Pasipo Msongo wa Mawazo II

6:38:00 PM Unknown 0 Comments



PASIPO MSONGO WA MAWAZO II
(STRESS FREE ZONE)
1.    Mpaka lini?
Wabeba maono wengi, watu wenye mipango ya muda mrefu na wenye shabaha za kipekee wanaweza kuwa wahanga wa swali hili. Hili huwakumba wengi ambao wanaona umri unakwenda, wanatamani wasimamishe saa ili watekeleze mpango kazi wao. Wana mipango na mawazo ya kiuchumi na kijamii ambayo wanashuhudia waziwazi  yakipishana na muda. Swali hili huua moyo wa Rick Warren anasema, “Hurry Kills Prayer.” sala na kutangaza maombolezo.
Swali hili linaonesha mtu amechoka kuomba na anataka kuchepuka, kupita njia ya mkato. Tunaweza kupata pumziko kama tutajua ya kuwa, kila kitu ni kwa ajili ya kuwapatia mema wale wampendao Mungu. Mungu anajua uzuri wa kuchelewa, ndio maana anaona bora usubiri ili upate kitu bora kuliko kuwahi na kuwa bora kupata kitu. Kukosa kazi, Kuchelewa kufikia mafanikio, kukawia kwa ndoto zako, kupoteza mali, kusingiziwa na kufukuzwa ni kwa ajili ya kukupatia mema. Mambo yote, mazuri na mabaya ni kwa ajili ya kukupatia mema. “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” Warumi 8:32
“Mungu anajua uzuri wa kuchelewa, ndio maana anaona bora usubiri ili upate kitu bora kuliko kuwahi na kuwa bora kupata kitu.”
Mpaka ujue maana ya tatizo lako ndipo litakapogeuka kuwa rafiki kwako. Kwa zaidi ya miezi sita nilikaa nyumbani bila ajira, inaumiza kwa kiasi fulani hususani kwa mtu mwenye maono na majukumu. Lakini kama nisingelipata nafasi ile nisingelimfahamu Mungu kwa kiasi hiki. Mungu anajua jambo la kukupa furaha badala ya pesa na badala ya kazi. Ni katika muda huo mgumu tumeandika vitabu viwili. Ningekuwa kazini nisingeliweza. Kila kitu kinasababu yake nzuri na yenye faida.
2.   Kwa nini nimepelekwa sehemu mbaya?
Watu wengi wanapenda maeneo mazuri ya kazi, pia ni wenye kuvutiwa na mikoa mizuri. Wanapenda makazi mazuri na maeneo yenye Baraka. Mimi pia ni mmoja wao. Lakini jambo la msingi ni lazima tujifunze kuwa baraka na si kukaa katika eneo lenye Baraka. Kuwa best badala ya kukimbila sehemu nzuri. Ukishakuwa Baraka au ukisha kuwa bora eneo litabadilika kwa sababu yako. Wakati Lutu akikimbilia bonde zuri la sodoma na gomora, Ibrahimu alienda sehemu ya kawaida tu. Kwa kuwa Ibrahimu ni baraka hata alikokwenda kuligeuka Baraka. Ukijua hili hutakuwa mtumwa wa mitaa na mikoa. Siku chache zimepita nilimwandikia rafiki yangu ujumbe kama huu, “As long as God dwells in me, When I move He moves.” Baraka si swala la upande wa kushuto na kulia ni habari inayokuhusu wewe na si mazingira. Ibrahimu alijijua kwamba, yeye ni baraka na hivyo hakutegemea mazingira badala yake alimtegea Mungu. “Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto.” Mwanzo 13:9
“Uchoyo hutunyima raha, tusipotoa zaka, tusipotoa sadaka na malimbuko tunakujikuta katika huzuni.”
3.   Je, Nijitoe kabisa?
Watu wengi wanapenda kujitoa kwa sehemu tu, na si kujitoa kabisa pasipo kujibakiza. Wengi ni vuguvugu, wanaenenda nuruni na gizani. Hata katika sadaka wengi hufanya hivyo, hutoa sehemu ndogo isiyowaumiza yaani, mabaki. Mara zote kabla Mungu hajakuhimiza utoe sadaka, huhimiza kwanza mtu ajitoe mwenyewe. Mungu anahitaji nafsi yako kwanza kabla ya pesa na sadaka zako. Msongo wa mawazo, huzuni na uharibifu hutokea kwa sababu tumekataa kujitoa. Hata katika sadaka jambo hili hutokea, tunapokataa kutoa kama tulivyoshuhudiwa ndani ya nafsi zetu huwa tunabaki na huzuni [stress]. Kuna wakati sikutoa pesa ambayo Mungu alitaka nitoe kutoka katika mshahara wangu, kweli pesa nilibaki nayo; lakini sikuwa mwenye furaha, wala sikujua ilivyokwisha. Ni kama mali bila daftari hivi!
Uchoyo hutunyima raha, tusipotoa zaka, tusipotoa sadaka na malimbuko tunakujikuta katika huzuni. Kuna furaha katika kumpenda Mungu na kumtii. Msongo wa mawazo na huzuni huja kwa sababu roho hupenda kumtii Mungu, kwa hiyo inapozuiwa kwa makusudi huumia na hivyo mtu husikia huzuni.
Ukijitoa kwa Mungu utabaki na furaha, ukishindwa kutoa utabaki na mali zako sawa; lakini utabaki na huzuni pia. Kila tunaposhindwa kujitoa kwa Mungu wetu tunaalika huzuni maisha mwetu. Kumbuka Yule kijana tajiri alivyokataa kuuza mali zake, japo alikuwa ameshika amri zote, hakujipambanua na mali zake, nafsi yake iliambatana na vitu kuliko Mungu. Licha ya Yesu kumwambia auze hakukubali, alibaki na mali zake lakini pasipo furaha, biblia inasema:
Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.Mathayo 19:22