Yesu Kazini

11:56:00 AM Unknown 0 Comments

YESU KAZINI
(Jesus in Action)
Miungu ya watu wengine ina miguu lakini haiendi, inamacho wala haioni, inamikono wala haishiki. Miungu hiyo [sanamu] imeumbwa na wale wanaoiabudu [wametengeza mungu wao]. Miungu hiyo ni pesa! Wako wanaozitumikia na kuziabudu. Miungu hiyo ni ng’ombe, tamaduni, mila au desturi zinazopingana na Mungu wa kweli. Miungu hiyo ni kitu chochote cha kufinyangwa, kuchongwa au kutengenezwa kinachochukua nafasi ya Mungu. Chochote kinachochukua nafasi ya Mungu katika moyo wa mwandamu ni sanamu.
Tukitegemea uwezo wetu kuliko Mungu uwezo huo unageuka sanamu. Tukitegemea uzoefu kuliko Mungu uzoefu huo unageuka sanamu. Tunapomfanya Mungu kuwa wa pili tunaingia katika mtego wa kuabudu sanamu. Tunaposema tujenge nyumba zetu kwanza ndipo tujenge nyumba ya Mungu tunaingia mtegoni kama watu wa nyakati za Hagai. God second! Selfish Priority.
Katika hekalu kulikuwapo na patakatifu pa patakatifu ambako kulikuwepo na kiti cha rehema mahali alipoketi Mungu wa rehema. Miili yetu pia ni mahekalu, iko sehemu ambayo ni maalamu kwa ajili ya Mungu wetu. Kama ilivyokuwa katika kiti cha rehema, leo Mungu anakaa katika mioyo yetu na hapo amestahili yeye tu, kutukuzwa na kuabudiwa. Mungu ni wa kwanza katika moyo wa mwandamu. Akikaa mwingine hapo huitwa sanamu, na akitambulika na kuheshimiwa huitwa ibada ya sanamu.
Yohana mbatizaji alitaka kujua kwamba, Yesu ndiye Kristo au vinginevyo. Yesu akitaka kumdhihirishia Yohana kuwa Kristo ni matendo alimjibu, “Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema” Kwa lugha nyingine ukisikia matendo haya ujue Yesu Kristo yuko kazini. Matendo haya yalitosha kumpa picha Yohana.
Mungu wetu anaonekana katika matendo mema, Mungu wetu anatembea katika maisha ya watu wake. Mungu wetu anawagusa vipofu, viwete, wenye ukoma [wenye dhambi], viziwi hata masikini pia. Tofauti na sanamu hazimgusi mtu, ni kazi ya mikono ya watu wala haziwezi kumstawisha mtu yeyote. Zinamikono wala hazishiki, zinamiguu wala hazitembei labda waliozifanya wazitembeze.
Tunaposikia uzima, amani, mafanikio na ustawi wa jamii zetu bila shaka tunatambua Yesu Kristo yuko kazini. Yesu ni matendo, Yesu ni upendo tena Yesu ni miujiza. “Nao walipofika kwake, walisema, Yohana Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona.  Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami. ” Luka 7:20-23
Wasiochukizwa na Yesu Kristo waseme na wabarikiwe. Mpaka wiki ijayo, amani iwe nawe.

0 comments :