Jambo muhimu katika maisha - II

5:43:00 PM Unknown 0 Comments

 
  JAMBO MUHIMU KATIKA MAISHA - II
Juma lililopita tuliangazia umuhimu wa kujijengea tabia ya kujitathimi mara kwa mara ili kupata fursa ya kuangalia au kuona kama aina au kiwango cha maisha anayoishi mtu; au muelekeo wa jambo fulani (kibiashara, kiroho au kikazi) ni sawa na matarajio (inavyotakiwa kuwa) yake au la! Mwenyehekima mmoja anasema, “Kama tutajitathimini juu ya aina au kiwango au uelekeo wa jambo lolote katika maisha yetu; lakini tusichukue hatua katika kile tulichojitathimini, muda utapita lakini kesho tutakuwa pale pale tulipokuwa jana na hivyo tutakuwa tumepoteza muda bure”.
Lengo la kujitathimini sio kujisikia vibaya au kuwa na hatia au aibu kwa mahali tulipo, bali kupata fursa ya kupiga hatua ili kesho tusiwepo mahali tulipokuwa jana au tulipo leo. Kama mwana mpotevu angejitathimini bila ya kuchukua hatua ya kutoka mahali alipokuwa kama matokeo ya kujitathimini kwake, basi kujitathimini kwake kusingeleta badiliko lolote katika maisha yake. Kumbuka, hakuna jambo hubadilika lenyewe. Mpaka umechukua hatua dhabiti, kutamani kuwa na mbadiliko pekee hakutabailisha kitu.
Mambo mawili nataka nikuhimize katika mapumziko ya mwisho wa wiki hii:
i. Chukua hatua kwa kuanza kujitathimini kwanza, kusoma ujumbe huu pekee hakutoshi; tunatamani kuona badiliko la kweli katika maisha yako, tunatamani kuona unafikia malengo yako na kilele cha mafaniko yako. Ndio maana tunakuhimiza chukua hatua, tafuta muda wa kujitathimini, zima redio, weka simu mbali, zima TV, acha ‘kuchat’ na ujitathimini. Kumbuka TV, Internet na Redio hufanyakazi masaa 24, hakuna siku watazima ili kukupa fursa ya kujitathimini; kila siku utasikia “mpenzi mtamaji/msikilizaji endelea kuangalia/kusikiliza kipindi kinachofuata”, hata kama ni saa nane usiku bado watasema endelea tu.
ii. Chukua hatua kwa kufanyia kazi matokeo ya tathimini yako kwa kuzingatia maswali muhimu ya kujiuliza yaliyopo kwenye toleo lililopita. Swali moja wapo lilisema: je, kwa sasa nikichukua maamuzi/hatua (actions) gani yatakuwa ni mwanzo wa mabadiliko katika maisha yangu? Mfano: kutoka katika mahusiano, kuomba msamaha, kutafuta kazi nyingine, kutafuta mshauri mwenye hofu ya Mungu anishauri, kujiunga na shule/kozi n.k!
Mwenyehekima mmoja anasema, “Watu hawafanikiwi kwa sababu wana mawazo mazuri; bali kwa sababu wanayafanyia kazi kwa wakati” Kufanya tathimini pekee hakutoshi, chukua hatua na kuyafanyia kazi kwa wakati ili kupata matokeo yaliyo bora zaidi.
There’s a place for you at the top

0 comments :