Usijihurumie; Fanya kazi
USIJIHURUMIE
Fanya kazi
Kama kuna mtu
ambaye angestahili kukaa na kutokufanya shughuli yoyote basi ni malkia wa
Uingereza na familia yake, Elizabeth II mwenye miaka 90 sasa. Nina hakika wewe
si wa kifalme kama yeye na familia yake, lakini huenda watoto na wajuu zake,
wanawajibika zaidi kuliko wewe. Wanajishughulisha na kujihatarisha kuliko wewe.
Katika ukoo wake wako wanaorusha ndege, wako waliokaa jeshini muda mrefu. Wana
kila kitu lakini bado wanachagua kazi na uwajibikaji. Prince Harry amekaa miaka
kumi katika vikosi vya jeshi. Watoto wa watawala wengi wangetamani kuwa
barabarani kila siku na magari ya kifahari, labda na kujihusisha na porojo za
mitaani. Sivyo ilivyo kwa jamaa ya Elizabeth II.
Kazi ni
heshima, tena kazi ni baraka. Mungu aliumba kazi kabla hata Adamu hajafanya dhambi,
kwa hiyo kazi haina uhusiano na laana, kazi ilikuja kabla ya laana, Adamu
alipangiwa kazi ya kulima na kutunza bustani kama sehemu ya baraka. Kula kwa
jasho kulikuja baadaye sana, kukakomeshwa na msalaba wa Kristo. Mwanzo 2:15
Kanuni ya kazi
inakutaka uanze na ulichonacho. Kama ni nguvu zitumie, kama ni pesa tumia kama
mtaji, hakuna kichache kisichotosha kuanzia. Wote huanza kwa hatua moja. Mtaji
wa masikini si nguvu zake tu, ni pamoja na akili zake mwenyewe. Kama umekaa
muda mrefu bila kupata kazi unaweza kuwasaidia ofisi iliyojirani na nyumbani
kwenu, ili kama hawakulipi kiasi chochote urejee kula chakula cha nyumbani.
Unaweza kujiunga pia na masomo ya bodi, ni rahisi kwa mtu anayesoma masomo ya
bodi kupata kazi kwa urahisi kwa kuwa anakuwa masomoni, akili yake hukumbuka
mengi na huwa na ujuzi unaofanana na wakati halisi.
Malkia ambaye
kimsingi anapata pesa nyingi kutoka serikali yao na angepaswa kukaa tu lakini
bado anafanya yafuatayo kama yalivyoripotiwa na gazeti la Business Insider UK;
“Alitimiza matukio 341 yaliyoko kwenye kalenda yake ya mwaka 2015 , analea
vituo 600 vya misaada (charities) na yeye na timu yake wanajibu barua laki moja
kwa mwaka wanazoandikiwa kutoka kwa watu mbalimbali.”
Maswali ya
kujiuliza, Je, unaratiba ya siku? , Je, unaratiba ya mwaka? Unaweza kupanga
mipango yako kwa miezi sita ijayo na ukatimiza? Kama hauna ratiba maana yake
hauna sehemu ya kujipima (benchmark). Kosa la kuishi siku moja bila tathmini
linaweza kupelekea kuishi mwaka mzima bila tathmini. Mtume Paulo alitathmini
mpaka maana na muda wa kwenda kanisani.
Si kila anayekwenda kanisani anakwenda kukusanyika kwa faida. Kama unakwenda
kanisani na haujengwi maana yake unabomolewa ama kiroho au kifikra.
Kuishi kwa
ratiba ni kazi ngumu, hakutoi nafasi ya matukio ya mwendokasi. Ratiba inabana
na hivyo wengi wanaona kuliko kibano cha ratiba ni bora waongozwe kwa matukio.
Twende pamoja kwa vitendo, chukua karatasi na kalamu. Andika nini utafanya kwa
siku ya kesho, kabla ya kulala hiyo kesho ujitathimini. Andika utakachofanya
kwa wiki, mwezi hata mwaka. Weka tathmini ya wiki katikati ya wiki (Jumatano),
tathmini ya mwezi katikati ya mwezi (tarehe 15) na mwisho wa mwezi, na tathmini
ya mwaka iwe kila baada ya miezi mitatu (kila baada ya robo).
Mwenye hekima
hufanya kazi hata kama mfukoni anapesa nyingi, asiye na hekima hufanya kazi kwa
sababu pesa zimeisha mfukoni. Mahitaji ya siku hayapaswi kukupeleka kazini,
bali mahitaji ya muda mrefu.
Mwenye hekima
huenda kwa ratiba na kalenda, mjinga hajui hata tarehe.
Mabadiliko
yanawezekana kabisa. Wewe ni baraka.
0 comments :