Linda Maamuzi yako ...
LINDA MAAMUZI YAKO, HASA WAKATI
UNAPOKUTANA NA CHANGAMOTO
Je
baada ya miaka mitano au kumi au baada ya muda kupita kutoka sasa, utajipongeza
kwa uamuzi uliochukua au utajilaumu? Utafurahi na kushangilia au utajutia na
kutamani kurudi nyuma ili kusahihisha uamuzi uliochukua? Kumbuka kila kitu kipo
katika uweza wa mtu mwenyewe na anawajibika kwa matokeo yote ya uchaguzi na
uamuzi wake.
Maamuzi
yako ya leo yana sehemu kubwa sana katika kuamua (determine) hali yako ya
baadae kiroho, kiuchumi, kihuduma na hata kifamilia; lakini pia maamuzi yako ya
leo yana sehemu kubwa katika kuamua hali ya baadae ya watu wanao kuzunguka.
Kesho yako, unaiamua leo kwa kujua au kwa kutokujua. Maisha yako ya kesho
yamefungwa katika maamuzi yako ya leo. Kesho nzuri inajengwa na maamuzi mazuri
ya leo; maamuzi yako ya leo ni ‘mbegu’ unayopanda, ndani yake imebeba maisha
yako ya kesho (maisha ya baadae).
“Kesho nzuri inajengwa na maamuzi mazuri ya leo; maamuzi yako ya leo ni ‘mbegu’ unayopanda, ndani yake imebeba maisha yako ya kesho.”
Jambo
kubwa ambalo adui anawinda wakati mtu anapitia changamoto fulani katika maisha,
ni maamuzi yake; rafiki yangu hupenda kusema, “Kwa mtu mwenye njaa hata sumu kwake huwa ni chakula” ikiwa na maana
kwamba, mtu anaekutana na changamoto anaweza kufanya maamuzi hata yatakayomdhuru
yeye mwenyewe baadae. Mtu huyu anafanya maamuzi kulingana na hali ya changamoto
anayokutana nayo wakati huo. Ndio maana ni muhimu sana kulinda na kuwa
muangalifu na maamuzi unayofanya hasa wakati wa changamoto (challenge).
Shauku
ya adui ni kuona unakosea kuamua. Mara nyingi “presha” ya jambo inapoongezeka
ni rahisi sana kusahau au kutokuzingatiza mambo ya msingi uliyokwisha kuamua au
kuyajua kabla ya jambo hilo kutokea. Presha ya mazingira unayoyaona sasa
inaweza kukusahaulisha dira na malengo makuu ya maisha. Mtu anapopitia wakati
mgumu, huweza kufikiri ndio mwisho wa maisha yake, au mwisho wa ndoto na mipango
yake. Ukweli ni kwamba hakuna changamoto itakayo dumu milele.
Esau
alifanya uamuzi wa kuidharau na kuiuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo
mmoja na hivyo akaikosa Baraka inayoambatana na haki hiyo. Maamuzi ya siku moja
yaliharibu na kubadili kabisa uelekeo wa maisha yake na uzao wake (Mwanzo 25:29-34,
Ebr 12:16).
Kabla
ya kufanya uamuzi au uchaguzi fulani katika maisha, ni muhimu kuangalia picha
ya mbele ya maisha unayoyataka. Kuamua kwa kuangalia mazingira yanayotuzunguka
hakutupi uhakika wa kufikia malengo makuu katika maisha. Ndio maana ni muhimu
kuwa na maono na ndoto inayokupa picha ya maisha ya baadae na kutupa msingi wa
kujengea maamuzi yetu ya kila siku ili kufikia ndoto hizo.
Na hiki
ndicho lilichomsaidia Yusufu kusonga mbele pamoja na changamoto zote
alizokutana nazo hata kufikia ndoto na picha ya maono ya maisha yake ya kuwa
kiongozi mkuu katika jamii. Kwa Yusufu, changamoto hazikuwa kikwazo bali jiwe
la kukanyagia ili kufikia ndoto yake. Changamoto zilimpa nguvu ya kusonga mbele
huku akijua Aliyeahidi ni Muaminifu na kwamba atatenda sawa sawa na alivyoahidi
katika Neno lake
“Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutoamini, bali alitiwa nguvu katika imani, Akimtukuza Mungu. Huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi” Warumi 4:20-21 (Msisitizo umeongezwa).”
Tunaweza
kupoteza muelekeo katika kuamua pale tunapoacha kuangali ahadi ya Mungu na
kuanza kuangalia mazingira au hali zinazotuzunguka kwa wakati huo. Kumbuka
jambo hili; Mungu anapokupa wazo au maono (vision), mara nyingi mazingira yako
hayatalingana na maono hayo. Wakati Habakuki anapitia changamoto pamoja na
jamii yake, hili ndilo lililokuwa jibu la Mungu kwake ili kumsaidia kulinda
maamuzi yake na jamii yake kwa wakati huo;
“…Bwana akajibu, akasema, iandike
njozi (ndoto, maono) ukaifanye iwe
wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii
bado ni kwa wakati ulioamuriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake,
wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja,
haitakawia” Habakuki2:2-3 (Msisitizo umeongezwa)