Kwa Msaada wa Bwana Mungu Tumeweza

9:49:00 AM Unknown 1 Comments

KWA MSAADA WA BWANA MUNGU TUMEWEZA
(Aksante Bwana Yesu) 

Kuna nyakati ambazo unajikuta njia panda na mbele ya macho yako njia zote zinaonekana ni njema au ni sawasawa tu. Na hapo unamuhitaji rafiki atakaye kugusa begani na kukwambia, “tafadhali, tupite upande huu” bila shaka upande atakao uchagua rafiki huyo ni upande salama. Kuna nyakati ambazo unajiona una mabaya mengi na hapo unamhitaji rafiki atakayekwambia, unamazuri mengi pia.

Hayati Dkt William Arthur anasema: “Mungu amekupa zawadi ya sekunde 86,400 leo, Je,umetumia hata moja kumshukuru?”. Kwa zaidi ya wiki hamsini na mbili (52) takribani mwaka mmoja sasa, Mungu ametupa neema ya kukujia kila siku ya Ijumaa kwa njia ya makala zetu. Tumekujia kama marafiki tukikwambia, “tafadhali, tupite upande huu ambao ni salama”. Leo tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu. Kama si Yeye tusingeliweza kabisa kukufikia kwa mwaka Mzima. Utukufu na heshima vimrudie Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo na Yesu Kristo aliyetumwa. Amina

Siku moja nilikuwa katika tamasha moja la kusimumua. Na mahali pale watu walikuwa wakielezea mafanikio yao na kuwatia moyo wengine. Lakini kuna jambo moja lilikuwa likisumbua kichwa changu siku ile nalo ni hili, katika maelezo ya kufanikiwa kwao sikusikia wakimtaja Mungu. Na mimi nikajiuliza: Ni kweli Mungu hakuwasaidia hawa? Je, mitaa yao haipati mvua kutoka juu? Je! Si Mungu aliyewapa afya njema hawa? Si Mungu aliyewavusha hawa? I was like where is my God in their speeches?

Hatumtaji Mungu katika maelezo yetu kama utaratibu au mtindo fulani tu (formality.) La hasha! Tunamtaja kwa sababu Mungu anaishi na tumeona akitusaidia. Kwetu sisi Mungu ni halisi zaidi (japo kwa macho ya nyama hatumwoni) kuliko tuwaonao na tuyaonayo kwa macho ya nyama.  Yuko karibu nasi kuliko nguo tuvaazo.  Yeye ni Mungu ndani yetu. Kama tumefanya vema basi amefanya, maana yu ndani yetu.

Nilipoanza kazi kwa mara ya kwanza nikiwa na maarifa ya darasani tu bila ya kujua kilichopo kazini nilipata funzo kubwa. Mhasibu wa ofisi ile aliacha kazi na Mhasibu pekee niliyebakia ni mimi na nilihitajika kufunga hesabu na kupeleka kwa bodi. Mara nyingi hesabu zilinisumbua hazikuwa sawasawa kwa lugha ya kihasibu, ‘not balanced or not tallies’ Mara nyingi hali hiyo ilipotokea nilifanya jambo ambalo halifundishwi shuleni wala chuoni. Mara kadhaa ilipotokea nilikuwa nikiinama chini au nikifumba macho yangu na kuomba kwa BWANA. Nilimtaka Roho Mtakatifu anisaidie kama mfanyakazi mwenzangu (co-worker) ni ajabu aliniitikia na kunisaidia kujua chanzo cha tofauti ya hesabu zangu. Kwangu mimi Mungu ni halisi hata katika mambo ya Uhasibu. Bila shaka ndio maana Daudi akasema hivi: “Haleluya. Nampenda Bwana kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote.”Zab 116:1-2

Tunapomshukuru Mungu tunaibadili siku ya kawaida kuwa siku kuu. Tunamposhukuru Mungu leo hatufanyi mila ya wazungu, tunapomshukuru leo hatutimizi ratiba bali tumemwona, tunamtambua na tunampenda Mungu wetu. Hakika Yesu yupo ametusaidia nasi tunamshukuru. Ee Mungu wewe uko umetusaidia nasi Ee Bwana tunakushukuru. Waliokombolewa na Bwana na waliomwona BWANA katika makala hizi 53 waseme. Amina.

Kama namna ya kumshukuru Mungu pamoja nasi waunganishe rafiki zako angalau watano kwa kututumia anuani ya barua pepe zao (email) ili nao pia wafikiwe na neno la Mungu. Pia unaweza kujiunga (kusubscribe) kwa kupitia kwenye blog yetu kwa kuandika email yako na kutuma, utakuwa ukipokea article zetu kila ijumaa. Usisahau kuichagua page yetu ya facebook pia kama njia moja wapo ya kukufikia. Leo tunategemea kupokea  anuani tano za marafiki zako unaowapenda na ungependa wapate makala hizi. Tafadhali tutumie tunasubiri.  Mungu akupe kukaa salama.

1 comment :

  1. We should praise Him (Jesus) everytime we have, He made it happen.
    ThankyouJesus#

    ReplyDelete