Jambo muhimu katika maisha
Mafanikio katika jambo lolote kwenye maisha
ya mtu si jambo la bahati nasibu; mafanikio huja kama matokeo ya kufuata au
kutekeleza kanuni muhimu katika maisha ya mtu. Jambo moja wapo muhimu (kanuni)
katika maisha ya mtu ili kufikia kilele cha mafanikio yake ni kujijengea tabia
ya kujitathimini mara kwa mara ili
kupata fursa ya kuona kama kile unachokifanya au kiwango cha maisha unayoishi
ni sawa na kile ulichopanga au kutarajia.
Mwenyehekima mmoja amewahi kusema, maisha
yasiyokuwa na kujitathimini ni maisha matupu (void). Si watu wengi wamejijengea
tabia hii ambayo ni kanuni muhimu sana ili kufikia mafanikio halisi katika
jambo lolote. Nioneshe mtu
anayejitathimini mara kwa mara, nikuoneshe mtu anayefanikiwa katika njia zake.
Mfano mzuri wa kanuni hii muhimu katika
maisha ni habari ya mwana mpotevu, ambaye aliishi maisha nje ya kile alichokusudiwa
mpaka pale alipoamua kufanya jambo muhimu la kutathimini aina na kiwango cha
maisha aliyokuwa anaisha. Kumbuka kila
kitu huwa sawa mpaka pale umesimama na kujitathimini. (Luka 15)
Kujitathimni kunatoa fursa muhimu sana
katika maisha katika maisha ya mtu. Kujitathimini kunaweza kufanyika wakati
wowote ule, mwanzo wa mwaka au mwisho wa mwaka au katika ya mwaka au kila mwezi
kulingana na malengo uliyojiwekea na mazingira uliyonayo. Kujitathimini kuna
faida nyingi ikiwemo faida saba (7)zifuatazo:
i. Kujitathimini kunakupa fursa na kuamsha
(renew or rejuvenate) hamasa (passion) na kukupa nguvu katika kile ulichokuwa
unafanya au kuchukua hatua katika kile unachotakiwa kukifanya ili kufikia
kilele cha mafanikio katika jambo husika.
ii. Kujitathimini kunakupa fursa na nafasi ya
kuangalia malengo na vipaumbele vyako ili kuona kama vinaendana au
vitakufikisha katika mafanikio unayoyatazamia.
iii. Wakati mwingine kujitathimini kunakupa
fursa ya kujitambua zaidi na kuanza upya ili kujinasua mahali ulipokuwa
umekwama.
iv. Kujitathimini kunakupa nafasi ya kuona
rasilimali na fursa (opportunities) zinazokuzunguka ili upate kuzitumia na kukufikisha katika malengo makuu.
v. Kujitathimini kunakupa nafasi ya kuziona
fursa badala ya vikwazo katika changamoto au mazingira uliyonayo.
vi. Kujitathimini kunakupa fursa ya kutambua ni
maeneo gani unayohitaji msaada (assistance) na mahali pa kupata msaada huo ili
kukuwezesha kufikia malengo yako.
vii. Kupata fursa ya kuona kama kile
unachokifanya au kiwango cha maisha unayoishi ni sawa na kile ulichopanga au
kutarajia
Njia thabiti ya kujitathimini katika jambo
lolote ni kwa kujiuliza maswali muhimu. Hii itakupa fursa ya kuona aina na kiwango
ulichopo au mwenendo wa jambo husika; yafuatayo ni baadhi ya maswali muhimu
unapojitathimini hasa katika kuangali aina na kiwango cha maisha uliyonayo sasa
(Kiroho, kibiashara, kifamilia,kiuchumi,
kiofisi n.k):
i. Hivi ni kwanini naishi maisha ya namna hii
kwa sasa? Je ningependa kuendelea na maisha haya hadi nitakapozeeka ama nataka
kubadilika? (kutoka kitabu cha Timiza
Malengo yako, Joel Nanauka)
ii. Je hivi aina na kiwango cha maisha
ninayoishi ni sawa na kile nilichopanga au kutarajia (plan)
iii. Je hiki ninachokifanya kinachangia katika
kufikia malengo yangu ya kimaisha?
iv. Je ni jambo gani naweza kufanya ili
kuongeza ufanisi na ubora katika kile ninachokifanya? Kitu gani naweza
kuboresha zaidi ili kutoa huduma au bidhaa bora zaidi ya sasa?
v. je, kwa sasa nikichukua maamuzi gani
yatakuwa ni mwanzo wa mabadiliko katika
maisha yangu? Mfano: kutoka katika mahusiano, kuomba msamaha, kutafuta kazi
nyingine, kujiunga na shule/kozi n.k (kutoka kitabu cha Timiza Malengo yako, Joel Nanauka)
“There’s a
place for you at the top”
0 comments :