Malezi ni mkataba mrefu
(Ni zaidi ya miaka 18)
Mwanadamu ni kiumbe anayekaa katika
utegemezi kwa muda kuliko watoto wa viumbe wengine. Viumbe wengine hulea watoto
wao kwa miezi sita au mwaka mmoja na kisha huwaacha wakaendelee na maisha yao.
Ndege hukaa na makinda yao kwa miezi mitatu,
wako wanyama wengine hukaa na watoto wao kwa kipindi ambacho ni chini ya mwaka
mmoja. Lakini sivyo ilivyo kwa binadamu. Malezi ya mtoto ili mtu awe mtu kamili
yanachukua zaidi ya miaka 18. Fikra za kupata mtoto lazima ziende mbele angalau
kwa miongo miwili (miaka 20). Mtoto wa binadamu anakaa nyumbani kwa zaidi ya
miaka 18 akiwa bado ni tegemezi. Wako wenye miaka zaidi ya 30 na wanalishwa na
kutunzwa na wazazi wao. Malezi ni zaidi ya chakula na dawa. Ni kuadabisha na
kufundisha utu wema. Mith 21:6
Mkataba wa kupata mtoto hautakiwi kuwa wa
usiku mmoja, mkataba wa kupata mtoto unapaswa kuwa mkataba unahusishwa elimu,
utu, makuzi, na hatma ya mtoto kwa mioungo isiyopungua miwili. Uamuzi wa kupata
mtoto ni lazima uwe ni mkataba wa milele, au uwe mkataba wa zaidi ya miaka 18.
Wenye utayari wa kupata mtoto lazima wawe na utayari wa malezi ya pamoja kwa
zaidi ya miaka kumi na nane. Kifo ndio sababu rasmi sana ya kibiblia ya kumfanya
mtu alelewe na mzazi mmoja, japo kijamii ziko sababu nyingi.
Pamoja na changamoto zote za malezi, mzazi
mmoja au wawili bado kulea ni kuzuri kunampa mzazi au mlezi nafasi ya kukijenga
kizazi kinachofuata. Katika ujenzi wa Taifa, familia ni sehemu ya kwanza na ya
msingi. Shule ya familia inatajwa kuwafanikisha
wengi kuliko vyuo vikuu.
Shule ya familia ikikosewa inaweza
kuwafelisha wengi kuliko wanaofeli katika madaraja mbali mbali ya elimu.
Familia isipowajenga watoto kwamba matatizo yapo, basi watakapo kutana nayo
watakata tamaa. Familia isipoamini katika uwepo na uhusiano na Mungu, basi
watoto wataabudu vitu ambavyo kwa asili si Mungu.
Watoto wasiojengwa katika ibada wanaweza
wasimwabudu shetani badala yake wakaabudu kazi, fedha, sinema na michezo.
Rafiki yangu alipenda ibada kiasi kwamba alikuwa hakumbuki ni lini hakuudhuria
ibada kanisani, lakini tunao vijana wengi ambao hawakumbuki ni lini walikwenda
kanisani. Makosa haya ni ya mfumo wa malezi.
Malezi ni jambo la pamoja mzazi hatoshi
peke yake wala hapaswi kufikiri kwamba anatosha. Ndio maana Mungu amwetuwekea
kanisa. Kanisa ni jumuiya ya waaminio ambapo ndani yake kuna walimu,
wainjilisti, wachungaji, mitume, manabii na watu wenye matendo ya miujiza.
Mtoto ni wa Mungu kwanza, wa wazazi na baadaye wa jamii yote.
Hitler kabla ya kuwa muaji alikuwa mtoto,
Iddi Amini wa Uganda kabla ya kuwa dikteta alikuwa mtoto. Mtoto ni kama
karatasi nyeupe isiyo na kitu chochote, mwandishi wa awali ni Mungu na baadaye
wazazi wanapata nafasi ya kuandika upendo au ugaidi, amani au chuki, uvumilivu
au kisasi. Mithali 21:6
0 comments :