YEYE badala ya Wewe
“YEYE” BADALA YA WEWE
(Alikwenda kama mwakilishi, kwa ajili
yako)
Watu wengi wanaposoma biblia wanadhani
Adam na Eva walizeeka. Ukweli ni huu, walikufa mapema hawakuweza kudumu kabisa;
kwa jinsi ya mwili waliishi miaka mingi na kuzeeka, lakini kwa jinsi ya kiroho
walikufa mapema mno, kumbuka mtu ni roho, anayo nafsi na anakaa ndani ya mwili;
mtu sio mwili bali roho. Siku waliyotenda dhambi, ndiyo siku waliyokufa.
Ndivyo walivyoambiwa na Mungu na ndivyo ilivyokuwa. Hata sasa dhambi ni rafiki yake kifo, huwezi kwenda
matembezini na dhambi na ukamuacha kifo nyumbani. Hawa ni mapacha, siku
ya dhambi ni siku ya kifo. “walakini
matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula
matunda ya mti huo utakufa hakika.” Mwanzo 2:17
Siku mtu anapotenda dhambi ndiyo siku
anayokufa, uzima wa mwili unadanganya tu. Dhambi ni mbaya, mistari mingi katika
biblia inayotaja dhambi, inaitaja kwa kuiunganisha na kifo (soma Methali 6:32,
Warumi 6:23). Dhambi huoana na kifo. Kama ni msomaji wa biblia utakubaliana na
mimi kwamba, ndoa kati ya dhambi na mauti ni imara sawasawa na shetani na
kuzimu. Huwezi kutenda dhambi bila ya kukikaribia kifo. Hatua muhimu kuelekea
kifo ni kuanza kutenda dhambi. Yesu alikufa kwa sababu alichukua dhambi zetu,
mauti ilimpata kama mshahara wa dhambi zetu.
Mungu anachukia dhambi, chuki yake
dhidi ya dhambi ni dhahiri. Chuki ya Mungu dhidi ya
dhambi ni chuki ya milele. Dhambi zetu zilikusanywa mahali pamoja yaani, katika mwili wa Yesu Kristo.
Kama mtu akusanyavyo takataka au uchafu sehemu moja na kisha akauchoma moto, ndivyo uasi wa wanadamu wote ulivyokusanywa katika
mwili mmoja wa Yesu Kristo na kisha akafa msalabani kama fidia yetu. Maasi yote na uovu wote uliwekwa juu ya
mwili wake.
Yesu ni mwakilishi wetu katika mauti,
yeye badala yetu {vicarious death}. Badala ya sisi kwenda katika mauti yeye alikwenda
kwa niaba yetu. Watu maalumu wanaposhindwa kuhudhuria katika hafla fulani au
katika chakula cha jioni huteua wawakilishi wao. Ni rahisi kwa watu hawa wakuu
kumpata mwakilishi kwani ni suala la
kwenda kula na kunywa. Lakini akitafutwa mwakilishi atakaye kwenda kufa kifo
cha aibu kwa niaba yao, hakika hawezi kupatikana. Yesu hakutuwakilisha katika
hafla na karamu za raha na furaha, bali alituwakilisha katika mauti naamu mauti
ya msalaba na aibu. Alituwakilisha katika baridi, katika kukosa usingizi katika kuteswa na
kuvuja jasho la damu, na katika kulia sana.
Kwa kitambo kirefu tulihitaji
mwakilishi na hakupatikana, kwa nyakati tofauti tofauti nabii Isaya na Daudi
walitamani Mungu aje na afanyike mwakilishi wetu. Walisikika wakisema, “laiti
mbingu zingekuja duniani” au “laiti BWANA angepasua mbingu” walitamani kuona
kile kinachoitwa kwa kizungu, ‘Heaven on Earth.’ Yaani mbingu duniani
Ombi lao lilijibiwa pale Yesu alipokuja
duniani. Yesu ndiye ukamilifu wa mbingu dunian. Mungu pamoja nasi yaani, Mungu
katika maisha na ratiba za kwaida kabisa za mwanadamu. Yesu ndio mbingu zote,
badala ya kutazama mbinguni sasa tunamtazama Yesu aliyekuja na aliye mbingu
duniani (Emanueli).
Ili uwe mpatanishi ni lazima uzifahamu
pande zote zinazokinzana kwa uzuri wote. Ili uwe mkalimani ni lazima ujue lugha
zote mbili kwa ufasaha, Yesu aliijua lugha ya Mungu na ya wanadamu pia. Yesu
alimjua Mungu (alitoka kwa Mungu) lakini kwa kuwa alikuwa mwanadamu alimfahamu
vizuri mwanadamu. Alijua
namna Mungu anavyochukia dhambi (alikuwa Mungu) lakini alijua jinsi dhambi
inavyomtesa mwanadamu kwa kuwa aliishi kama mwanadamu. Aliona magonjwa, hali zao ngumu za kimaisha, aliona utawala wa giza na
utumwa wa dhambi. Kwa kuwa alizijua namna zote ndio maana hakulalamika kwamba
mateso yamezidi pale msalabani, kwani aliijua chuki ya Mungu dhidi ya dhambi.
Huwezi kujiandaa kufanya malipo kama hujui gharama au bei ya bidhaa.
Yesu alibatizwa ili aitimize haki yote.
Ubatizo wa Yesu ni muhimu sawasawa na kifo chake. Alikufa kwa ajili yetu,
alibatizwa kwa ajili yetu pia. Yesu hakuwa na haja ya kubatizwa, hata Yohana
alitaka kukataa kumbatiza. Ubatizo wa Yohana ulikuwa ni ubatizo wa toba, Yesu hakuwa na sababu ya kutubu,
hakutenda dhambi. Asiye na dhambi hana haja ya kubatizwa ubatizo wa toba. Lakini kwa ajili yako alibatizwa. “Wakati
huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na
wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi
sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.” Mathayo
3:13-15
Ubatizo ndio ulikuwa mlango pekee ambao
Yesu alipitishwa ili kuutwaa uovu wetu na kuitimiza haki yote. Pale mtoni
alikwenda kuchukua dhambi zetu, pale msalabani alikwenda kulipia deni lililotokana
na dhambi alizochukua pale mtoni-katika ubatizo. Ni baada ya ubatizo ndipo
yalinenwa maneno haya: “Siku ya pili yake
amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye
dhambi ya ulimwengu!”Yohana 1:29
Ni muhimu kujua kwamba tu wadhambi na
Yesu alituwakilisha katika kupokea mabaya. John Newton mtunzi wa wimbo wa
‘Amazing grace’ katika moja ya maandishi yake ameandika hivi: “mimi si mtu mwenye kuweza kukumbuka mambo yote lakini mambo mawili siwezi
kuyasahau kwa hakika kwamba, ‘mimi ni mdhambi mkuu, na Yesu Kristo ni mwokozi
Mkuu”. Ukweli huu ni muhimu kwa kila anayetaka kuwa karibu na
Yesu
Mtu mmoja amewahi kusema “katika matendo yote atendayo mwanadamu,
toba au kutubu ni tendo la Ki-mungu zaidi kupita yote.” Inawezekana kabisa
hujazaliwa mara ya pili au bado una dhambi zinatendeka kwa siri, hakuna anayejua
zaidi ya wewe; fanya uamuzi wa kuziacha leo, jikatalie ya dunia na ungana na
Yesu sasa. Alikufa kwa ajili yetu, hatuna budi kuishi kwa ajili yake 2Kor5:15. Kama
uko tayari basi tamka maneno haya kwa imani:
“BWANA YESU, NAOMBA UNIREHEMU MIMI
MWENYE DHAMBI. NINAAMINI KATIKA UBATIZO WAKO, NINAKIRI WEWE NI BWANA NA
NINAAMINI KWA MOYO KWAMBA, MUNGU ALIKUFUFUA KUTOKA KATIKA WAFU. NIPE NA ROHO
WAKO BWANA ILI ANIONGOZE DAIMA.” AMINA
Hongera kwa uamuzi uliofanya, usisite
kuwasiliana nasi kwa email au simu zetu, nasi tutazidi kukuombea na kukushauri.
MUNGU AKUBARIKI SANA.
0 comments :