Katika nchi hii, ni nani jasiri kama mimi?

11:52:00 AM Unknown 0 Comments

 
KATIKA NCHI HII NI NANI JASIRI KAMA MIMI?
(Neno Lake ndio ujasiri wetu)
Kichwa cha makala hii ni nukuu ya  maneno ya mwanasiasa aliyekuwa na haiba ya aina yake hapa Nchini Tanzania hayati Mchungaji Mtikila. Katika moja ya mazungumzo yake alihoji, “katika taifa hili ni nani mtu jasiri kama mimi?” Tunahitaji watu wenye ujasiri kama wa Mchungaji Mtikila lakini msingi wa ujasiri wao na uwe ni neno la Mungu. Tunahitaji watu wenye uhakika na maisha  yao (life is predictable) na msingi wao uwe ni ukweli wa neno la Mungu.
Wasiwasi ni yale mawazo yanayompata mtu anaposahau neno la Mungu. Kwa nini leo watu wengi wanahuzuni? Kwa nini leo watu wengi wamekata tamaa?  Kwa nini leo watu hawapati usingizi? Kwa nini leo wengi wanahofu na kesho yao? Ni kwa sababu wamesahau Yesu alivyosema.
Mwenye hekima mmoja anasema, hekima ni uwezo wa kulitumia neno la Mungu katika hali na maeneo tofauti tofauti. Tutalitumiaje neno ambalo tumelisahau? Tutalitumiaje neno ambalo hatulijui? Mpaka tumejua namna ya kulitumia neno la Mungu katika uchumi, katika kuachwa, katika dhiki, katika kushinda, katika kazi, katika masomo na biashara ndipo tunaweza kujiita wenye hekima.
Nyakati nyingine katika shida na mateso neno pekee ambalo Mungu aliwatumia watu wake ni kwamba, yuko pamoja nao. Ile tu kujua kwamba katika shida yako uko pamoja na BWANA inakutia nguvu. Siku moja nafsi yangu ilikuwa imeugua na nilikuwa najua sijatenda vema mbele za Bwana. Katika hali ya kukata tamaa ndipo nilipoona maono kwamba, Mungu yuko pamoja nami pamoja na mapangufu yangu, na nikajawa na furaha sana. Utajiri wa Mungu si tu wa fedha na Dhahabu bali ni pamoja na utajiri wa rehema, neema, msamaha, upendo na amani.  Wanaoujua utajiri wa Mungu wanajisamehe na kuwasamehe wengine haraka.
Je, Unamashaka kwa sababu umekaa kitambo kirefu bila mchumba? Je, bado haujapata kazi na unatafuta? Kumbuka alivyosema, Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. ” Mhubiri 3:1
Je, unaogopa itakuwaje? Kumbuka neno, Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai. ” Zaburi 27:13
Mitume wa Yesu walifika kaburini na kushangaa kuona BWANA hayumo kaburini waliogopa na kudhani mwili wake umeibwa. Na malaika wawili walijua mitume hawa wanamaradhi na tiba yake ni kuwakumbusha neno la Kristo mwenyewe na hapa Malaika akawaambia: “Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya” Luka 24:6
Wasingeliambiwa kumbukeni kama wangelikuwa wanakumbuka. Pamoja na Yesu kusema sana habari za ufufuko wake mitume walisahau. Ndio maana ni Muhimu kusoma neno la Mungu mara kwa mara, kusahau kupo!  Kukumbuka alichosema BWANA wetu Yesu ni ufunguo wa upatikanaji wa mahitaji yetu. Kumbukeni alivyosema, andikeni malengo yenu na maombi yafanyike, yapelekwe mbele zake BWANA. Usisahau kumpa utukufu MUNGU wetu  atakapo kujibu nina hakika atajibu tu.
Tukutane kileleni mahali wanapopatikana washindi.


0 comments :