Mabaya hayatakupata wewe
(Hata baya litageuka na kuwa jema
kwako)
Mungu
haleti mabaya; hata kama yakitokea
huyageuza mabaya kuwa mazuri. Kwa wenye tumaini hata wanapoona jambo
lenye sura ya kutisha bado wanaamini halitakuwa la kuwadhuru. Wana wa Israeli
wakiwa utumwani Babeli, walipatwa na machungu mengi; hawakuwa na makazi, tena walitengana na ndugu zao. Katika kizazi
chetu cha sasa hatujaonja hali ya utumwa wa kitaifa. Kama ilivyokuwa kwa wana
wa Israeli, zamani watu walichukuliwa toka Afrika kama watumwa na kupelekwa
Ulaya kufanyishwa kazi nzito. Si rahisi mtumwa kuamini kama bado Mungu ni mwema
kwake.
Wana
wa Israeli hawakujua mabaya hayo yangekuwa mpaka lini. Hawakujua ukomo wa
utumwa wao. Katikati ya shida yao (utumwa) Mungu ananena kwa kinywa cha nabii
Yeremia kwamba anawawazia mema. Anapanga mizuri kwa ajili yao kwa hiyo
wasiogope. “Maana nayajua
mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya,
kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” Yeremia 29:11
Si
rahisi kwa mtu aliyekatika shida kuamini kwamba Mungu anampango mzuri na maisha
yake. Katikati ya ombwe la kukosa ajira lazima uamini Mungu anampango mzuri na wewe.
Katika hali ya kuugua lazima ujipe moyo kwamba Mungu anampango mzuri. Katikati
ya kutengwa na kuachwa bado lazima utambue Mungu ana kusudi jema. Katika hali
ya utumwa Mungu anasema na Israeli kwamba mambo yatakuwa mazuri.
Njia
za Mungu ni juu sana. Pale ambapo adui anapanga mabaya na kuleta utumwa Mungu
hugeuza mabaya hayo na kuwa mazuri. Wakipanga kukwamisha watajikuta
wanakufungulia njia bila wao kujua.
Tyndale
Mwingereza ambaye ni mmoja kati ya watafsiri wa awali walioandika Biblia katika
lugha ya kiingereza anahusishwa na simulizi zenye mafunzo mengi. Tyndale
alifanya kazi kama mtafsiri katika nyakati ambazo Biblia ilikuwa katika lugha
ya kilatini na haikuruhusiwa kutafsiri kwenda lugha nyingine. Kwa nia ya
kumkwamisha, Askofu mmoja wa Durham alinunua nakala zote za Biblia toka kwa
mwuza vitabu kwa nia ya kwenda kuziharibu, akidhania kwamba jambo hilo
lingekwamisha kazi ya Tyndale. Badala yake pesa hiyo ilitumika kununua
malighafi zilizoandaa toleo jipya na bora zaidi. Tyndale alipohojiwa akiwa
gerezani alitakiwa amtaje aliyemfadhili katika uandishi wa toleo bora la Biblia
alisema ni Askofu Durham. Nadhani umeona walipanga kumkwamisha kwa kununua
Bibla zote na kuzichoma wasijue ya kwamba, pesa yao inaweza kusaidia kuandaa
toleo bora zaidi.
Tangu
kale mpaka sasa Mungu ni mwema. Kila mahali wanasema Mungu ni mwema wala huna
haja ya kuogopa. Yesu Kristo ni mfalme na alikuja kutuokoa, lakini njia
aliyoitumia kutuokoa haikueleweka mioyoni mwa wengi. Wengi walidhani mfalme
atatuokoa kwa kutumia vita wala si kwa njia ya msalaba. Wengi waliona msalaba
kama njia dhaifu, walitegemea kuona farasi wa moto, mabomu na mikuki, kwao kufa
msalabani haikuwa njia sahihi ya kutuletea wokovu.
Oh!
ilionekana ni njia dhaifu kumbe ni njia sahihi na kamilifu. Endelea kumtumaini
Mungu, mwombe akuletee wokovu lakini usichague njia. Hata kama hatuoni wala kuzielewa njia za Mungu bado twaweza kuziamini.
Don Moen mwimbaji wa nyimbo za injili mwenye alama amerekodi maneno haya kwa
uchache nanukuu: “He (God) works in ways
we cannot see” (Mungu hufanya kazi kwa namna tusiyoweza kuona)
Hata
shetani hakujua kwamba kwa njia ya msalaba watu watakombolewa. Angelijua
asingelimchinja Yesu Kristo. Hawakujua kwa njia ile dhaifu BWANA anatupatia
ushindi. Mwenye hekima mmoja anasema: “When the devil killed Jesus, Jesus
Killed the devil.” Yaani, “Pale shetani alipomuua Yesu, Ndipo Yesu alipomuua shetani.”
Endelea kumwamini Mungu.
0 comments :