Kifo ni hatua muhimu kuelekea mafanikio

2:11:00 PM Unknown 0 Comments

 
KIFO NI HATUA MUHIMU KUELEKEA MAFANIKIO
(DIE TO SELF AND LIVE ALL TO HIM)

Kifo hakina maana moja tu; Kifo ni zaidi ya kupoteza pumzi. Tunapoacha kila jambo tulipendalo kwa ajili ya Bwana tunakuwa wafu katika hali yetu ya ubinafsi na tunakuwa hai kwa BWANA. Tunapopenda mambo yetu binafsi na kuyakataa ya BWANA MUNGU tunakuwa hai kwetu na tunakuwa wafu kwa BWANA. Jambo la msingi ni kuwa hai kwa BWANA. Biblia inatutaka tujitoe kama dhabihu hai. “…Itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai...” Warumi 12:1
Watu wengi wakuu wamepitia kifo, na katika kipindi hicho cha kifo agenda zao binafsi zilikufa na agenda za Mungu zikahuishwa na kutukuka katika maisha yao. Miaka 27 jela ilimfanya Nelson Mandela awe kama mfu katika ubinafsi wake, miaka 40 ambayo Musa alikaa Midiani ilimfanya awe mfu kwa agenda binafsi na awe hai kwa agenda za Mungu. Charles Spurgeon amewahi kusisitiza kwamba ufunguo wa mafanikio yote ni mmoja nao ni: “Die to self and live all to Jesus” yaani, “Ufe katika ubinafsi wako na umwishie (uwe hai) Kristo”
Hudson Taylor Mmisionari aliyeacha alama ya aina yake kule China amekuwa msaada kwangu kila nisomapo habari zake. Naye kama mtu mwingine yeyote alilazimika kufa ili mapenzi ya Mungu yachukue mkondo katika maisha yake. Hii ni moja ya kauli zake kabla ya kuliacha jiji zuri la London na kuelekea China kama Mmisionari. Alisema, “Kwa ajili ya kusudi la kwenda China niko tayari kutoa kila kitu, kila sanamu, hata kama ninaipenda.”  Yaani  “For this I could give up everything, every idol, however dear”
Kwa kuwa Mtume Paulo alipenda sana sheria kuachana na sheria kwake ilikuwa ni sawa na kifo. Kwake kuacha sheria na kuiona kama mavi ni kuachana na jambo alilolipenda mno. Kwa ajili ya utukufu wa Mungu aliachana nayo. Maandiko yamemnukuu akisema amepata hasara ya mambo yote kwa ajili ya Kristo. Ni kauli ya ndani, ni kionjo cha moyo. Nimepata hasara ya mambo yote! Paulo alikufa katika ubinafsi wake ili Mungu atukuzwe. “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.”Wafilipi 3:7
Kila mtu mkuu ninaye mtazama kwa asilimia fulani naona jinsi alivyokufa katika mambo binafsi ili ajenda za Ki-Mungu na Ki-utu zipate nafasi. Nyerere alijikatalia wizi ili usawa utawale nchini mwetu Tanzania. Tangu akiwa sekondari Tabora  hakuwapenda wanafunzi waliokuwa wanachukua chakula kingi bila ya kujali wenzao. Bill Winston aliacha kazi ili kutii wito wa Mungu wa uinjilishaji. Reinhard Bonnke alijikatalia kukaa Ujerumani baada ya kuona maono ya bara la Afrika likioshwa kwa damu ya Yesu, akaamua kuja Afrika. Leo hii hawa wote ni watu wakuu na waliofanikiwa kuandika historia nzuri.
Je, uko tayari kuacha ubinafsi na kufa ili Mungu aishi ndani yako? Je, unadhani ni kitu gani Mungu anataka utoe kwa ajili ya utukufu wake? Umewahi kuwaza uzuri wa mafanikio yako ikiwa utatii na kujitoa kwa Mungu?
Nasikia moyoni mwangu ule wimbo wa tenzi “Yote kwa Yesu” ukiimbwa hebu utafakari na ukiweza imba. Moja ya beti inasema, “Nimeacha na anasa kwako Yesu nipokee.”   Oh! jitahidi ujitoe kwa Yesu, na kuachana na anasa za kidunia. Yes All to Jesus I surrender…Endelea kuimba na hakikisha unajitoa na unayaua mapenzi yako ili Yesu atukuke.  Mpaka wiko ijayo, Shallomu!

0 comments :