Mimi ni mchezaji wa timu ile

2:16:00 PM Unknown 0 Comments

 
MIMI NI MCHEZAJI WA TIMU ILE.
(I belong to a winning team) 
Kwa mfano huu jifunzeni. Lauden alikuwa mchezaji mahiri wa timu yake ya kidato cha tano, alijituma sana na kujizuia ili kufanikisha ushindi. Siku moja kabla ya fainali Lauden alilala mapema ili kupata muda mwingi wa kupumzika na kujiandaa na fainali. Baadhi ya wanatimu walikwenda disko kucheza muziki na hivyo walichelewa kulala, wengine walikwenda mitaani katika mambo ya uasherati na ulevi. Licha ya bidii na juhudi za Laudeni katika kujikatalia anasa na kulala mapema bado timu yao haikufua dafu. Juhudi za Laudeni hazikufua dafu, timu yake ilishindwa mbele ya mahasimu wao. Ingawa Laudeni alionekana kuwa mchezaji wa kipekee katika mchezo, bado hakuweza kuisaidia timu yake kushinda.
Wapinzani wao hawakuwa na vipaji vikubwa, ila walikuwa na umoja. Wapinzani wao walizingatia maelekezo na kufanya inavyowapasa kwa pamoja kama timu. Wapinzani wao walielezea kuwa siri ya mafanikio yao ni umoja na ushirika katika mazoezi na mtazamo.
Timu nyingi hazifungwi kwa sababu ni mbaya, bali ni kwa sababu ya utengano. Tunaweza kuwa na umoja ndani ya uwanja na utengano nje ya uwanja hii nayo haifai. Utengano katika mtazamo, maneno na matendo ndio chanzo cha kushindwa. Umoja ni muhimu uwanjani na nje ya uwanja. Mhubiri mzuri haonekani jukwaani bali nyumbani. Ni nje ya uwanja ndipo hutoa jibu la kinachoonekana uwanjani.  Kwa wanafunzi muda wa likizo ndio unaoamua ushindi, ni muda ule ambao mwalimu hajakupangia jambo la kufanya.
Timu ikishinda ushindi ni wa kila mtu, na ikifungwa basi ni wote wameshindwa wala si mlinda mlango peke yake. Ushindi ni jambo la pamoja. Si sahihi kwa mwanatimu kufikiri anaweza peke yake wala si sahihi kwa mwanatimu kufikiri kwamba hana mchango wowote. Tamko la timu ni bora kuliko tamko binafsi
John Maxwell ambaye ni mwalimu mzuri wa uongozi anasema, “moja ni namba ndogo sana kufanya mambo makubwa.” waswahili nao wanasema, “kidole kimoja hakivunji chawa.” Wote wanasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja na kwa umoja kama timu. Biblia inasema, wawili ni bora kuliko mmoja, tena inasisitiza kwamba, Si vema mtu awe peke yake ndio maana akamfanyia msaidizi.
Utengano hutokea pale mmoja anapoacha kutimiza wajibu wake. Timu haifungwi kwa sababu nafasi zote zimeyumba la hasha! Bali ni kwa sababu nafasi fulani imeyumba. Inawezekana ikawa ni nafasi ndogo lakini ndio chanzo cha kuyumba kwa timu. Kila mchezaji ni muhimu katika timu. Oral Robert katika moja ya vitabu vyake anaelezea umuhimu wa mgawanyo wa kazi kwa kuzingatia karama na talanta za mwanatimu. Oral anamnukuu rafiki yake Bob De Weese aliyemwambia maneno haya; “Oral, you be there to preach and pray, and your team will do the rest.
Kwa nini tunapungukiwa baadhi ya mambo maishani mwetu? Moja ya sababu ni ili tujue kwamba mwanadamu ni kiumbe wa mahusiano. Katika kuhusiana na wanatimu, wanajumuiya na wanajamii wengine anakamilika. Timu ni muhimu, mizizi ya timu huenda mbali kuliko juhudi za mtu mmoja, bila ya timu tunaweza kukamilisha kazi kidogo. Yesu alikuwa na wanafunzi wake, Paulo alikuwa na Timotheo na Tito, Sauli alikuwa na Daudi na nabii Nathani. Vipi uko na nani? Bill Gates na Hayati Steve Jobs walikuwa na timu zao za ushindi. Nina amini hata Dangote na yule Strive wa Kwese Tv wana timu zao za ushindi.
Si rahisi mtu asiye na timu na ushirika na watu wengine akawa na ushirika na Mungu. Kuna nyakati ambazo kuwaacha watu maana yake ni kumwacha Mungu. Si kila asiye na kikundi ni wa kiroho. Mwezi uliopita tuliandika andiko fulani, tuliowaandikia walituuliza kama tunafanya kazi kama timu au lah! Tunamshukuru Mungu tunafanya kazi kama timu ya, Life Minus Regret Team, tazama wasifu wa timu yetu (team profile) katika: www.lifeminusreget.blogspot.com
Jisikie furaha kuwa sehemu ya timu fulani, usharika fulani, jumuiya fulani au kanisa fulani. Televisheni si kanisa, lengo lake ni kuwaleta watu kanisani na si kuwaacha sebuleni na rimoti zao. Unahitaji kukutana na watu waaminio kwa ajili ya ibada, kumega mkate na kuwajua wahitaji wanao hitaji msaada wako.
Endelea kuifurahia timu yako ya ushindi. Barikiwa!!!

0 comments :