Fikra huru kamwe hazifungwi
FIKRA HURU KAMWE HAZIFUNGWI
Mwili
waweza kufungwa lakini fikra huru kamwe hazifungwi. Huwezi kubaki jela kama
tayari akili yako iko nje kwenye uhuru. Kuwa na fikra chanya na sahihi ni
oparesheni (brain surgery) unayoweza kuifanya mwenyewe. Ili kuwa na fikra
chanya hauhitaji kwenda hospitali ya Apollo nchini India au kule John Hopkins
Marekani , unahitaji taarifa sahihi tu. Neno la Mungu ambalo ni Habari njema
ndio taarifa sahihi. Neno la Mungu ni taa
ya miguu yetu, hutupa hekima kuliko watu wa rika letu.
Kupata
mtazamo chanya ni operesheni rahisi kuliko kuwa na mtazamo hasi. Matatizo mengi
ambayo huwapelekea watu kwenda kwa waganga wa kienyeji yana majibu katika mfumo
wa maandishi, majibu hayo yako katika biblia na katika maduka ya vitabu. Badala
ya mkono wa albino iko elimu ya ujasiliamali, wako akina Kiyosaki wanatoa elimu
hiyo. Wako akina Brian Tracy wanatoa elimu ya masoko.
“Shida yako inafanana na gereza, gereza linaweza kuwa na ukuta mrefu, lakini ni wazi pale ambapo mwanadamu hawezi kupanda kwa mikono na miguu anaweza kupanda kwa kuwa na mtazamo (mawazo) sahihi.”
Viko
vitabu vya namna ya kujenga mahusiano bora vinavyoliwa na mchwa ilhali kuna mtu
anaoga dawa barabarani bila nguo ili apendwe na mumewe. Hilo nalo ni gereza
lililowafunga wengi. Naamini Ili uende kwa mganga wa jadi au kienyeji (mchawi)
ni lazima ukamilishe mambo matatu: uwe na akili nyeusi, mtazamo feki, na roho
nyeusi. Wapendwa tujifunze kwenda katika maduka ya vitabu, ili akina sangoma na
wasoma nyota wajumuike katika sera ya kilimo kwanza.
Shida
yako inafanana na gereza, gereza linaweza kuwa na ukuta mrefu, lakini ni wazi
pale ambapo mwanadamu hawezi kupanda kwa mikono na miguu anaweza kupanda kwa
kuwa na mtazamo (mawazo) sahihi. Unajua katika shida watu hulia, hatutegemei
kumuona mfungwa anacheka, au anaimba kwa furaha. Ukiona mfungwa anaimba kwa
shangwe ujue yuko gerezani kimwili bali akili yake iko nje ya gereza.
Hiki
ndicho kilichotokea kwa Paulo na Sila, kwa kawaida usiku wafungwa hulala tena
hugeuka kwa filimbi, wafungwa hawaimbi usiku. Unajua ili tujue kwamba wewe si
mfungwa hauhitaji kuseme, ‘mimi si mfungwa’ matendo yako yakiakisi mtu huru
tutajua wewe u huru kweli.
“Unaweza kuwafunga watu elfu kumi (10,000) wanaolia na kulalamika, lakini huwezi kumfunga mtu mmoja anayesifu na kumwabudu Mungu..”
Paulo
na Sila kimwili walikuwa jela ila kimtazamo walitambua wao si wafungwa. Wakati
wafungwa wamelala wao walianza ibada, mtazamo wao ni wa nje ya gereza. Mfungwa
hafanyi ibada bila kibali wakati wa usiku. Ukiona ana ujasiri huo basi ujue
huyo si mfungwa. Mtazamo wa Paulo na Sila uliwazalia matunda na wakatoka. Mwenye
hekima mmoja anasema, “Unaweza kuwafunga
watu elfu kumi (10,000) wanaolia na kulalamika, lakini huwezi kumfunga mtu
mmoja anayesifu na kumwabudu Mungu.”
Inawezekana
wewe pia una shida lakini ukuta ni mtazamo wako, labda uko jela ya kukosa kazi
au mtoto; badilisha mtazamo wako, tembea kama mtu huru. Nakumbuka wakati sina
kazi, nilikuwa na upako kuliko waendao kazini, nilikuwa nina sababu za
kumshukuru Mungu kuliko wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania hata ya Washington
DC. Nilitoa sadaka kama kawaida.
Siku
nyingine nilikuwa navaa vizuri kama boss! Moyoni najua sina kazi. Nilikua
naombea wengine kazi utadhani mimi ninayo. Mtazamo huru ulinivusha. Ukipata
kazi utafanya nini? Fanya sasa. Paulo na Sila hawakusema tukitoka jela
tutakusifu, walimsifu Mungu wakiwa jela kinyume cha sheria za bwana jela. Mtazamo huru ni kutenda bila kizuizi.
Jela
ni kizuizi, lengo lake ni kukuzuia. Jela huzuia kicheko, jela huzuia tabasamu,
jela hunyima usingizi, jela hutuzuia tusimsifu Mungu wala kutoa sadaka ya
shukrani. Tukiweza kucheka, kutabasamu, kusifu na kushukuru basi tu watu huru,
na milango ya gereza itafunguka.
Akili
yako ikishatoka jela, mwili utakufuata tu. Unaposifu unaunganika na Mungu,
unaalika mbingu duniani. Mungu hakai jela akishuka sehemu inabadilika jina, pengine
aliposhuka huitwa Jehova Jire, mahali pengine Ebenezer na Jehovah Shama. Hawezi
kushuka na eneo likabaki vile vile. Aliposhuka wafungwa wote walikuwa huru,
Paulo na Sila wakageuka wahudumu na si wafungwa tena. Nadhani badala ya kupaita
gereza la ukonga au segerea palipata jina lingine. Leo hii watu huenda Ugiriki
kutazama mahali ambapo Paulo na Sila kwa sifa za BWANA waliandika historia ya
ushindi. Mungu aliyeweka siku ya kuanguka kwako ndiye atakayeleta siku ya
kusimama kwako. Hebu msifu BWANA na tetemeko litokee kwako leo kama wakati wa
Paulo na Sila. Amen