Mpaka umevuka, hakuna kusogea..!
MPAKA UMEVUKA HAPA, HAKUNA KUSOGEA...!
Wakati yupo shule (akiwa mdogo),
aliyewahi kuwa kiongozi mashuhuri Dr. Myle Munroe; alikuwa mwanafunzi wa mwisho
darasani katika kila matokeo. Kwa wakati ule hakuna aliyefikiri angeweza
kufanya jambo lolote la maana; si tu ulimwenguni lakini hata katika maisha yake
binafsi. Anasema siku moja wakati anasoma biblia alikutana na na sehemu
inayosema, “Nayaweza mambo yote katika
Yeye (Kristo) anitiae nguvu”; na hapo ndipo ulipokuwa mwanzo wa maisha yake
kubadilika pamoja na mabadiliko kimasomo; kwa wastani wa mwaka mmoja alitoka
kuwa mwanafunzi wa mwisho darasani hadi kuwa mwanafunzi bora shule nzima, mpaka
anamaliza.
Mpaka
tumefikiri sawasawa, hatuwezi kuishi sawasawa. Mawazo yaliyopata nafasi ndani ya mtu juu ya jambo fulani au eneo
fulani la kimaisha, ndiyo yatakayoamua hatima yake katika eneo hilo. Kama mtu
hajaridhika na hali fulani katika maisha yake; njia ya pekee na ya kudumu ili
kutoka mahali hapo, ni kwa kukutana na wazo mbadala litakalo zaa matumaini kwa
kumpa kuona picha iliyobora zaidi anayopaswa kuifanyia kazi. Mwanadamu
atabaki katika hali hiyo hiyo aliyopo mpaka wazo mbadala limeingia na kutawala
katika kichwa chake (Exposure).
Kama tunataka kuwa na matokeo
tofauti na watu wa kawaida (average people) au tofauti na wakati uliopita
katika eneo fulani; ni lazima tufikiri na kufanya tofauti. Kama haulidhishwi na
kiwango cha kimaisha au kiroho ulichopo sasa; hali hiyo ya kutokuridhika
unayoisikia ndani yako ni wito wa
kukutaka ufikiri na kufanya tofauti na unavyofanya
sasa. Mwanasayansi Albert Einstein
amewahi kusema, “Ni uendawazimu; kufanya
kitu kile kile kwa namna ile ile, na kutegemea kupata matokeo tofauti” (Tafasiri isiyo rasmi)
Hakuna mtu
anayeweza kwenda mbali zaidi ya mawazo yake aliyonayo sasa; mpaka umeelewa jambo hili, mambo hayawezi kusogea.
Isaac Newton, “mwanafisikia” katika kanuni yake ya kwanza (Newton’s first law of motion) anasema, “Kitu kitabaki katika hali yake hiyo hiyo iliyopo, mpaka imekutana nguvu
kutoka nje” (Tafasiri isiyo rasmi)
Mwandishi wa karne ya kwanza Paul
katika kitabu chake kwa wafilipi anatoa vigezo vya kuzingatia unapochagua aina
ya mawazo yanayopaswa kupata nafasi na kutawala ndani yako; akiwa na maana
kwamba, endapo wazo halitakuwa na sifa au vigezo hivyo, usilipe nafasi ya
kufanya makazi ya kudumu katika moyo [akili] wako.
“Hatimaye,
ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote
yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa
njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote. Yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na
kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni
hayo...” Wafilipi 4:8-9 (Msisitizo
umeongezewa)
0 comments :