Unayo nafasi

7:34:00 PM Unknown 0 Comments

UNAYO NAFASI YA KUANDIKA HISTORIA YAKO-II
Watu na wafanikiwe kupitia kufanikiwa kwako
Kila mtu ana shauku ya kutaka kujua namna ya kufanikiwa na kumiliki vitu. Vitabu vyenye picha za fedha, majumba na vitu vya thamani huchapishwa, makampuni hufunguliwa na mahubiri hutolewa yakiwa na lengo la kuvutia watu katika kufikia ndoto zao. 
Tunaishi katika karne ambayo kila mtu anataka kumiliki vitu [possessions], na wengine wako tayari kupata vitu kwa gharama yoyoye ile hata ikibidi “kukanyaga” haki ya mtu mwingine;   Si ajabu kuona watu wa namna hii wanafanikiwa kupata vitu walivyokuwa wakivitafuta na pia wanafanikiwa kupoteza afya zao, familia, furaha, heshima, mahusiano yao na wengine hata kupoteza maisha yao. Tunaishi katika karne ambayo uthamani wa mtu unapimwa kwa mali, cheo au vitu anavyomiliki na sio ubinadamu wake. Maneno “zangu”, “wangu”, “yangu” “mimi” yanaonekana kuwa na mashiko zaidi katika kizazi hiki. Hii ni hatari!
Baraka ya BWANA hutajirisha na wala hachanganyi na huzuni nayo” mithali 10:22
“Kila mtu anataka kufanikiwa, lakini si kila mtu anaelewa kusudi la Mungu la kuleta mafanikio hayo katika maisha yake”
Kila mtu anayo shauku ya kutaka kufanikiwa; wanafunzi wengi wanasoma  wapate kazi yenye kipato kizuri ili waweze kumiliki vitu, mfanyabiashara pia anatafuta kufanikiwa katika biashara zake ili amiliki vitu, mfanyakazi  anatamani afanikiwe na kufikia cheo cha juu katiika ofisi yake. Kila mtu anaimba wimbo wa mafanikio, hata aliye masikini ana ndoto za kutoka katika umasikini wake na kumiliki vitu. Hii ni kuanzia ngazi ya mtu moja moja hadi ngazi ya taifa. Wakati kila mtu akifikiri na kupanga namna ya kufikia mafanikio katika maisha vivyo hivyo serikali hufikiri na kupanga namna ya kufikia mafanikio kama taifa.
Kufanikiwa au kutamani kuwa na vitu si jambo baya, ni jambo zuri kabisa; Shauku ya kutaka kufanikiwa ipo ndani ya mtu tangu kuumbwa kwake. Ni mpango wa Mungu na ni shauku yake kuona [kuhakikisha] tufanikiwe na kufikia malengo yote katika maisha yetu (Kumb 28:3-13, Yeremia 29:11). Mzee Yohana alipopata ufunuo huu aliandika, “mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo YOTE na kuwa na afya yako...” Mungu anataka tufanikiwe katika MAMBO YOTE sio moja au mawili.  Shida inakuja pale tunaposhindwa kujua sababu (kusudi) ya Mungu juu ya vitu hivyo anavyotubariki navyo.  Kila mtu anataka kufanikiwa, lakini si kila mtu anaelewa kusudi la Mungu la kuleta mafanikio hayo katika maisha yake.
Mahali ambapo kusudi au sababu ya kuwepo kitu haijajulikana, uharibu [destructions] huchukua nafasi; hii ni kuanzia ngazi ya mtu binafsi hadi ngazi ya taifa. Kitu chochote kisipotumika kama kilivyokusudiwa kuna uwezekano kikaharibika au kikatengeneza uharibifu mahali kilipo. Mfano, Ni rahisi zaidi kwa kijana kujiingiza katika uharibifu wa madawa ya kulevya au ukahaba au ujambazi endapo hajui kusudi la Mungu juu ya maisha yake kuliko kijana anayejua kwamba, amezaliwa kwa sababu maalumu. [Yeremiah 1:4-7]
“Mungu anatuinua juu si ili sisi tuonekane bali kwa makusudi ya Yeye apate nafasi (platform) ya kuonekana, kujulikana na kutukuzwa katikati ya watu wake hasa waliopotea ili wapate kumrudia Yeye.”
  1. Vitu vyote hutolewa ili Mungu avitumie kutimiza kusudi lake
Muda, vipawa, fedha, fursa na rasimali watu, vyote hutolewa ili kusudi la Mungu lisimame na ufalme wake uimarike zaidi juu ya nchi. Mafaniko yoyote ni muhimu yakatumika katika kumtukuza Mungu (Kumfanya Mungu ajulikane) mahali ulipo.  Mwana masumbwi Manny Pacquiao ni mfano wa watu wanaoelewa kusudi la Mungu juu ya mafanikio yake katika mchezo wa ngumi, anatumia umaarufu (influence) wake na vitu vyake kumfanya Mungu wake ajulikane na aheshimike. Mafanikio yake yamekuwa madhabahu ya Mungu ya kuwafikia watu wasiofikika kirahisi. Mungu anataka kutumilikisha vitu ili avitumie kutimiza kusudi lake alilonalo juu ya nchi (Possessions are not meant to be the end [purpose] but means to an end).
Mungu anapokufanikisha katika shughuli zako si kwa sababu anataka wewe ujulikane, bali anataka yeye ajulikane. Hatuwi maarufu ili sisi tujulikane, tunakuwa maarufu ili Mungu ajulikane. Mungu anakufanikisha si ili watu wakupigie magoti, anataka kukufanikisha ili watu wampigie Yeye (Mungu) magoti.  Mungu anatuinua juu si ili sisi tuonekane bali kwa makusudi ya Yeye apate nafasi (platform) ya kuonekana, kujulikana na kutukuzwa katikati ya watu wake hasa waliopotea ili wapate kumrudia Yeye. Mungu anataka kutumia mafanikio yetu kudhihirisha; uwezo, nguvu na upendo wake kwa watu wake ili watakapoona nguvu zake katika maisha yetu wasema, hakika BWANA ndiye Mungu  [1Falme 18:36-39]. 
 “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” Mathayo 5:16
“Hatuinuliwi juu ili kuwatizama walio chini, tunainuliwa juu kwa kusudi la kuwavuta wengine juu.”
Swali langu ni je, watu wanapotutizama katika mafanikio yetu wanatuona sisi au wanamuona Mungu? Tunataka tupewe heshima sisi, au apewe Mungu? Baada ya mafanikio yetu tunataka watu waimbe majina yetu au waimbe Jina la Mungu wetu. Jiulize, Kitu gani kinakusukuma (Motivates) kutamani kufanikiwa katika maisha yako, kuwa na vitu n.k? Kwanini unataka kuwa millionea au mfanyabiashara mkubwa, au mwanasiasa anayejulikana sana au mhudumu nchi nzima? Je tunapozungumza na watu juu ya mafanikio yetu kimaisha au kimasomo au kihuduma; wanaona akili na nguvu zetu au wanaona Uwezo wake na Nguvu zake ndani yetu? [Kumb8:12-18]
  1. “Nikiinuliwa nitawavuta wote kwangu”
Hatuinuliwi juu ili tuwe na watu wa kuwatizama chini yetu; au tuwe na watu watakaokaa chini ya miguu yetu. Mungu alimwambia Ibrahimu, katika yeye [through] mataifa watabarikiwa; maana yake, pamoja na kwamba Mungu angembariki yeye na uzao wake; pia, Mungu alimuamini sana Ibrahimu kiasi cha kumpa Baraka za mataifa mengine. Alijua baraka zikipitia mikononi mwa Ibrahimu zitafika kwa wahusika.”...Na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa” Mwanzo12:2-3! Ibrahimu alikuwa mkondo  wa baraka kutoka kwa Mungu kwenda kwa jamaa zote za Dunia.
Hatuinuliwi juu ili kuwatizama walio chini, tunainuliwa juu kwa kusudi la kuwavuta wengine juu. Mwalimu na Kiongozi wetu ametupa mfano mzuri juu ya jambo hili, mara kadha katika mafundisho yake amewahi kusema “Nami nikiinuliwa juu ya nchi nitawavuta wote kwangu”. [Yoh. 12:32] Umepata nafasi ya kwenda shule ili uwe msaada kwa wasiopata nafasi kama yako, Mungu hakukupa nafasi hiyo ili umdharau asiyekwenda shule; hakukupa nafasi ya kupata maarifa kwa ajili yako tu, amekupa maarifa ili jamii, taifa na ulimwengu unufaike na maarifa hayo.  Bill Gate amewahi kuandika, “Tangu siku zangu za mwanzo katika Microsoft, nimetamani kushirikisha [kugawana] na ulimwengu manufaa ya tehamana (Tafasiri isiyo rasmi)
Kwa mtu ambaye ni daraja hata mali zake hufanyika daraja pia. Kwa mwenye kulijua kusudi la Mungu katika maisha yake hata umaarufu wake ni daraja. Wako watu ambao mbao zao katika mitandao (post/status) ya jamii zinasomwa na mimilioni, lakini wanayoyaandika hayamtukuzi Mungu.
“Kile tulichokifanya kwa ajili yetu tu, hufa na kuzikwa pamoja nasi kaburini; lakini kile tulichokifanya kwa ajili ya wengine na kwa ulimwengu huendelea kuwepo na hakitakufa”
Watu wengi wana mafanikio lakini wanagubikwa na huzuni, kwa sababu wamekataa mali na mafanikio yao zisiwe nyenzo ya kuwavusha wengine ili na wao wafikie mafanikio yao. Wametafuta mafaniko ili wawe na mafanikio tu, hawajisumbui zaidi ya hapo. Huzuni ni matokeo ya mtu mwenye maono ya mafanikio tu, na si zaidi ya hapo. Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.Mathayo 19:22; kijana huyu aliyejulikana kama kijana tajiri, alibaki na mafanikio yake pamoja na huzuni nyingi. Alipoteza furaha yake japo akaunti zake za benki zinasoma vizuri. Huzuni na uchoyo ni ndoa isiyovunjika. Kila tunapozuia mafanikio zetu kumpa Mungu utukufu, tununua huzuni.
Kile tulichokifanya kwa ajili yetu tu, hufa na kuzikwa pamoja nasi kaburini; lakini kile tulichokifanya kwa ajili ya wengine na kwa ulimwengu huendelea kuwepo na hakitakufa [hata wakati sisi hatupo]”-Albert Pike, (Tafasiri ya mwandishi)



0 comments :