Roho ya Batromayo Kipofu
ROHO YA BATROMAYO KIPOFU
“ONA FURSA”
Batromayo aliona watu kama miti. Watu wengi
wanasumbuliwa na roho hii hawaoni picha halisi, picha yao haijatulia. Ni kama
vile ungo wao wa kudakia mawimbi haujatulia, hawapati picha halisi. Ni muhimu
sana mwaka huu 2018 sote tumuombe Mungu afungue macho yetu tuweze kuona fursa!
Kwa uzoefu mdogo nathubutu kusema, “fursa
haziwezekani bila imani”. Macho ya mwili hayotoshi, ile kwamba macho yetu
yanaona taa za barabarani na tunavuka salama haina maana kama tunaona fursa
pembezoni mwa barabara. Mtu anayeweza kufikiri kimkakati “strategic thinking”
anaweza kuona fursa na kuzitumia. Kufikiri kimkakati kutakuwezesha uone miaka
kumi ijayo na zaidi.
Kwa kukosa imani watu hauza mambo ambayo
baadaye yangekuwa fursa kubwa, kwa uhaba wa imani watu huogopa kuanza jambo
ambalo halijazoeleka. Anayewekeza miaka mia moja ijayo anaamini kwamba, Mungu
atamlinda na kumpa uhai, ndani yake mtu huyo hamna hofu ya kifo. Fursa inataka imani katika sura tatu,
kwanza mwamini Mungu muumba wako, jiamini na kisha amini wazo lako. Adui mkubwa wa fursa ni hofu, uwekezaji
unakwenda na ujasiri.
Zamani walituambia, “wasiwasi ndio akili”
si kweli. Nenda msituni utagundua mnyama mfalme wa msitu ni simba ambaye ni
mnyama jasiri. Njoo duniani utagundua mataifa makubwa yana ujasiri mkubwa pia. Alisema msemaji wa Marekani wa mambo
ya nje wakati huo John carry, “Dola ya Washington haitatikisika” alisema hayo
kwa ujasiri sana akionya taifa moja alilolitazama kama adui. Hatuna sababu ya
kuogopa amesisitiza Shiv Khera katika kitabu cha, Unaweza Kushinda: “Losers want security, winners seek
opportunity. Losers more afraid of life than death…”.
Tunawezaje kuona fursa? Maana kama
hatukuijua fursa kabla ya kukutana nayo, siku ikitokea tutaiona kama mkosi. Lazima
ujifunze kuhusu fursa na uzifahamu ili siku ukikutana nayo uitambue kirahisi.
Wewe si tajiri ila jitahidi usome kuhusu utajiri. Leo wewe si mfanya biashara
lakini jitahidi kusoma na kujifunza kuhusu biashara. Soma wasifu wa wafanya
biashara kama; Mohamed Dewji, Warren Buffet, Reginard Mengi, Ratan Naval Tata,
Alhaji Dangote, Said Bakhresa na wengine wenye ushawishi kwako.
Watu wengi wanapenda kushinda ila ni
wachache tu ambao wanapenda maandalizi kwa ajili ya kushinda. Fursa zinakutaka
ufanye maandalizi. Wewe ndiye unapaswa kuisubiri fursa kwani fursa haina nafasi
ya kumsubiri mtu! Fursa huja kwa waliojiandaa. Preparation is the Key!
Sala: Ee Mungu Baba Muumbaji wetu,
utufungue macho ili mwaka huu 2018 sote kwa umoja wetu tuweze kuona fursa.
Katika Jina la Yesu Nimeomba. Amina.
Usisite kutuandikia kwa anuani yetu kwa
maoni, ushauri na maombi. Barikiwa!
0 comments :