Itifaki ya Upendo

10:24:00 AM Unknown 2 Comments


ITIFAKI YA UPENDO
(Love Protocol)
Mambo mengi katika maisha ya sasa yanazingatia itifaki. Sote tu mashahidi wa jambo hili, mara nyingi katika kutambulisha, ofisini na hata katika ngazi ya familia itifaki huzingatiwa. Jamii nyingi katika chakula ni wazee ambao hutangulia kunawa au kunawishwa mikono yao kwanza kabla ya rika la vijana na watoto. Mahali pengine ni viongozi wa ngazi za juu huwasili mwishoni baada ya kutanguliwa na wale ngazi za chini, na inafahamika wazi kwamba, viongozi wa meza kuu ndiyo hutambulishwa kwanza. Yote hii ni itifaki.
Amri kumi za Mungu zimekaa katika namna au mpangilio wa ki-itifaki. Ukizisoma kwa utulivu utaona kuna itifaki ndani yake. Zinaanza kwa kuonesha kwamba Mungu peke yake ndiye astahiliye kuabudiwa, zinaendelea na umuhimu wa kuheshimu wazazi na kuwapenda, baadaye zinatufunza namna njema ya kukaa na jirani zetu na kuwapenda.
“Alishatoa kila kitu kwa ajili yetu, hivi sasa hakuna kilichosalia mbinguni. Alipomtoa Yesu alitoa kilicho cha thamani kutoka mbinguni”
Leo tunatamani msomaji wetu uijue itifaki ya upendo (love protocol) ambayo ni muhimu katika maisha yetu ya kila siku. Ni rahisi kabisa, itifaki ya upendo inataka aanze Mungu, ufuate wewe, wazazi na baadaye jirani yako. Mpende BWANA Mungu wako, jipende, na mpende jirani yako kama unavyojipenda.  Mathayo 22:37-39
MUNGU; Ni Baba yetu mwema Yeye alitupenda kwanza, alitupenda upeo. Alishatoa kila kitu kwa ajili yetu, hivi sasa hakuna kilichosalia mbinguni. Alipomtoa Yesu alitoa kilicho cha thamani kutoka mbinguni (Warumi 8:32). Mbele za Mungu Baba, Yesu alikuwa ni kila kitu, ni zaidi ya jinsi Ibrahim alivyompenda Isaka. Lakini kwa ajili yako na yangu alimtoa. MUNGU ndiye anayetutunza, asubuhi hutoka kwake; Yeye ndiye aliyetuumba, tena tu kazi ya mikono yake. Hatuna budi kumpenda kuliko yeyote na kupita chochote. Itifaki ya upendo inadai MUNGU kwanza wengine baadaye. Si vema kujipenda zaidi kuliko kumpenda Mungu. Mpe kipaumbele asubuhi, mtukuze jioni, mtafakari usiku. Mzee Yohana anaeleza vizuri katika 1Yohana 4:10-11: “Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana.
“Unatakiwa kujipenda kiasi kwamba ikitokea nafasi ya kuumbwa tena uchague kuwa wewe katika rangi hiyo hiyo na urefu huo huo”
WEWE; Mara nyingi tumewakumbatia wale waliotuumiza na kutitirisha machozi kila uchwao, huko ni kukosa kujipenda; huwezi kumpenda jirani yako kama hujipendi. Huwezi kutoa usichonacho. Katika usanii wa hali ya juu ni pale ambapo asiyejipenda anajaribu kupenda, hahaha ni vituko! Kujichubua ngozi kwa vipodozi (kuji-cream) ni matokeo ya kutojipenda. Mtu anayetamani kwenda ulaya hata kuhatarisha uhai wake utadhani pamekuwa Mbinguni ni matokeo ya kutojipenda, binafsi natamani kwenda mbinguni kazi yangu ikiisha. Mungu ndiye aliyeweka mipaka, anasababu ya kufanya uwepo katika nchi uliyopo. Kutamani kuzaliwa mzungu badala ya Mtanzania au Mwana wa Afrika ni kutojipenda pia. Unatakiwa kujipenda kiasi kwamba ikitokea nafasi ya kuumbwa tena uchague kuwa wewe katika rangi hiyo hiyo na urefu huo huo. Usitamani kuwa fulani bali tamani kuwa wewe ambaye Mungu anataka uwe. Kujipenda ni kujikubali hata kama hujavaa nguo fulani, hujazaliwa familia fulani au hujaenda nchi fulani. Ninajipenda kiasi kwamba hujitoa katika mtoko wa jioni, najifurahia, najisemea mwenyewe na ninajiheshimu kabla mtu mwingine hajaniheshimu. Zingatia itifaki jipende tafadhali! Usipate hadhi au kupanda chati kwa sababu umevaa nguo fulani bali nguo ipate hadhi kwa sababu wewe umeivaa.
WAZAZI; Itifaki inataka tuwapende wazazi wetu. Biblia imewataja moja kwa moja kwamba, tunapaswa kuwaheshimu. Wazazi ni lango la baraka, anaweza asikupe mtaji wa biashara lakini maneno yake tu ni “dili”. Kumbuka Yakobo na Esau, walitaka haki ya mzaliwa wa kwanza ambayo hutolewa kwa maneno tu. Nakumbuka siku moja Baba yangu alinipigia simu akaniambia nitafanikiwa kwani, sijachukua cha mtu na nikaamini nitafanikiwa; Ukiniuliza kwa nini nitakujibu, ‘baba kasema’. Japo nasoma maandiko na najua jinsi Yesu alivyotufanikisha kwa Damu yake lakini sipuuzi Baraka ya wazazi. Mwalimu Mwakasege anaandika, “Ukitaka kujua mchumba wako ataishi muda gani angalia anachowatendea wazazi wake.” Sasa kama unataka kuwa mjane mapema si lazima kujua hili. Usisahau hili, heshima kwa wazazi huamua juu ya urefu wa maisha yako hapa duniani. Wasamehe wakikosa, wasikilize wakikuonya, wasaidie kila upatapo nafasi. Wapende.
“Je uko tayari kuvunja uhusiano wowote unaoharibu itifaki ya upendo katika ngazi ya Muumba wako? Je, unaweza kukaa mbali na huyo mtu anayekuwa chanzo cha kuharibu uhusiano wako na Mungu?”
JIRANI; ujirani si habari ya nyumba au ya kuishi mtaa mmoja. Ujirani ni nafasi ya kusaidia. Kila unapokuwa na nafasi ya kumsaidia mtu unafanyika jirani yake. Safarini kuna majirani, barabarani kuna majirani, ofisini kuna majirani, kanisani kuna watu huhitaji msaada pia. Ni ajabu kama hatutatambua hisia na mahitaji ya watu wengine na tukaendelea kujiita wakristo. Ukianguka barabarani ungependa watu wakutendee nini? Siku yako ya kuzaliwa ungependa watu wafanye nini? Ukiugua ungepende watu wachukue hatua gani?  Ukipata msiba ungependa watu wachukue jukumu gani? Ukishindwa masomo ungependa watu wazungumze maneno gani? Ukigombea nafasi ya uongozi na usiipate au ukakatwa, ungependa watu wanene maneno gani? Yale ambayo ungependa ufanyiwe basi watendee na wengine pia. Maneno ambayo ungependa kusikia, wasikilizishe na wengine pia na huo ndio ujirani.
ANGALIZO; Unajua itifaki inaweza kuvamiwa au kuingiliwa, wengine husahau na hivyo kushindwa kuzingatia itifaki. Mahali ambapo baba na mama wapo usianze kuwatambua mashemeji zako kwanza, mahali ambapo mwenyekiti yupo usianze kumtambua mweka hazini kwanza. Wengine hutambua vitu kabla ya watu na utu, wengine hutambua wapendwa wao kabla ya Mungu. Ibrahimu alikuwa tayari kumpoteza Isaka ilimradi itifaki ya kwamba Mungu ni Mkuu izingatiwe. Biblia inasema kidole chako kikikukosesha ukikate, Je uko tayari kuvunja uhusiano wowote unaoharibu itifaki ya upendo katika ngazi ya Muumba wako? Je, unaweza kukaa mbali na huyo mtu anayekuwa chanzo cha kuharibu uhusiano wako na Mungu?
Kuhani hupenda ibada, mwinjilisti hupenda mahubiri, manabii hupenda unabii; heshima ya nabii ni kutimia kwa unabii wake. Lakini Mungu hupenda watu hatulii hadi aone usalama wa viumbe vyake. Yona alivunja itifaki, alipenda unabii wake kuliko watu. Alisikitika kwa nini Mungu hajawaangamiza watu wa Ninawi kama alivyotabiri. Kwake yeye bora watu wafe ilimradi unabii utimie, kwa Mungu bora unabii ubatilike lakini watu waokolewe. Yona 4:1
Yesu alizungumza kwa habari ya kuhani aliyependa ibada kuliko utu. Alimwacha mgonjwa aliyevamiwa na wevi kwa sababu anawahi ibada, huyu naye hakujua itifaki ya upendo. Mungu kwanza, wewe na jirani ndio mnafuata; Karama na vitu huja baadaye, Haleluyah! Itifaki ya ki-kristo inatutaka tuwapenda adui zetu na tuwatakie mema hili nalo si jambo la kubezwa. Tafadhali itifaki izingatiwe na neno la BWANA lizingatiwe kwa vitendo.
Tukutane katika mbingu mpya na nchi mpya.
Naomba kuwasilisha.

2 comments :

  1. Mungu akubariki sana kwa ujumbe mzuri, wa kweli.
    Nimejifunza sana kutokana na kile umeandika.
    Mungu akubariki ja kukuongeza.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Tunashukuru ndugu, Endelea kufuatilia article zetu kila siku ya Ijumaa. Bwana Akubariki sana

      Delete