Napendekeza Usikope - II

1:53:00 PM Unknown 0 Comments

 
NAPENDEKEZA USIKOPE
(Makala ya Pili)

Katika toleo liliopita niliahidi kuendelea kujenga hoja yangu katika toleo hili. Hoja iliyomezani ni pendekezo langu kwamba, usikope. Mikopo inapaswa kutumika tu kama daraja la kuelekea kutokukopa (debt is a means to a debt free life)
Nimefanya utafiti kwa kusoma vitabu kadhaa vya kifedha kikiwepo, Money Master The Game cha Anthony Robins, The Richest man In Babylon cha George S Clason na vingine vingi. Katika vitabu hivyo mikopo haitajwi kama siri ya utajiri. Kwa mtazamo wangu, mkopo ni dharura sasa ni hatari kama kila siku itakuwa ni dharura. Yes! It’s dangerous if every day is an emergency day. Kanuni ya kumkimbiza mwizi inatudai tufunge mlango kwanza ndipo tumkimbize, vinginevyo unaweza ibiwa mara mbili. Hapa ni vema tufunge mlango ndipo tupambane na umasikini.
Mkopo unatoa ishara zifuatavyo:
1.      Ni dalili ya kupungukiwa. Tunawezaje kusema tumebarikiwa ikiwa tunamadeni? Hudson Taylor ni mmisionari aliyekataa kukopa anaeleza kwamba, tukikopa kwa lugha nyingine tunatamka kuwa Mungu ameshindwa kukutana na mahitaji yetu ndio maana tumeamua kukopa ili kujisaidia wenyewe. Maandiko yanasema, “Kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.” Waebrania 13:5c
2.     Ni kinyume cha baraka, Neno la Mungu halichagizi kukopa. Moja ya Baraka kwa warithi wa Ibrahimu ni uhuru wa kifedha, si baraka kuu lakini ni moja ya baraka. Unaweza kukubali au kukataa kuwa sehemu ya ahadi hii, hilo ni juu yako ndugu: “nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe” Kumbukumbu 28:12 Si kila tajiri anauhusiano mbaya na Mungu, na si kila masikini ni mcha Mungu. Uhusiano na Mungu unajengwa na namna tunavyovitumia vitu tulivyonavyo na kuwa navyo au kutokuwa navyo si kosa.
3.     Ni kizuizi cha kutoa fungu la kumi, Shetani anaweza kutumia mikopo kuwashawishi watu wasitoe fungu la kumi ambalo ni chanzo kikubwa cha Baraka. Nimewahoji watu kadhaa wenye mkopo mmoja na zaidi ya mmoja na kati yao hakuna hata mmoja anayetoa fungu la kumi la mshahara wake. Sababu mikopo imefanya mshahara wao umekuwa mdogo ukilinganisha na matumizi. Mmoja aliniambia alishasahau kutoa fungu la kumi, anaomba Mungu amsamehe.
4.     Inaua ubunifu, Mtu akishaifanya mikopo kuwa suluhisho la maisha yake hujisahau na hivyo si rahisi kwake kutumia njia sahihi za mafanikio kama vile: kuweka akiba, kuwekeza, na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.Kuna msemo usemao: “Pesa mikononi mwa Muhindi {Indians} hukaa sana kuliko mikononi mwa Mwafrika {Africans}” Usemi huu unaonesha jinsi Waafrika tulivyo na tabia kula pesa kwa haraka, na kuwa na matumizi mengi na hivyo hela haikai mkononi kwa kitambo kirefu, ilhali wengine huzalisha kidogo wapatacho na kukiongeza.
5.     Ni dalili ya utumwa. Biblia inasema wazi “Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye” {Mithali 22:7b} Kuna furaha ambayo hurejea mara mtu anapomaliza kulipa deni au mkopo wake. Ni wazi furaha ile ambayo hurejea siku mtu anapolipa deni ndiyo furaha aliyoipoteza siku alipoingia katika deni. Utumwa wa kimwili na kifikra huanza kwa utumwa wa kifedha. Si rahisi kuyakataa mawazo ya mtu anayekudai, ndio maana nchi masikini hazina sauti, hazisikiki hata zikisema kwa nguvu. Waswahili husema, “dawa ya deni ni kulipa” maana yake, deni ni ugonjwa, deni ni usumbufu na kero na ili tuwe huru lazima tulipe na tusikope tena.
Suluhisho: Wiki ijayo nitataja njia kadhaa za kukusaidia kutoka katika mikopo na kuelekea utajiri. Usikose makala ya wiki ijayo itakayokueleza njia za kukutoa katika mikopo hadi utajiri. Shallomu! Peace and Prosperity upon you


0 comments :

Napendekeza usikope

5:47:00 PM Unknown 0 Comments


 
NAPENDEKEZA USIKOPE
(Makala ya Kwanza) 
Kukopa katika benki (taasisi za fedha) ili kujikomboa kiuchumi ni sawa na kujificha chini ya transifoma ya umeme wakati mvua kali yenye kuambatana na radi ikinyesha. Benki nyingi hazikopi hovyo na zikilazimika kukopa hufanya hivyo ili kuwakopesha wengine. Wanakopa ili kukopesha na kuwekeza. Je, ni watu wangapi ambao wana mikopo benki; walichukua mikopo hiyo ili kukopesha wengine au ili kuwekeza kwa lengo la kupata riba? Mpaka tumejitazama na kuhamia katika nafasi ya benki hatuwezi kupata matokeo mazuri kama benki zipatavyo faida katika mikopo yake. Kwa kweli nalazimika kukumbuka na kujaribu kutafsiri maneno ya mshairi huyu: “Benki ni mahali wanapokupatia mwavuli wakati hali ya hewa ni tulivu na kukutaka urejeshe mara tu mvua itakapo anza kunyesha” Robert Frost
Inawezekana ujumbe wangu ukaleta ukakasi masikioni mwako na ganzi katika meno yako, ndiyo! Sote tumelelewa na kukua huku; nchi, wazazi, walezi pamoja na jamaa zetu wakikopa na hivyo makala hii inakabiliwa na upinzani mzito kutoka katika Historia. Sijui kama unajua, mtoto akizaliwa jela hupaita nyumbani badala ya gerezani. Tuliozaliwa katika mazingira yenye changamoto lazima tufikiri kwa upya namna ya kutoka katika ombwe la mikopo. Namna ya kuvunja kawaida isiyofaa.  Kawaida nzuri au utamaduni mzuri waweza kuwa sheria lakini si busara kuacha kawaida mbaya kuwa kama sheria.
Kuna watu wanakopa kwa sababu hawataki kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Kuna matumizi mengi tunayafanya na hayana tija ndani ya dakika tano zijazo. Ni matumizi ambayo hutupatia furaha wakati tunapoyafanya na baada ya hapo kilio. Mwenye hekima mmoja anasema, “Ikitokea bahati mbaya mchimba shimo akajikuta ndani ya shimo jambo la kwanza analopaswa kufanya ni kuacha kuchimba shimo hilo ili asijichimbie kwenda kina kirefu zaidi”. IKiwa uko katika madeni na mikopo isiyokwisha jambo la kwanza la msingi ni kuamua kuacha kukopa. Ninapendekeza usikope katika benki na taasisi nyingine zenye kutoza riba kubwa.
Mikopo inadumaza akili, inakutaka uwe mteja wa benki kila siku tena haikupi nafasi ya kufikiri kama benki. Badala ya kuwaza  kukopesha watu wengine, milele utakuwa ukiwaza kukopa. Wakati wewe unawaza ukope shilingi ngapi, benki wanawaza wakutoze riba kiasi gani. Umewahi kuwaza kwamba kusingekuwa na mikopo ungeishi vipi? Ni kweli kwamba, hakuna namna nyingine ya  kuishi isipokuwa kwa kukopa tu? Naamini jawabu ni hapana.
Jambo la kwanza kabla ya kufanya uamuzi wa kukopa si kuitazama shida yako bali ni kuangalia masharti ya mkopo husika. Je, unauwezo kiasi gani wa kuyasoma na kuyadadavua masharti ya mkopo? Kesi ya meno hupelekwa kwa daktari wa meno, mambo ya nyota kwa mamajusi iweje mambo yahusuyo pesa yaende bila idhini wala ushauri wa mtaalamu yeyote?  Ni vizuri wataalamu wakupe ushauri kuhusu mkopo wako, na wataalamu hao wawe ni nje ya benki. Kesi ya nyani usimpelekee tumbili.
Kila tunapokopa kwa lugha nyingine tunatangaza kwamba sisi si wabarikiwa. Je, unalijua na hili? Tunapokopa tunamaanisha tumepungukiwa ilhali ahadi inasema hatuta pungukiwa: Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.” Waebrania 13:5
Tafakari halafu Chukua hatua, usikope hovyo. Wiki ijayo nitaendelea kujenga hoja ili tujue ubaya wa mikopo hii ni kulingana na utafiti nilioufanya kwa kuwahoji na kutazama mwenendo wa jamii ya sasa. Hadi wiki ijayo, Shalomu!!!
Kwa maswali au maoni  kuhusu hili tuandikie katika email na blog yetu.

0 comments :

Nuia Kuacha Alama - II

10:18:00 AM Unknown 1 Comments

 
NUIA KUACHA ALAMA - II
(“Nani atalia utakapokufa” Robin Sharma)

Kila mwanadamu anawajibu kwa Mungu na kwa jamii yake. Rafiki yangu hupenda kusema, “Wajibu mkubwa ulionao ni kutambua au kujua kuwa unawajibu” (The greatest responsibility is to know, that you are responsible). Tunapozungumza kuhusu kuacha alama (legacy) hatuzungumzi kuhusu kuacha majengo au vito vya thamani; bali tunazungumza aina na mfumo wa maisha utakaokuwezesha kuishi kwa ufanisi hapa duniani; kugusa maisha ya watu na kuacha alama katika mioyo yao.
Watu wote walioacha alama walijua kwanini wapo duniani katika nyakati zao, walikuwa tayari kutumia uwezo ulikuwa ndani yao ili kuwafaidia watu wengine na kugusa maisha yao; walijua wanawajibika kwa jamii zao na kwa vizazi vitakavyo kuja baada yao. Kazi zao na kujitoa kwao kumerahisisha maisha yetu ya sasa, na kufanya ulimwengu kuwa bora zaidi. Hata mimi na wewe tunaowajibu wetu kila mmoja, swali la kujiuliza je tutautimiza wajibu huo kikamilifu?
Mwandishi wa kitabu cha The leader who had no title, Robin Sharma amewahi kuandika chapisho, “Nani atalia utakapokufa” Hii ikiwa na maana kwamba, je! ni jambo gani litabaki hai kama alama utakapomaliza utumishi wako hapa duniani? [2Tim4:6-8]
Katika jamii ya Wayahudi endapo mtu angekufa na jina lake likasahaulika haraka katika jamii hiyo ilihesabiwa kuwa ni laana. Watu wengi walioacha alama wanaishi zaidi wanapokufu kuliko wanapokuwa hai, umaarufu wa Princes Diana uliongezeka zaidi baada ya kifo chake kuliko alipokuwa hai, vivyo hivyo Yesu Kristo. Tunapaswa kuishi kwa nidhamu ambayo itatupatia maisha hata tutakapokuwa kaburini.
Utakapoondoka duniani unataka watu [jamii yako, familia yako, rafiki zako] waseme wewe ulikuwa mtu wa namna gani? Au ungependa vizazi vijavyo baada ya wewe viseme wewe ulikuwa mtu wa namna gani? Ungependa utambulike kama mtu wa namna gani? Muadilifu? Mfano wa kuigwa kwa vijana? Mkarimu? Mtu aliyetumia uwezo wake kumtukuza Mungu na kuwafaidia wengine? Mtu aliyeishi kwa ufanisi [effective life]?
Utakapoanza kujiuliza maswali haya mara kwa mara; ghafla utapata kutambua na kujua namna ikupasavyo kuishi kulingana na kile unachotaka kisemwe baada ya kuondoka kwako. Kile unachotaka kisemwe kuhusu wewe, Anza kukiishi sasa; usisubiri kesho. Kumbuka, usiniambie unachoweza kufanya; nioneshe.
Kile tulichokifanya kwa ajili yetu tu, hufa na kuzikwa pamoja nasi kaburini; lakini kile tulichokifanya kwa ajili ya wengine na kwa ulimwengu, huendelea kuwepo hata wakati sisi hatupo”-Albert Pike, (Tafasiri ya mwandishi)


1 comments :

Nuia Kuacha Alama

6:53:00 PM Unknown 0 Comments

 
NUIA KUACHA ALAMA
(Tumia uwezo ulio ndani yako) 
Mwandishi wa vitabu na kiongozi maarufu Dr. Myles Munroe, amewai kuandika, “The greatest tragedy in your life will not be your death but what dies with you at death. What a shame to waste what God gave you to use” yaani Jambo baya kabisa katika maisha yako halitakuwa kifo chako, bali ni kifo cha kile ulichokufa nacho. Ni fedheha kiasi gani kufa bila kutumia uwezo uliopewa na Mungu ili uutumie (Tafasiri isiyo rasmi).
Mara nyigi mtu anapofikiri juu ya kifo chake, ghafla anapata hekima na nidhamu juu ya aina na mfumo wa maisha anaoishi sasa; na kuanza kuishi kwa kuzingatia vipaumbele muhimu katika maisha yake. Watu wote walioacha alama (legacy) duniani, walifikiri juu ya vifo vyao kwanza; walijua wao si wa kudumu hapa duniani; na kuna siku hawatakuwepo, hivyo walifanya bidii kuishi na kutumia uwezo [potentials] waliokuwa nao kwa namna iliyowapasa ili muda wao utakapoisha wasiwe watu wa kujuta.
“Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima” Zaburi 90:12
Ili kuacha alama inatupasa kuishi kwa ufanisi kwanza, kutumia kile tulijaliwa na Mungu kwa ajili ya sifa na utukufu wake na kwa kuwafaidia wengine. Hapa nataka nikushirikishe hatua tatu muhimu zitakazokusaidia;
Hatua ya kwanza, ni kutambua uwezo ulionao. Kila mtu anao uwezo ndani yake, hakuna mtu alikuja duniani bila kupewa uwezo fulani utakaompa Mungu utukufu na kuwafaidia watu wengine. Inaweza kuwa ni kuongea, kuandika, michezo (athletes), kuimba, ‘uwezo wa biashara’, kusimamia na kuongoza, Mawazo ya kuanzisha kampuni, kufundisha, kuhubiri, kupika, kufurahisha wengine  n.k
Hatua ya pili, ni kuufanya uwezo huo kuwa bora kila siku (Improve) ili makusudi utakapokuwa unautumia, uwe katika kiwango cha ubora na ufanisi zaidi. Kama ni kazi au huduma unafanya leo, uifanye katika ubora kuliko ulivyofanya jana. Nuia kufanya kitu bora kila siku kuliko ulivyofanya jana. Hii itakulazimu kujifunza na kupata maarifa zaidi ili kuboresha uwezo huo.

Mfano. Unaweza kuwa na uwezo wa kuimba lakini haujui kuimba, yaani hauna maarifa ya kukusaidia kuimba katika ubora. Mwenyehekima mmoja amewahi kusema, “Watu hawavutwi na uwezo ulionao, bali wanavutwa na ujuzi ulionao”.

Kuwa na uwezo tu haitoshi, unahitaji maarifa yatakayo kusaidia kutumia uwezo huo. Ujuzi ni tofauti na uwezo hauji kwa kuwekewa mikono, unakuja kwa kujifunza[1Tim4:13, 14], yaani kama wewe haujajifunza sheria; utawekewa mikono na Mwanasheria mkuu wa serikali mpaka upate upara, na bado utatoka haujui
Hatua ya tatu, usisubiri uwe kila kitu ili ufanye kitu; usipate shida kuanza na biashara ndogo, ikiwa ndani yako unaona kampuni. Biblia inasisitiza kuwa, mtu asidharau mwanzo mdogo [Zekaria 4:10, NKJV]. Mwal. Christopher Mwakasege amewahi kushuhudia kwamba alianza kuhubiria watu wanne, leo hii anahudumia maelfu; Mwandishi wa kitabu cha The Leader who had no title, Robin Sharma anasema katika mkutano wake wa kwanza ukumbi mzima ulikuwa na watu wapatao ishirini na wanne, kati ya hao ishirini na mmoja ni ndugu zake.
Mama Teresa wa Calcutta hakuwa na fedha alipoanza kuwasaidia masikini kule India; alijua kamwe hawezi kuwafikia masikini wote na kuwapatia huduma muhimu; hii haikumkatisha tamaa, alianza na mmoja. Kumbuka jambo hili: Usiniambie unachoweza kufanya, nioneshe.

0 comments :

Usiogope; Yesu Yu Hai

11:40:00 AM Unknown 0 Comments


USIOGOPE, YESU YU HAI
(Sasa ni Haleluyah) 

Rejea toleo la 12 katika blog yetu lililokuwa na kichwa, “Ogopa kuogopa” (http://lifeminusregret.blogspot.com/2015/08/ogopa-kougopa.html).  Ni kweli kama wakristo hatuna sababu ya kuogopa, na kwa wale ambao wanaona hawawezi kabisa kuisha bila hofu hao tunawasihi angalau waogope kuogopa. Si unajua hata daktari akiona hauna ugonjwa unaokusumbua, lakini unadai unaumwa huwa anaandika panadol, basi dozi yako “ogopa kuogopa”.
Mchungaji David Wilkerson Yule wa kitabu cha “ Wahuni waliobadilika” amekuwa mfano mzuri kwetu. Moja ya kauli zake anasema: “Worry is the tendency of those who have no heavenly Father” yaani, “Hofu ni tabia ya wale wasio na Baba wa mbinguni”. Yesu anasema msijisumbue mtakula nini wala mtavaa nini. Umewahi kujiuliza ni kwa nini Yesu anasema hivi? Jibu ni rahisi; tunaye Baba yetu wa mbinguni ajuaye kama tunahitaji hayo.
Hofu inaletwa na uyatima, hofu ni ukosefu wa Baba wa mbiguni. Kwa watu wa mataifa hofu kwao ni ibada. Mtoto asiye na wazazi ni lazima ajitafutie kila kitu, ni lazima ajilinde na ajisimamie. Majukumu haya huwa ni mazito na hivyo humfanya aishi katika hofu. Lakini sivyo ilivyo kwa wakristo, sisi tumeitwa kupumzika, Baba yuko kazini.  (Mathayo 11:28)
Kikomo cha hofu ni pale mtu anapofanyika Mwana. Njia ya kufanyika mwana ni kupitia Imani kwa Yesu Kristo. Imeandikwa, “Bali wote waliompokea [Yesu Kristo] aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu ndio wale waliaminio Jina lake” Yohane 1:12
Mara mtu anapofanyika mwana anapaswa kuachana na tabia za watu wa mataifa ambao hawana Baba mbinguni ila duniani tu. Mhubiri mmoja anasimuli, alipokuwa akiomba bibi yake alimsikia na akamkosoa kwa kumwambia, “Unaomba vibaya”. Alipomuuliza bibi kwa nini unasema hivyo? Bibi yake akamjibu, “Unaomba mambo madogo Mungu ni Mungu Mkubwa”. Ni kweli, ingawa tunaye Baba wa mbinguni anayejishughulisha na mambo yetu lakini bado wengi wetu hawajui kuringa, hawajui kuomba mambo makubwa wanasumbukia mambo ambayo wasio na Baba wa mbinguni husumbukia pia. Mungu atusaidie tufanywe upya nia zetu!
Kifo cha Yesu kilikuwa sababu pekee iliyofanya mitume wake waogope. Walikuwa wanashinda ndani, milango ikiwa imefungwa kabisa. Leo hii Yesu Kristo yuko hai lakini bado wakristo wanaogopa. Kwa jinsi wakristo walivyo wengi, kama kila mmoja angetembea katika faida ya ufufuko wa Yesu basi badala ya kusikia, kokolikoo…. asubuhi mapema  tungesikia Haleluyah….Haleluyah…Haleluyah…. Haleluyah
Ninafanya hivyo karibia kila siku ninapo tafakari pendo lililo msukuma Mungu Baba kuandika mpango wa wokovu. Na mwisho wa tafakari yangu jadidi huwa ni Haleluyah, Haleluyah. Ni kweli, hakuna awezaye kumshinda mtu anayemsifu Mungu. Mitume walipata mashaka wakidhani Yesu ataoza kaburini, lakini siku ya kwanza ya juma Yesu alitoka kaburini akiwa hai na hivyo akafuta sababu zote za kuogopa.
Tunataka kujenga kizazi kisichoshangilia matangazo ya vifo, bali kinachosisimka kisikiapo habari za Yesu Yule aliyetoka kaburini. Yule ambaye kaburi lilishindwa kumshika, Yule ambaye mauti ilishindwa kummudu. Yule ambaye kifo kilimwachilia upesi kisimshike tena. Oh! ingekuwa mbaya sana kama Yesu angekaa kaburini milele kama walivyokaa babu zetu na bibi zetu. Huenda tungekuwa wanyonge na wenye hofu. Lakini kwa kuwa Yesu Kristo amefufuka, Simba wa kabila la Yuda, sasa ni Haleluyaaaaaaaaaa, Oh Glory……
Mpe Bwana utukufu maaana Yu hai milele.

0 comments :