Je unalijua hili?
Ili
kufanikiwa katika jambo lolote; liwe kubwa au dogo, inahitajika nidhamu; pia
ili kutunza mafaniko ya jambo hilo ulilolipata kwa sababu ya nidhamu uliyokuwa
nayo wakati unaanza, unahitaji nidhamu pia. Hakuna mafanikio ya kweli yasiyohitaji
nidhamu dhabiti. Nioneshe mtu
aliyefanikiwa; nikuoneshe mtu mwenye nidhamu katika njia yake. Ni nidhamu ndiyo inayoleta mafanikio; Ni
nidhamu ndiyo itakayotunza mafanikio hayo.
Mchezaji
wa mpira wa kikapu kwa jina Michael Jordan, alikuwa akiamka alfajiri na mapema
na kwenda uwanjani peke yake, ili kufanya mazoezi. Wakati vijana wa umri wake
wamelala, yeye alifanya mazoezi. Alijua kuwa hawezi kuwa bora katika kikapu “basketball”
endapo atafanya mazoezi kwa kiwango na kiasi cha muda ule ule sawa na watu
wengine. Nidhamu yake ilikuwa ya hali ya juu. Kwa sababu ya nidhamu hii,
jina lake linatajwa katika kila kona, kama shujaa wa mpira wa kikapu
ulimwenguni. Watu wengi hutamani kuwa na mafanikio kama yake; lakini hawako
tayari kulipa gharama ya kuwa na nidhamu aliyokuwa nayo. Nioneshe mtu mwenye nidhamu, nikuoneshe hatima yake.
“Watu wakuu hawakufikia kilele cha cheo kwa
sababu walikimbia (hawakuwa na uwezo
kuliko wengine); bali wakati wenzao
walipolala wao walipanda juu” (kitabu cha uongozi wa Kikristo, Oswald
Sanders, msisitizo umeongezwa)
“Kama ungejua mambo uliyoyapoteza katika
maisha kwa sababu ya usingizi [uliopitiliza],
ungeshangazwa sana” (Pastor Chris Oyakhilome, msisitizo umeongezwa)
Nidhamu ni uwezo na nia ya kujitawala na kujiongoza; kuamua kujiwekea mipaka,
kujinyima, kujikatalia na kujizuilia mambo yanayoonekana kuwa mazuri sasa ili kupata yaliyo bora zaidi kesho.
Ni muhimu kujiwekea viwango (standards) vya maisha na kuvisimamia, lazima
kujijengea uwezo wa kuwa na msimamo ulio dhabiti; na kusimamia maamuzi yako ili
kufikia mfanikio ya malengo uliyojiwekea.
Je
unajua gharama ya kutokuwa na nidhamu [discipline /self-control]? Gharama ya
kutokuwa na nidhamu ni kuharibu maono na ndoto zako. Hata kama tutakuwa na
malengo, pamoja na mipango mizuri, hasa katika mwanzo huu wa mwaka; kama hatutachagua kujenga nidhamu dhabiti;
ni sawa na mtu anayekimbia haraka ili kuwahi mahali asipopajua.
Njia
ya mkato inatajwa kuwa chanzo cha ukosefu wa adabu na nidhamu. Badala ya
mazoezi watu wanatumia dawa za kuongeza nguvu michezoni kama njia ya mkato.
Badala ya kusoma watu wanaiba vyeti kama njia ya mkato. Badala ya subira watu
wanaingia katika tabia chafu kama njia ya mkato. Ni kweli, easy way is the
source of all immoral behavior!
Kumbuka;
kusoma Neno la Mungu kunahitaji nidhamu, Kuweka akiba kunahitaji nidhamu,
kuamka mapema kunahitaji nidhamu, mahusiano bora yanahitaji nidhamu, matumizi
bora ya muda yanahitaji nidhamu, kusoma kunahitaji nidhamu; ili kufikia malengo na mipango yako
uliojiwekea unahitaji nidhamu pia…kwa kifupi, hakuna jambo lenye kufaa ambalo
nyuma yake hakuna nidhamu iliyojengeka ili kufanikisha jambo hilo.
0 comments :