Pasipo Msongo
PASIPO MSONGO WA MAWAZO - I
[Stress Free Zone]
Katika
maisha haya ya sasa watu wengi wanakabiriwa na maswali mengi; na wale wasio na
maswali wana majawabu ya uongo yaani, ambayo si sahihi. Lini nitaajiriwa? Lini
nitaolewa? Nitavaa nini? Nini itakuwa hatima ya maisha yangu? Ni miongoni mwa
maswali tata katika kizazi chetu.
Kwa
kuwa ukombozi wa Yesu Kristo unahusisha; mwili nafsi na roho hakuna namna
tunavyoweza kuepuka kujibu maswali haya kama viongozi na watumishi katika
Kristo. Kwa wanasiasa baadhi ya maswali haya ni mtaji wao wa kuwafikisha katika
matarajio yao.
“Kila mmoja wetu anahitaji kuishi pasipo msongo/mgandamizo wa mawazo, pasipo moyo mzito; bila ya hofu wala mashaka yoyote.”
Kila
mmoja wetu anahitaji kuishi pasipo msongo/mgandamizo wa mawazo, pasipo moyo
mzito; bila ya hofu wala mashaka yoyote. Tunahitaji kuwa wepesi, tena tunapaswa
kuwa wenye nguvu. Mt Francis De Sales amewahi kunukuliwa akisema: “Mtakatifu mwenye uso wa huzuni [asiye na
furaha] ni mtakatifu bandia”
Moja
ya kitu ninachokosa ninapozuru katika hoteli na maeneo mbali mbali ya huduma ni
tabasamu. Watoa huduma wengi hawana tabasamu bashasha, wana uso unaonesha
kwamba, maswali yao hayajajibiwa. Kwa nini ameniacha? Kwa nini nimepelekwa
kule? Kwa nini mimi nimekosa? Kwa nini hajanitetea? Yote haya hupasua vichwa
vya wengi.
Tuanze
kujibu maswali haya ambayo huitwa pasua kichwa, tunatoa majibu ili uondokane na
mganadamizo/msongo wa mawazo kwa kizungu, ‘stress’.
1.
Nitaweza
kweli?
Mara
nyingi tunakabiriwa na majukumu mazito na pengine tusiyoyaweza. Mara nyingi
watu hujiuliza: nitaanzaje, nitasema nini mbele yao, nitamwambia nini,
itakuwaje na watanionaje. Nakumbuka siku
yangu ya kwanza kazini nilijikuta katika wakati mgumu, nilitakiwa kufanya kila
kitu cha uhasibu na hakukuwa na mtu wa kunielekeza. Stress nyingine
husababishwa na kukabiliwa na tishio la majukumu mazito.
Katika Mithali 16:3 maandiko yanasema: “Mkabidhi Bwana
kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.” Biblia ya
kiingereza inatumia neno, ‘roll’ yaani, kabidhi au achilia. Picha nzuri ni kama
vile unapokuwa na kitu kizito cha duara au mviringo na kwa kuwa hauwezi
kukibeba unaamua kukiachilia katika mteremko au mikononi mwa mwenye nguvu ili
kiende haraka au ili akibeba na wewe ubaki huru. Hiyo ndio maana ya kumkabidhi,
ni vema ujifunze kuviachilia na kuvisukuma [roll] vitu vyote vinavyokukabili
ili kuondokana na mgandamizo wa mawazo. Visukume kuelekea mikononi mwa Mungu,
yuko ili kukusaidia. Ni vizuri wewe ushindwe ili Mungu akuwezesha. Please roll!
“Muda huu unaposubiri ni kwa ajili ya faida ni ili kukuletea mema, kuna kitu kizuri Mungu anafanya wakati huu ambapo uko peka yako.”
2.
Nitaolewa
lini na nani? Nitaoa lini, nitamuoa nani?
Kila
kijana anapenda kupata kitu chema yaani, mke mwema na mume mwema. Nitakujibu
kupitia historia yangu, siku moja nilipasua kichwa changu nikitafuta jibu la
maswali haya. Nitamuoa nani na lini? Hatari mojawapo inayofutana na swali hili
ni kujirahisisha siunajua usemi huu, “kwa
mtu mwenye njaa hata sumu ni chakula.” Nikiwa nawaza niliamua kuomba, na
katika sala Roho aliniambia taratibu mambo machache na moyo wangu ukalipuka kwa
furaha. Alisema, “Jambo pekee ambalo Mungu angeweza kuwazuilia wanadamu
(kuwanyima) ni kumtoa mwanaye wa pekee Yesu Krsito wala si mke mwema. Kwa kuwa
alishamtoa Yesu pale msalabani hawezi kuacha kukupatia mke mwema.” Baadaye
alinidokeza tena kwa kizungu, “everything works for good to them that love God”
yaani, ‘Kila kitu kinafanya kazi ili kuwapatia mema wale wampendao Mungu.’ [Warumi 8:32]
Muda
huu unaposubiri ni kwa ajili ya faida ni ili kukuletea mema, kuna kitu kizuri
Mungu anafanya wakati huu ambapo uko peka yako. Wakati huu, kabla hujaolewa ni
mwema na Mungu ana makusudi nao tafadhali furahi.
Sala
nzuri kwa mtu ambaye hajaoa au kuolewa ni ile inayomsaidia kujilewa na
kuwaelewa watu wengine. Mithali hii ya kichina ni ya muhimu: “Seek to
understand before seeking to be understood” Ni sala inayompa kijana nafasi ya
kuvaa mavazi ya kiroho yaani, huruma, rehema, heshima, utakatifu, utu wema,
fadhili na ibada {Waefeso 4:32}. Mpaka pale mtu anapovaa huruma, fadhili, na
msamaha ndipo anaweza kuwa mtahiniwa sahihi wa ndoa [right candidate].
3.
Kwa nini
nijishushe?
Changamoto
nyingine ambayo ni pasua kichwa ni swala la unyenyekevu ambao wengi hudhani ni
utumwa. Jambo hili limevunja mahusiano ya watu wengi katika ngazi mbalimbali,
toka ofisini mpaka kwenye familia . Kwa mfano, kama umesoma uhasibu na siku
moja ukafagia ofisi kitendo hicho hakikuondolei uhasibu wako. Tumezoea kuona
watoto wakiwanawisha mikono wakubwa zao yaani, rika la juu; na ni utaratibu
mzuri katika jamii zetu, tena ni wa kitambo. Siku moja baba mmoja aliamua
kuacha kidogo utaratibu huu na akathubutu kuwanawisha mikono watoto wake wote.
Na baada ya kumaliza kuwanawisha mikono na kuwafuta akawauliza swali, “Je,
mmekuwa baba zangu?” wakajibu, “Hapana.”
Alitaka wajue soma hili la kunyenyekea, ukijishusha haikuondoi kwenye
nafasi yako, badala yake inakupandisha zaidi. Alitaka wajue kwamba unyenyekevu
hauwaondolei nafasi zao, baba atabaki kuwa baba hata kama ndiye atakayepika
siku hiyo. Tusipojua hili tutaendelea kupigana, ni rahisi kusikia mtu akilaumu
kwa maneno haya: huyu hana adabu, hajatoa vyombo, hajaniheshimu, anadhani tuko
sawa. Yesu aliwaosha mitume miguu yao, na bado amebaki kuwa BWANA, MUNGU na
MFALME. Kwa kutoa koti la nafasi zetu ndio tunaziimarisha zaidi wala
hatutaondolewa. Mtu mmoja anasema, “Mambo
ambayo nilikuwa nayafanya katika kazi ndogo, ndiyo niliyokutana nayo katika
usaili wa kuelekea katika ofisi nyingine” Kukubali kwake kufanya kazi
mahali penye hadhi ya kawaida ndio ilikuwa ngazi ya kumpeleka juu, tafadhali
nyenyekea wala usidharau huo mwanzo mdogo.
“Neno linatukutaza kuisumbua kesho lakini halitukatazi kuwaza na kupanga kwa ajili ya mwisho wetu yaani, future.”
4.
Nini
itakuwa hatima ya maisha yangu?
Mara
nyingi tunawaza sana kuhusu hatima yetu na hivyo tunapoteza furaha ya sasa.
Ibrahimu alikuwa anajikuta katika msongo wa mawazo kila alipowaza kuhusu hatima
yake ya baadaye. Alikuwa mzee, tajiri na mwenye mafanikio mengi, lakini hukuwa
na mtu atakayerithi hayo. Alikuwa anaumia, hakujua nani atarithi jina lake na
mali zake. Alidhani ni Elieza mdamaskasi na kumbe ni Isaka. Usisahau mawazo
mabaya huleta hoja au jawabu tofauti na mpango wa Mungu ambao ni amani. Neno
linatukutaza kuisumbua kesho lakini halitukatazi kuwaza na kupanga kwa ajili ya
mwisho wetu yaani, “future.” Kuna tofauti kati ya, tomorrow na future.
Ukijipanga vizuri leo moja kwa moja kesho itakuwa nzuri lakini mwisho wako
yaani, “future” itakuhitaji ujipange kila siku. Wengi kwa sababu ya kutokujua
mwisho wa siku zetu tumejikuta katika msongo na mgandamizo wa mawazo. Ndio
maana Mungu ameamua kututoa katika hali hiyo kwa neno lake: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia
ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini
siku zenu za mwisho.” Yeremia 29:11
Mawazo
ni jambo la baadaye, huthibitika baada ya kitambo kupita. Mungu angeweza
kuficha mawazo yake kwetu, lakini anayaweka wazi ili tusiwe na wasiwasi.
Anataka tujue kwamba mambo yataenda vizuri yaani kila kitu viwili viwili
[double-double]. Anasema ni mawazo ya amani. Mwanadiplomasia Helmet Coil
amewahi kusema: “peace is more than
absence of war.” Akimaanisha, “amani ni zaidi ya kutokuwepo/kukosekana kwa
vita.” Amani maana yake, chakula cha kutosha, afya njema, fedha za kutosha,
maji safi, familia nzuri, malazi mazuri na uhusiano mzuri na Mungu. Hii ndio
amani anayotuwazia na anayotutamkia Mungu wetu, waipatao huwa kama mti
uliopandwa kandokando ya maji.