tunasema, tuko tayari kwa jehanamu, tuko tayari kwa jehanamu ya moto. Binafsi ninaogopa ni heri nitubu na kugeuka.

KInachowafanya watu wapende jehanamu na kumkataa Mungu ni uhuru. Wanataka wafanye kile miili yao inapenda, wavae kili miili yao inajisikia, waishi wanavyotaka, na waseme wawezavyo. Hawataki kujitia chini ya mamlaka ya Mungu na Kristo wake.

Waefeso 5:5 “Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.” Hawafanyi kwa bahati mbaya, Biblia inasema wanajua. Uhuru wowote unaoturuhusu kulidharau neno la Mungu ni utumwa. Sheria za nchi zinazopingana na neno la uzima ni pingu ya milele kwa raia wa nchi husika. Chagua moja leo mbinguni au Jehanamu? 

Tubu ufalme umekufikia leo. Kama uko tayari kugeuka sema pamoja na mimi: “Bwana Yesu wewe ni mwenye haki na mimi ni mdhambi. Unirehemu Bwana na uyafute makosa yangu yote. Uniumbie na moyo safi kwa maana, sina moyo safi. Nipe na Roho wako Bwana aniongoze tena. Amina”

0 comments :

Swali lililowapoteza wengi

5:28:00 PM Unknown 0 Comments

 
SWALI LILILOWAPOTEZA WENGI
(Nitakula nini, Nitavaa nini)
Kujiuliza kwamba, utakula nini na utavaa nini ni swali ambalo limewapoteza wengi, wengi kwa kujiuliza swali hilo wameachana na wito wao. Wengine wamepoteza wito wao kwa kujiuliza kuhusu wazazi wao na jamaa zao, watakula nini na watavaa nini.
Naamini wazi ni kwa sababu hiyo Yesu alitutaka tusijiulize swali hilo. Aliwataka wanao mwamini waachane na swali hilo. Alitumia mfano wa maua ya kondeni na ndege wa angani ambao hawapandi wala hawavuni lakini wanaishi, alisema sisi ni bora zaidi mbele zake kuliko ndege wa angani. Akawaambia wanafunzi wake, Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie maisha yenu, mtakula nini; wala miili yenu, mtavaa nini.” Luka 12:22
Yesu anasema hatuwezi kutumikia mabwana wawili, hatuwezi kutumikia Mungu na mali. Unapoitwa ni lazima uchague kimoja. Wengi wanapoitwa katika uinjilishaji wanakataa kwa sababu biashara zao zitakufa. Wengi wanaoitwa katika wito wa ukombozi wa nchi zao au wa roho za watu wanakataa kwa kuwa jambo hilo litaumiza wanaowategemea kwa chakula na mavazi.
Rai yangu kwako leo ni kwamba, unaposikia kuitwa na Mungu kufanya kazi fulani usijiulize swali ambalo Yesu ametukataza. Wengi wamejikuta wanaogopa kupigania haki kwa sababu tu itaathiri kipato chao au chakula chao. Wito wako ndio kitambulisho chako, kukataa wito ni kujikataa. Wengi wanajulikana kwa majina ya wito wao: mwalimu, mwinjilisti, mchungaji, kiongozi, waimbaji, wasanii na wabunifu.
Wito unaleta faida kwa watu wengi zaidi kuliko sisi na familia zetu, mamilioni ya wana wa Israeli walitegemea utii wa Musa, Mamilioni ya watu wa Afrika kusini walitegemea utii wa hayati mzee Nelson Madiba Mandela.Tunapoishi kwa ajili ya Mungu tunaishi kwa ajili ya watu wengi ambao kwa hakika hata si ndugu zetu wa damu.  Pastor Chris Oyakhilome anasema, “It is the spiritual family that means so much to God, It is not for your biological family” yaani, “Ni familia yako ya kiroho ndiyo yenye mashiko zaidi mbele za Mungu, wala si kwa ajili ya ndugu zako wa damu”
Ingawaje kwa asili Musa alikuwa Mwebrania lakini kimwili alikuwa ni mwana wa binti Farao, alijulikana kama mtu anayetokea katika familia ya kitajiri. Angeliweza kukubali kuishi kwa ajili ya familia ya Farao. Lakini familia ya kiroho ya Musa ilihusisha watumwa, watu wasio na kitu, watu wanaoteswa utumwani. Musa aliitwa kwa ajili ya watu wasio na kwao, uwe na hakika wito wako utakuletea familia na utapaswa kuteseka kwa ajili ya familia hiyo.
Bwana anapokuita na kukutuma kwa ajili ya jambo fulani uwe na hakika hatakupungukia kwa chochote. Alipowaita na kuwatuma mitume wake hawakuwa na kitu lakini pamoja na hayo hawakupungukiwa na kitu. Usijiulize kuhusu nguo na mavazi ya ndugu zako, usijiulize kuhusu chakula chakula chako, mara zote walioitwa walilazimika kuacha mifugo yao (kondoo), wengine biashara zao(uvuvi) na ndugu zao (wazazi).Katika hawa wanafunzi wote pamoja na kuacha kila kitu bado hawakupungukiwa chochote, na Yesu anawauliza mitume wake swali la kuwajenga: “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!” Luka 22:35
Wanafunzi walijibu, ”lah!” wakiwa na maana kwamba hawakupungukiwa na kitu. Katika maisha yetu tumemwona Bwana na sasa tunakika naye hata jangwani tunajua hatutakosa maji, hata usiku tunajua hatutaogopa, hata hatarini tunahakika tutatoka salama. Kuna maneno mawili tu ndiyo twaweza kumjibu BWANA pale tunaposikia kuitwa, nayo ni, “ndiyo BWANA.”

0 comments :

Kwa kila ambaye....... II

10:11:00 AM Unknown 0 Comments

KWA KILA AMBAYE HAJAOA AU KUOLEWA - II
(Amua kuwa na familia ya aina hii)
Tunapoandika kwa kila ambaye hajaoa na kuolewa sisi pia ni wahusika. Tunapokufundisha tunajifunza pia, na nyakati nyingine tunayasema yale ambayo BWANA ametupa sirini ili kutusaidia. Mengine ni uzoefu wetu unaotokana na miongo kadhaa ambayo Bwana ametukirimia hapa Duniani, yamkini pia ni mafunzo kutoka katika  kukosea kwetu au kutoka kwa  wale ambao tumepata nafasi ya kuwafuatilia. Msanii mmoja anasema, “wasio na watoto ndiyo wanajua kulea vizuri” anamaanisha ndio wanazungumza sana wakidhani ni rahisi wasijue kinachowapata wazazi katika kulea na kukuza watoto. Katika makala hii ninaandika nikiwa na tahadhari hiyo kichwani.

Ili kuepuka majuto na sintofahamu kila ambaye hajaoa na kuolewa azingatie mambo yafuatayo:

Mungu ndiye atoe jawabu: Hili ni gumu ila ni la kweli na hivyo hatuna budi kulisema. Maandiko yanaonesha wazi wazi, “BWANA ndiye akataye nena” pengine imenenwa, ‘’jawabu la ulimi latoka kwake” yote yakimaanisha kwamba, BWANA MUNGU ndiye mwenye maamuzi ya mwisho na ndiye mwenye sauti ya mwisho. Yesu alipotaka kuepuka kikombe cha mateso aliomba, alitaka iwe ni mapenzi ya Mungu kukiepuka na hata alipokipokea bado ilikuwa ni mapenzi ya Mungu. Mwenye hekima mmoja anasema, “You cannot say, ‘Your will’ without saying ‘not my will’” Ni kweli hatuwezi kusema tumemwachia Mungu aamue ilhali sisi wenyewe bado tumeshikilia msimamo wetu. Kinachonifanya nimwombe Mungu si tu ni kwa sababu nampenda bali ni kwa sababu sijimiliki, Yeye ni muumba wangu na mimi ni mali yake. Yeye ni mfinyanzi na mimi ni chombo chake. Si urembo, urefu na utanishati ndio uwe kivutio chetu, la hasha! Chaguo la Mungu ndiyo chaguo letu. Epuka kumnyima Mungu kuwa mwamuzi wako katika jambo la msingi namna hii. Derek Prince anakiri kila ilipokuja suala la kuoa mara zote (mbili kufuatia kifo cha mke wa kwanza) alimtegemea Mungu pasipo kuweka ujuzi wake. Nimefuatilia hekima ya wengi waliotutangulia, akiwamo Sunday Adelaja, Billy Graham na Derek Prince kwa ujumla wanashauri watu waoe chaguo la Mungu. Waachane na watu waliowachora kichwani (chaguo la fikra) badala yake wapokee zawadi toka kwa Bwana.

Jizatiti katika Viwango vya kimungu (Committed to God’s standard): Ndoa ni ya kimungu, ni wazo lililotoka moyoni mwa Mungu wala si akilini mwa Adamu. Ziko ndoa za kihindi, za kiafrika, za mkeka, za serikali na nyingine nyingi. Lakini ndoa hizi kama hazikuwekwa katika viwango vya kimungu ambavyo ni vya kibiblia si tu kwamba huwa hazina mashiko bali huwa hazikamilishi kazi. Kusudi la ndoa ni kazi, anayetoa kazi hiyo ni Mungu. Ndiye anajuaye wanaofaa kwa ufanisi bora wa jukumu hilo. Viwango vya kimungu ni pamoja na kuwa na mke mmoja tu (msaidizi na si wasaidizi), kuwa na watoto waadilifu, kukamilishana, kuwa na usafi na utakatifu. Mungu hakutaka kuleta Dunia ya watu bilioni saba kwa siku moja bali alitaka kwa kupitia familia moja (ya Adamu na Eva) wapatikane watu wote zaidi ya bilioni saba. Nadhani nia kubwa ni kupata ubora ule ule wa utakatifu, uchaji na uadilifu. Rafiki yangu aliandika: “Quality is never an accident, it is planned”

Achana na ndoto: Kuna rafiki zangu wa kike ambao walikuwa na ndoto na maono kwamba, tutaoana na sasa hivi wameshaolewa na watu wengine kabisa; tena kwa ndoa takatifu, na mimi naziheshimu. Kuna wengine nilipata maono na wao wakapata njozi lakini sasa wako na watu wengine na mimi nawaita shemeji. Ndoto ni hatari! Ndoto ni njia isiyoaminika. Zamani nabii akiota ndoto na kuisema au akitabiri na isitimie basi aliuawa. Kama ndoto za ndoa zingekuwa hivyo basi wengi wangepigwa na kuchinjwa kama manabii wa uongo mfano wa manabii wa baali walivyochinjwa na Eliya. Naamini ukikaa katika neno la Mungu utakuwa salama, achana na ndoto. Ndoto zinapoteza wengi kuliko wanaonufaika. Ndoto za injili na kazi hazina shida lakini za harusi na ndoa zinamatatizo, si kigezo halali cha kumkubali mtu.

Omba bila kukoma: Wanaosema hili si la kuombea hawana tofauti na wanaosema hakuna Mungu. Binafsi najua Mungu atanijibu na kunipa haja ya ninachostahili katika Kristo. Si tu kwamba najua atanijibu, bali ninajua tena kwa hakika. Omba kwa bidii kiasi kwamba hata Mungu akijibu usiweze kujua amekujibu maombi uliyaomba lini bali uwe unajua tu, amekujibu. Nampenda Hudson Taylor mmisionari mwenye alama anasema, “kila alichonacho ni matokeo ya maombi”. Hata mshahara wake ulipochelewa hakuthubutu kumwambia kiongozi wake, bali aliingia kwenye maombi alitaka mshahara wake uwe ni jibu liliotokana na maombi. Ni furaha namna gani kuwa na familia ambayo baba, mama na watoto wote ni matokea ya maombi? Nimeshuhudia watoto katika nyumba ya dada yangu ambao  ni matokeo ya maombi, na ni furaha kuona matunda ya maombi katika ulimwengu wa nyama. Pray, pray, pray

Tukutane wiki ijayo, usikose makala yako. Shallom…

0 comments :