Wito binafsi
(Umeitwa kwa jina lako)
Wakristo,
wanafunzi, wachungaji, waimbaji, wainjilishaji, wafanyakazi, wataalamu,
wanaharakati n.k, ni majina ya vikundi ambayo hayatoi wajibu mkubwa kwa mtu
binafsi. Ukweli ni kwamba wito ni ile sauti inayokuhamisha kutoka katika
kikundi fulani, nchi yako, mipango yako binafsi na hata katika mwelekeo
binafsi.
Wito
si jambo jepesi, unaweza ukuleta usumbufu. Wito unahitaji aliyeitwa awe shupavu
katika kukata kona (kuitikia wito),
awe na uwezo wa kugeuka haraka. Pale mwanafunzi anapoteseka miaka zaidi ya
mitano katika masomo yake ili awe daktari na baadaye sauti ya Mungu inamwita
katika mwelekeo mwingine tofauti na udaktari, kunahitajika ushupavu na usikivu.
Pamoja na kuwepo kwa gharama ya usumbufu, wale wanaotii sauti ya Mungu baadaye
hufurahi na kufaidika.
Kuna
wito ambao Mungu anamwita kila mtu, wito huu huhusisha aina na mtindo wa maisha
tunaopaswa kuenenda nao hapa duniani. Uko wito wa kuishi maisha matakatifu, uko
wito wa wokovu uko wito wa kumfuata Yesu yaani ufuasi. Wito wa ujumla haubagui
kila mtu lazima aitikie sauti hiyo.
Katika
makala hii ninalenga wito wa kipekee, wito ambao hauhusishi mke wala mume,
hauhusu kikundi fulani cha watu bali unahusu mtu binafsi. Ameandika mchungaji
mmoja, “Yuko wapi mke wa Petro?” Hatutazamii kumuona mwingine katika wito wako
bali wewe peke yako. Ibrahim aliacha nchi, baba na nduguze kwa ajili ya
wito. “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni
wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa
nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.” Yohana 21:15
Yesu
alimwita Petro kwa jina, na alimpa kazi kwa jina. Alimwita mara tatu kwa jina
lake. Badala ya kusema mitume alisema, Simoni Petro lisha kondoo zangu, Baadaye
akamtaja kwa jina kwamba, achunge kondoo zake.
Watu
wenye wito wa pekee mara nyingi wanashangaa kwa nini hawasaidiwi au kupunguziwa
mzigo, mara nyingi wanajiuliza, “kwani watu wengine hawaoni umuhimu wa jambo
hili?” Yesu alipokuwa akiomba alishangaa mitume wake wakilala usingizi,
alijaribu kuwaamsha mara kadhaa lakini bado walilala. Ninaamini ni kwa sababu
wito wa wokovu si wa kwao, ulikuwa ni wa Yesu Kristo peke yake. Kwenye familia
kunaweza kukawa na watoto wengi lakini si wote wanakuwa na mzigo wa kuwasaidia
ndugu na jamaa, mara nyingi mzigo wa kusaidia wazazi na ndugu unaweza
kumwangukia mmoja. Mwenye mzigo huo (wito wa kusaidia) huwa anatamani apate
msaada na mara nyingi haiwi hivyo kwa kuwa ameitwa kwa jina lake.
Ili
kijana afanikiwe ni muhimu ajue wazi kwamba kati ya vijana bilioni 1.8 waliopo
duniani ni yeye tu ameitwa tena kwa jina lake. Ili mtu mwenye wito wa pekee
afanikiwe ni lazima ajue kwamba katika dunia hii yenye watu bilioni nane
ameitwa peke yake, tena kwa jina lake. John Wesley akitambua hili alisema, “Naona
dunia nzima kama parokia yangu”.
Endelee kubakia kilele…..mpaka wiki ijayo shalom.
0 comments :