Kuelekea Uhuru wa Kifedha
KUELEKEA UHURU WA
KIFEDHA
(THE BIBLICAL LAWS OF MONEY)
Tafiti mbalimbali zinaeleza kwamba, moja ya
changamoto kubwa ulimwenguni hasa bara la Afrika ni umasikini mkubwa wa kipato.
Ni ukweli unaosikitisha, na eneo hili ni moja ya maeneo ambayo hayana msisitizo
mkubwa ndani ya mwili wa Kristo (kanisa). Eneo la maarifa kuhusu fedha au
uchumi ili kumkomboa mtu kiuchumi ni kama limeachwa; Na kwa sehemu kubwa ukiona
mahali fedha inatajwa kanisani au kikundi cha sala basi ujue ni sadaka
inayozungumziwa. Ni watu wachache sana wanaozungumzia au kuhubiri au kufundisha
maarifa kuhusu fedha na uchumi ili kumuwezesha mtu kupiga hatua katika eneo
hilo kwenye maisha yake na jamii yake.
Jambo moja ambalo ni halisi na halikwepeki
ni kwamba, ili kuishi katika ulimwengu huu wa sasa kila mtu anahitaji fedha za
kutosha kumuweza kukidhi mahitaji yake na mahitaji ya wale wanaomzunguka. Kumbuka
fedha haina dini, haijali kabila wala rangi yako; haiwezi kuja kwako kwa sababu
wewe ni wa dini au dhehebu au rangi au kabila fulani (it is neutral). Na kwa sehemu kubwa, kiwango cha fedha au mafanikio
ya kiuchumi ya mtu yanategemea kiwango cha maarifa na ufahamu sahihi alionao juu ya kanuni za fedha
(The laws of money).
Nakumbuka siku moja wakati nipo sekondari niliwahi
kuhudhuria kikundi cha sala mahali
fulani, na siku hiyo tukafundishwa kuwa ili kufanikiwa kifedha basi ni
lazima tutoe sadaka ya kupanda ili makusudi tuvune mara mia kwa kigezo kwamba
ukitoa utapokea mara mia ya ulichotoa (bila shaka unakumbuka hilo andiko). Na tena
nikakumbuka lile andiko la kila apandacho mtu ndicho atakachovuna, basi
nikapiga hesabu zangu pale, kwamba endapo nitatoa elfu moja basi nitarajie
kupokea laki moja (bila shaka sijakuacha hata kama ulikimbia hesabu, elfu moja
mara mia ni laki moja). Sijui kama unaelewa maana yake nini upo sekondari
unatarajia kupokea laki moja ya kwako binafsi (hahahaha). Nikawaza tu nikiipata
hiyo laki moja napanda elfu kumi, sasa piga hesabu hapo elfu kumi mara mia,
mavuno ni kiasi gani? (tajiri mtoto anayechipukia).
Japo unaweza kucheka, inawezekana umewahi
kuwaza hivyo pia. Kanuni moja muhimu sana kuhusu fedha ambayo huwa haifundishwi
na leo nataka niigusie ni kanuni ya
uzalishaji bidhaa au huduma (The law of production). Pamoja na kwamba
sadaka na maombi ni muhimu sana kwa ustawi wa mtu; ni ukweli uliowaza kwamba
hakuna aliyefanikiwa kiuchumi kwa mambo hayo TU (bila uzalishaji huduma na
bidhaa) isipokuwa aliyepo upande wa kupokea. Wazo kuu tunalotaka ulipate kwa siku ya
leo ni kwamba, ukitaka kufanikiwa kiuchumi hauwezi kukwepa uzalishaji bidhaa au
huduma kwa namna moja au nyingine.
Nioneshe anayeuza bidhaa au huduma, nikuoneshe mtu atakayefanikiwa
kiuchumi. Zalisha huduma au bidhaa ambayo tunauhitaji nayo, na sisi tutakuwa
tayari kukupa fedha kwa kuipata bidhaa/huduma hiyo kwa sababu tunaihitaji na
hapo mafanikio ya kiuchumi yatakuwa dhahiri kwako.
Mungu ameahidi mvua ya Baraka, sio mvua ya
fedha. Mungu ameahidi kushusha Baraka kwenye kazi ya mikono yako, kapu lako na
chombo chako cha kukandia unga, mifugo yako, mazao shambani kwako, hakuna
mahali ameahidi kushusha fedha toka juu. [Kumbukumbu la torati 28:4-5, 8]. Kusubiri
mavuno ya sadaka uliyopanda tangu mwaka juzi ili utoke kwenye mkwamo wa
kiuchumi uliona sasa, ni uvivu wa kufikiri, na ni kukosa uwajibikaji
(irresponsibility).
There’s a place for you at the top!
0 comments :