Napendekeza usikope IV
NAPENDEKEZA USIKOPE
(Makala ya Nne)
Wiki
hii ninamalizia kwa kutaja kanuni nyingine zenye uwezo wa kutupatia uhuru wa
kifedha ikiwa tutaziangalia na kuzitenda. Waswahili wanasema “huwezi kuvuka mto
kwa kuuangalia” kwa hiyo ili upate matokeo bora ni lazima uzifanyie kazi kanuni
hizi. Lazima uzitende kwa bidii vinginevyo hauwezi kupata matokeo tarajiwa. Ili
kutoka katika hali ya mikopo fanya yafuatayo:
- Weka akiba: Wawekezaji wengi wanasifa ya kutumia kidogo na kuweka akiba kubwa. Hatuwezi kuweka akiba kama tunatumia kila tulichokizalisha au tunakula kila tunacholipwa. Warren Buffet tajiri mkubwa duniani anatoa kanuni mbili za kukusaidia kukuza uchumi wako anaitaja ya kwanza ni, “usipoteze pesa na ya pili inasema, usisahau kanauni ya kwanza, usipoteze pesa.” Katika kila ngazi ya mshahara wako, haijalishi ni kubwa au ndogo hakikisha unaweka akiba. Pasipo akiba huwezi kuwekeza. Ukilipwa laki tano weka akiba, ukilipwa milioni tano weka akiba. Usipoweka akiba katika ngazi ndogo ya mshahara hautaweza hata utakapo kuwa na ngazi kubwa. Akiba ni uamuzi ambao msingi wake ni nidhamu. Mataifa yenye akiba kubwa (35%) ni yale yenye nidhamu katika pesa. Kama ambavyo benki hukata pesa yao ya mkopo moja kwa moja ndivyo ambavyo mtu anapaswa kujifunza kuweka akiba moja kwa moja. Serikali hukata kodi yake (PAYE) bila majadiliano, mtu hupokea mshahara ambao tayari umeshakatwa kiasi cha kodi ya serikali na hivyo mtu haoni maumivu kwa kuwa hajizipeleka kwa mkono wake katika taasisi ya kodi. Vivyo hivyo unapaswa kuhakikisha akiba yako haiguswi bali inaingia moja kwa moja katika akaunti yako ya akiba au ile ya malengo.
- Jilipe kwanza; Mshahara wako ni ile hela unayobaki nayo baada ya kutoa matumizi yako yote ya mwezi. Kama ukitoa matumizi yako yote ya mwezi hubakiwi na kitu basi ujue huna mshahara bali una posho. UKigundua huna mshahara anza kufikiri namna ya kupata mshahara. Hela unayopeleka dukani na shuleni kulipa ada ni mshahara kwa hao unaowapelekea na si yako. Hakikisha unajilipa kwanza na kama hamna hakikisha unaishi kwa namna ambavyo unapata kipato cha ziada. Pesa inayokwenda katika chakula, maji, ada na mavazi ni pesa ya kujikimu na hii haitoi jibu la uhuru wa kifedha. Uhuru wa kifedha unaletwa na pesa inakwenda kwenye miradi. Kama hautuweki akiba na kujipanga kuwekeza maana yake tunaishi ili kujikimu tu.
- Wekeza katika mali zisizo hamishika: Ukifanikiwa kuwa na akiba kubwa wekeza katika mali zisizo hamishika. Unaweza kumiliki mali isiyohamishika kama kiwanja kwa kuamuru (issue standing instruction) kampuni au taasisi inayohusika na utoaji viwanja kukata sehemu ndogo ya mshahara wako kila mwezi mpaka itakapotosha kununua kiwanja. Kwa mazingira ya sasa na mishahara ya kitanzania si rahisi kununua kiwanja kwa kulipia mara moja lakini kwa njia hii ninayopendekeza ni rahisi kabisa. Inawezekana kabisa mpaka muda ambao unamaliza kulipia kiwanja hicho tayari kikawa na thamani kubwa kuliko jumla ya makato yako yote. Mali zisizo hamishika ndizo humtambulisha sana mtu mwenye utajiri. Hakikisha utajiri wako unajumuisha pia mali zisizo hamishika kama vile; viwanja, mashamba, nyumba na miti. Ukiwekeza katika ardhi leo, ambapo huenda unazaidi ya miaka ishirini kuelekea kustaafu inawezekana ardhi yako ikakupatia karibu robo tatu ya pesa ambayo utalipwa wakati wa kustaafu (miaka 60).
- Jifunge kwa kujiwekea masharti: Mkopo usio na masharti ni mkopo mbaya. Kama benki hawajakupa masharti hakikisha wewe binafsi unajiwekea. Mikopo mikubwa huhitaji mchanganuo wa biashara ambao kwa kiasi fulani unasaidia katika kuleta matokeo chanya ya matumizi ya pesa. Mikopo binafsi ambayo watu wa kati wanachukua ni hatari kwa kuwa haihitaji hata mtu aeleze anapeleka wapi. Unaweza kuzitumia katika sherehe ya ndoa, katika kununulia vinywaji au chochote unachotaka.
Nakushukuru
kwa kusoma makala hii. Naaomba kuhitimisha na ninapendekeza usikope kwa vigezo
nilivyovitaja katika makala zote nne. Na ukiweza kukopa basi hakikisha
unavigezo nilivovitaja katika makala zote nne. Mpaka wiki ijayo, Shalomu!!!
0 comments :